JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


NAPE ATOA NENO UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA, ASISITIZA NCHI ZA NJE KUIHESHIMU TANZANIA KWA UHURU WAKE

Share This
Na Janeth Raphael MichuziTv Bungeni - Dodoma

Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuhakikisha inazikumbusha nchi za nje kuheshimu uhuru wa Tanzania, akisisitiza kuwa taifa hilo halipaswi kudhalilishwa wala kunyanyaswa katika ushirikiano wa kimataifa.

Akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni leo  jijini Dodoma, Nape amesema Tanzania iko tayari kushirikiana na mataifa mbalimbali duniani, lakini msingi wa ushirikiano huo ni kuheshimiana na kulinda heshima ya kila upande.

Amesema baadhi ya nchi rafiki zinapaswa kukumbushwa kuwa Tanzania ilipata uhuru wake kupitia mapambano makubwa ya wananchi wake, hivyo uhuru huo haukupewa kama zawadi bali ulipiganiwa na kulipiwa gharama kubwa, jambo linalopaswa kuheshimiwa katika mahusiano ya kidiplomasia.

“Marafiki zetu waje, lakini watuheshimu na wasitumie changamoto tulizonazo kutunyanyasa, kutukandamiza, kutuonea au kutudhalilisha. Watumie fursa tulizowapa kushirikiana nasi kwa heshima, nidhamu na upendo,” amesema Nape bungeni.

Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano wa muda mrefu na mataifa mbalimbali duniani, na changamoto za muda hazipaswi kuathiri au kuvunja misingi ya ushirikiano huo, bali zinapaswa kushughulikiwa kwa njia ya kidiplomasia na mazungumzo ya heshima.

Aidha, Nape amesisitiza kuwa historia ya Tanzania imejengwa na Watanzania wenyewe, hivyo ni wajibu wa wananchi na viongozi kulinda heshima ya taifa kwa wivu mkubwa na kutoruhusu taifa kudhalilishwa, kuonewa au kutumika kama sehemu ya kushinikiza kisiasa kutokana na changamoto za ndani au za kimataifa.

Aisha Nape  ameiomba  Wizara ya Mambo ya Nje kuendelea kuwakumbusha washirika wa kimataifa kuwa mataifa yote, makubwa kwa madogo, yako sawa katika misingi ya kidemokrasia na ushirikiano wa kimataifa, hivyo yanapaswa kushirikiana kwa staha bila upendeleo wala shinikizo.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa yote duniani bila kufungamana na upande wowote, ikiwa ni sehemu ya sera yake ya diplomasia ya usawa, heshima na manufaa kwa pande zote.

Kauli hiyo ya Nape imekuja wakati Bunge likiendelea kujadili bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, huku wabunge wakitoa maoni kuhusu namna Tanzania inavyopaswa kuimarisha nafasi yake katika medani ya kimataifa.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad