
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
KATIKA ghala moja la kuhifadhi mazao nchini Tanzania, mfumo wa kielektroniki unapiga kengele. Dakika chache baadaye, ujumbe unaingia kwenye simu ya msimamizi wa ghala ukionya kuwa kiwango cha joto na unyevunyevu kimeanza kufikia mazingira yanayoweza kuzalisha sumu kuvu kwenye mahindi yaliyohifadhiwa.
Onyo hilo halihusu moto wala uvamizi wa wahalifu. Linaashiria uwepo wa mazingira yanayoweza kuchochea kuzalishwa kwa sumu kuvu kwenye mazao ya chakula.
Ingawa mazao kama mahindi, mtama na karanga ni sehemu ya chakula cha kila siku kwa mamilioni ya Watanzania, si wananchi wote wanaofahamu kuwa yanaweza kuwa chanzo cha hatari kubwa kiafya yanapoathiriwa na sumu kuvu.
Unapuzungumzia sumu kuvu katika mazao kama vile mtama, mahindi, na karanga, siyo Wananchi wote wanafamu kuwa sumu kuvu inaweza kuleta madhara kwa binadamu na mifugo na hatimaye kusababisha kansa ya ini.
Sumu kuvu ni aina ya sumu inayotengenezwa na kuvu au fangasi wanaoota kwenye mazao mbalimbali hasa nafaka kama vile mahindi, mtama, ngano, mchele na ulezi. Kuvu hao wanapoota huonekana kama ukungu. Mahindi ndiyo nafaka inayoshambuliwa zaidi na uchafuzi wa sumu kuvu ikilinganishwa na nafaka nyingine.
Mazao mengine yanayoweza kushambuliwa na fangasi hawa ni pamoja na mbegu za mafuta kama karanga, pamba, alizeti na korosho; mihogo mikavu; viungo vya chakula mfano iliki na mdalasini; mboga za majani pamoja na matunda yaliyokaushwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO), sumu kuvu huharibu karibu asilimia 25 au zaidi ya chakula kinachozalishwa duniani kila mwaka.
Kutokana na madhara hayo, Idara ya Teknolojia na Sayansi ya Vyakula, Ndaki ya Kilimo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, imetengeneza teknolojia mpya ya mfumo wa kidigitali wa kudhibiti vigezo vinavyosababisha uzalishaji wa sumu kuvu (aflatoxins) ili kugundua viatarishi vinavyosababisha sumu kuvu katika mazao.
Hii si teknolojia kutoka nje ya nchi. Ni ubunifu uliotengenezwa Tanzania na timu ya watafiti wakiongozwa na Profesa Mshiriki Lilian Kaale kutoka Idara ya Teknolojia na Sayansi ya Vyakula, Ndaki ya Kilimo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Kaale ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ubunifu na Ujasiriamali chuoni hapo anasema ubunifu huo unalenga kudhibiti sumu kuvu kabla haijazalishwa kwenye mazao yaliyohifadhiwa maghalani.
Anaeleza kwamba safari ya utafiti huo ilianza mwaka 2018 baada ya kupata ufadhili wa takribani Sh milioni 100 kutoka UNESCO.
“Niliona tatizo la sumu kuvu ni kubwa sana Tanzania. Mbali na kuharibu mazao, mazao yaliyoingiliwa na sumu hii yanaathiri afya za binadamu kwa kiwango kikubwa hususan kuchangia saratani ya ini,” anasema.
Baadaye aliomba ufadhili kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ambapo alipata shilingi milioni 120 ili kuendeleza tafiti zaidi kuhusu namna ya kutumia teknolojia ya kidigitali kugundua na kuzuia mazingira yanayochochea uzalishaji wa sumu kuvu.
Kwa mujibu wa Kaale, sumu hiyo huzalishwa na fangasi aina ya aspergillus pale mazingira fulani yanapokuwepo, hasa joto na unyevunyevu mkubwa.
“Vimelea hivi vinaweza kuwepo kwenye mazao lakini visizalishe sumu kuvu mpaka mazingira yanayowawezesha kufanya hivyo yatokee,” anasema.
Anataja mahindi, karanga na mtama kuwa miongoni mwa mazao yanayoathirika zaidi.
Anasema ubunifu huo umetengenezwa kwa kutumia vifaa vinavyopima kiwango cha unyevunyevu, joto na hali ya hewa ndani ya ghala.
Mfumo huo unapogundua mazingira yanaanza kufikia kiwango hatarishi cha kuzalisha sumu kuvu, kengele huanza kulia na ujumbe hutumwa moja kwa moja kwa msimamizi wa ghala kupitia simu.
“Ukidhibiti mazingira hayo mapema, fangasi hawawezi kuzalisha sumu kuvu,” anasema Profesa Kaale.
Anaeleza kwamba mfumo huo umeunganishwa na simu za wasimamizi wa maghala kuwawezesha kuwasha feni au kufungua milango ili kupunguza joto na unyevunyevu kabla hali haijafikia kiwango hatari.
Kwa mujibu wake, mazao baada ya kuvunwa hubaki hai na huendelea kuzalisha joto na unyevunyevu, hali hiyo huongeza uwezekano wa kuzalishwa kwa sumu kuvu wakati wa uhifadhi.
“Tafiti zinaonesha upotevu mkubwa wa mazao hutokea baada ya kuvuna, hasa kipindi cha uhifadhi,” anasema.
Anafafanua kuwa kwa sasa teknolojia hiyo imefungwa katika ghala lililopo Chemba mkoani Dodoma chini ya usimamizi wa Wizara ya Kilimo na wadau wengine wa serikali kama mfano wa majaribio tangu Agosti mwaka jana.
Kwa sababu ya gharama zake, Profesa Kaale anasema mkulima mmoja mmoja hawezi kuimudu kwa sasa na kwamba inalenga zaidi maghala makubwa ya serikali na wafanyabiashara wakubwa.
"Tumeshirikiana na serikali kwa sababu athari za sumu kuvu ni za taifa. Mfanyabiashara binafsi anaweza kupata mfumo huo kwa gharama ya takribani Sh milioni 30 ili kuusimika kwenye ghala lake," anasema.
Kwa mujibu wa Profesa Kaale, sumu kuvu ina madhara makubwa kwa ini na imehusishwa pia na magonjwa yasiyoambukiza pamoja na udumavu kwa watoto.
Anasema tatizo hilo linaweza kuathiri mamilioni ya Watanzania kwa sababu zaidi ya watu milioni 50 hutumia mahindi na karanga kama chakula cha kila siku.
“Ukilisha wanyama pumba zenye sumu kuvu, madhara yanaweza kurudi kwa binadamu kupitia mnyororo wa chakula,” anasema.
Anakumbusha tukio la mwaka 2015 mkoani Dodoma ambapo watu walifariki baada ya kula chakula kilichoathiriwa na sumu kuvu.
Kwa upande wake, Ibrahim Kinyoro ambaye ni mwanafunzi wa PhD anayesimamiwa na Profesa Kaale, anasema anakubaliana na teknolojia hiyo kwa kiasi kikubwa katika kukabiliana na sumu kuvu nchini.
Anasema teknolojia mbalimbali zimetumiwa na mtafiti huyo ikiwemo mifumo ya kengele "alarm" ya kutambua uwepo wa sumu kuvu.
"Teknolojia nzuri na nyingi zipo tayari na zimetoa matokeo isipokuwa uwekezaji na uendelevu wa teknolojia hizo kutumiwa na wakulima una gharama kubwa," anaeleza.
Kinyolo anasema ni wakati wa serikali, watunga sera na sekta binafsi kushirikiana kuwekeza katika teknolojia na kuwakomboa wakulima kukabiliana na sumu kuvu.
Anaeleza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na namna wanavyozalisha mazao yao, kuvu wataendelea kukua.
Kinyoro anasema sumu kuvu ikishaingia kwenye mahindi au karanga kuna baadhi ya hatua zikifanywa hupunguza kwa asilimia kidogo uwepo wake ikiwemo kuyachagua moja moja, kupepeta au kukoboa.
"Hizi ni njia za asili zinazotumika kuondoa sumu kuvu lakini mazao haya yakishambuliwa kwa wingi, zile unazozitoa kwa macho ndiyo ambazo zimeshambuliwa kwa kiwango kikubwa na zipo nyingine huwezi kuziona kwa macho."
Kwa upande wake, Mshauri wa Sera wa taasisi ya GRAIN, Leticia William, anasema sumu kuvu ni hatari sana ikiingia mwilini mwa binadamu au mnyama kwani inaua kimyakimya na inaweza kusababisha saratani.
Anasema ongezeko la uchafuzi wa sumu kuvu kwenye mazao ya chakula na chakula cha mifugo linaendelea kuwa tishio kubwa kwa afya ya binadamu na wanyama nchini Tanzania.
“Kutokana na hali hiyo, watu, watoto, ng’ombe, kuku, nguruwe na wanyama wengine wako kwenye hatari kubwa kutokana na matumizi ya mazao yaliyoathirika,” anasema.
Naye Mchumi Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Dkt. Deogratius Lwezaura, anasema utafiti uliofanywa kati ya mwaka 2012 na 2014 katika kanda saba za kilimo ulithibitisha kuwa sumu kuvu inaweza kusababisha saratani ya ini, mzio, kudumaa kwa watoto pamoja na kuathiri ukuaji wa akili.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa Martin Kimanya kwa kushirikiana na watafiti wa Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela mwaka 2016, Tanzania ilipoteza zaidi ya Sh bilioni 550 kila mwaka kutokana na athari za kiafya na kiuchumi zinazosababishwa na sumu kuvu kwenye mazao ya chakula.
Hasara hiyo inajumuisha mazao yanayokataliwa katika masoko ya ndani na nje pamoja na gharama za matibabu ya magonjwa kama saratani ya ini.
Ripoti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pia ilieleza kuwa bara la Afrika hupoteza wastani wa Dola za Marekani milioni 670 kila mwaka kutokana na bidhaa za kilimo kukataliwa katika masoko ya nje kwa sababu ya uchafuzi wa sumu kuvu.
Katika taifa linalotegemea kilimo, vita dhidi ya sumu kuvu si suala la maabara pekee. Ni suala la afya, usalama wa chakula na mustakabali wa uchumi wa taifa.



No comments:
Post a Comment