
Na Mwandishi Wetu.
Hospitali
ya Benjamin Mkapa (BMH) inahitaji kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 7
ndani ya kipindi cha miaka miwili kwa ajili ya kufanikisha matibabu ya
ubingwa bobezi ya upandikizaji wa uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa
selimundu pamoja na upandikizaji wa figo kwa wananchi wenye uhitaji
mkubwa wa huduma hizo.
Mahitaji
haya yametangazwa leo tarehe 21 Mei 2026 katika Ukumbi wa NIMR Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi
katika mkutano wake na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri, Tanzania
Bloggers Network (TBN) na Jumuiya ya Miitandao Tanzania (JUMIKITA).
Alisema kwa sasa kuna watoto 50 wanaohitaji upondikizaji wa uloto na wengine 50 kwa ajili ya upandfikizaji wa figo.
Mkutano
huo ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka
10 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, hapo Julai 15 ,2026 ambapo
safari ya maadhimisho haya ilizinduliwa rasmi mwezi Oktoba mwaka 2025.
Tangu
kuanzishwa kwa hospitali hiyo Oktoba 13,2015, Hospitali ya Benjamin
Mkapa imekuwa na dhamira ya kutoa huduma za kibingwa kwa kutumia
teknolojia ya kisasa katika kuzuia, kuchunguza, na kutibu magonjwa
mbalimbali, pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa afya na kufanya
tafiti.
Kwa
sasa, BMH inahudumia takribani wananchi milioni 10 kutoka mikoa nane ya
Tanzania, ikiwa na vitanda 400 na watumishi 1,073, wakiwemo madaktari
bingwa na bingwa bobezi zaidi ya 100.
Kwa
mujibu wa Profesa Makubi Hospitali hiyo inatoa huduma 20 za kibingwa na
huduma 18 za ubingwa bobezi zikiwemo upandikizaji wa viungo, upasuaji
wa moyo kwa kufungua kifua, uchunguzi wa mishipa ya moyo, huduma za
radiolojia ya kisasa, upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, ubadilishaji
wa nyonga na magoti, upasuaji wa njia ya matundu madogo, pamoja na
uchujaji wa damu.
Profesa
Makubdi amesema ndani ya miaka 10 ya utendaji, hospitali imepata
mafanikio makubwa yaliyochangiwa na uwekezaji wa serikali katika
miundombinu na vifaa vya kiasi cha shilingi bilioni 283, huku idadi ya
watumishi ikiongezeka kutoka 20 tu mwaka 2015 hadi kufikia 1,076 mwaka
2026.
Hospitali
imefanikiwa kupanua na kuboresha huduma za matibabu ya kibobezi,
ikiwemo uanzishwaji wa huduma muhimu za upandikizaji figo na uloto kwa
watoto wenye selimundu, pamoja na kukuza tiba utalii kwa kuhudumia
wagonjwa wa kigeni na viongozi mashuhuri, wakiwemo wagonjwa 2,897 kutoka
Burundi, 526 kutoka Comoro, na wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo (DRC).
Ubora
wa huduma umeongezeka kupitia upasuaji wa matundu na uanzishwaji wa
Kliniki ya Kifalme (Royal Clinic) mnamo tarehe 10 Julai 2025, ambayo
imeshalaza na kuhudumia wagonjwa 18,607, wakiwemo wagonjwa wa kimataifa
390 waliofanyiwa uchunguzi mkubwa wa afya (Master Health Check-up).
BMH
pia imepata ithibati ya kimataifa ya maabara ya ISO 15189:2022,
imeboresha mifumo yake ya TEHAMA, imeweka mfumo wa kisasa wa kuelekeza
wagonjwa (queuing system) na kutoa maoni, na imefanikiwa kupunguza muda
wa mgonjwa kusubiri huduma kutoka wastani wa saa 8 hadi saa 3 tu.
"Tunatoa
shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na serikali
yake kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya na hasa ndani ya BMH, na
ninatoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kuokoa maisha ya wagonjwa
huku sisi tukiahidi kuendelea kuishi kwa kauli mbiu yetu ya kuvaa viatu
vya mgonjwa, uwajibikaji, na kujituma, " alisema Profesa Makubi.
Katika
kuimarisha miradi ya kimkakati, hospitali inaendelea na ujenzi wa jengo
la matibabu ya saratani lenye thamani ya shilingi bilioni 32, jengo la
matibabu ya figo la shilingi bilioni 44.9 linalojengwa kwa ushirikiano
kati ya Serikali ya Japani iliyochangia bilioni 28 na Serikali ya
Tanzania iliyochangia bilioni 16.9, uanzishwaji wa Kituo cha Umahiri cha
upandikizaji uloto, pamoja na chuo kinachotoa elimu ya ngazi ya
Stashahada.
Akizungumzia
mwelekeo Preofesa Makubdi alisema taasisi hiyo kwa miaka 10 ijayo
inajipanga kubobea zaidi na kuwa kijiji cha utalii wa matibabu katika
Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Kuelekea
kilele cha tarehe 15 Julai 2026, matukio mbalimbali yamepangwa na
mengine tayari yamefanyika ili kuongeza uelewa na ushiriki wa wadau,
ikiwemo mikutano iliyofanyika mwezi Aprili 2026 jijini Dar es Salaam na
Arusha na Watendaji Wakuu wa Mashirika na Taasisi zote za Umma, ambapo
takriban shilingi bilioni 4 zimeshapatikana kutoka kwa wadau wa sekta ya
umma na kampuni zenye ubia na serikali.
Aidha,
Kongamano la Kisayansi lililoangazia hali ya huduma za upandikizaji
viungo nchini lilifanyika tarehe 6 Mei 2026 katika Ukumbi wa Domiya
Estate likishirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi, na hivi sasa
maandalizi ya dhifa za chakula cha jioni (Gala dinners) pamoja na mbio
maalumu za Marathon yanaendelea ili kuchangisha fedha hizo.
Zoezi
hili la harambee la kusaidia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na
figo linafanyika kwa kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya (NHIF) kwa lengo la kuwasaidia Watanzania wasio na uwezo ambao
idadi yao inaongezeka kila siku.
Harambee
hiyo kubwa itakayofanyika tarehe 15 Julai 2026 jijini Dodoma,
inatarajiwa kuongozwa na Mgeni Rasmi Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Profesa
makubdi ameyaomba Mashirika, taasisi, makampuni, wadau, na wananchi
wote kuchangia kupitia njia rasmi zilizowekwa ambazo ni namba ya malipo
(Control Number) 986930000001 au kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kwa
akaunti namba 102501000407 zote zikiwa kwa jina la BMH Organ
Transplant.






No comments:
Post a Comment