JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


KIHONGOSI: CCM YAPOKEA RIPOTI YA JAJI CHANDE KWA UZITO, YASISITIZA MARIDHIANO.

Share This

 Katibu wa NEC Itikadi, Mafunzo na Uenezi CCM Taifa, Kenani Kihongosi, amesema chama hicho kimepokea kwa uzito mkubwa ripoti ya Tume ya uchunguzi wa matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, 2025, akieleza kuwa imelisaidia Taifa na imefanya kazi kwa uzalendo na weledi mkubwa.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Mei 4, 2026, amesema CCM inaamini njia sahihi ni maridhiano na inalenga kuhakikisha Taifa linakuwa moja, pia amesisitiza umuhimu wa kuundwa kwa Tume ya upelelezi ili kubaini waliohusika na kuwawajibisha kuhusu matukio hayo.

Amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda tume hiyo pamoja na Mwenyekiti wa Tume, Jaji Othman Chande, kwa kufanikisha uchunguzi huo.

Akizungumzia suala la Katiba mpya, amesema ni ajenda ya CCM kupitia ilani yake ya mwaka 2025–2030 na inapaswa kupatikana, ameeleza kuwa tangu miaka ya 1980, CCM imekuwa ikifanya mageuzi ya mara kwa mara ya maboresho ya sheria ili kuendana na mahitaji ya jamii.

Amesisitiza kuwa Katiba si mali ya chama chochote cha siasa bali ni mali ya wananchi na inabeba masuala mengi sio ya ajenda ya uchaguzi pekee.

Ametoa wito kwa makundi yote ya jamii kushiriki katika maridhiano, akieleza kuwa taifa haliwezi kujengwa kwa kutumia nguvu na kwamba mageuzi ya kweli yanahitaji majadiliano yenye nia njema na kufuata misingi yake.

Amewataka Watanzania kuepuka vurugu na badala yake kujadili na kufikia mwafaka, amewakumbusha vijana, hasa wasomi, kutojihusisha na vitendo vya fujo na kuzingatia umuhimu wa elimu.

Ameongeza kuwa wanaochochea vurugu mara nyingi si vijana, na endapo uharibifu wa miundombinu kama ya elimu utatokea, waathirika wakubwa watakuwa ni vijana wenyewe, hivyo amesisitiza umuhimu wa kupima hoja kwa makini na kudumisha amani ya nchi.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad