JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Benki ya NBC Yazindua Kampeni ya “Shinda Trip ya Mauritius” Kukuza Matumizi ya Malipo ya Kidijitali

Share This
Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imezindua kampeni inayofahamika kama “Shinda Trip ya Mauritius”, yenye lengo la kuhamasisha matumizi mapana ya mifumo ya malipo ya kidijitali kupitia kadi za NBC Visa sambamba na kuwapa wateja wake fursa ya kujishindia safari ya kipekee ya kutembelea visiwa vya Mauritius.

Kampeni hiyo, iliyozinduliwa rasmi leo, makao makuu ya benki hiyo jijini Dar es Salaam, ni sehemu ya dhamira pana ya NBC katika kuendeleza uchumi usiotegemea matumizi ya fedha taslimu pamoja na kuimarisha ujumuishaji wa kifedha kupitia huduma za kibenki zilizo salama, za kisasa na rahisi kutumia. Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa na waandishi wa habari, viongozi, wafanyakazi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya huduma za kifedha.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC, David Raymond alisema kampeni hiyo ya miezi mitatu inalenga kuwahamasisha wateja kutumia zaidi mifumo ya malipo ya kidijitali kwa kufanya manunuzi na miamala mbalimbali kupitia kadi zao za NBC Visa ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Raymond, kampeni hiyo haijalenga tu kuwazawadia wateja, bali pia kuwasaidia Watanzania kutambua umuhimu unaozidi kuongezeka wa huduma za kifedha za kidijitali katika dunia ya sasa inayobadilika kwa kasi kubwa.

“Tunalenga kuona wateja wetu wanakumbatia kikamilifu matumizi ya malipo ya kidijitali kwa sababu ni salama zaidi, yanafanyika kwa haraka na ni rahisi zaidi katika maisha ya sasa. Dunia inaelekea katika matumizi ya mifumo janja ya kifedha, na sisi NBC tunataka kuhakikisha wateja wetu wanakuwa sehemu ya safari hiyo,” alisema Raymond.

Aliongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, wateja watapata nafasi ya kujishindia safari ya ndoto kwenda Mauritius huku wakiendelea kufurahia urahisi na usalama unaotokana na matumizi ya kadi za NBC Visa.

“Tunaamini kampeni hii itasaidia zaidi kuimarisha utamaduni wa matumizi ya miamala isiyotumia fedha taslimu nchini,” alisisitiza.

Kupitia kampeni hiyo, kila mteja atakayefanya miamala mitano au zaidi kwa kutumia kadi ya NBC Visa ataingia moja kwa moja kwenye droo ya kila mwezi, ambapo washindi watakaobahatika watajishindia safari ya gharama zote kulipiwa kwenda visiwa vya Mauritius.

Raymond alibainisha kuwa jumla ya washindi watatu wanatarajiwa kupatikana katika kipindi chote cha kampeni, huku kila mshindi akipata nafasi ya kusafiri akiwa ameambatana na mtu mmoja wa chaguo lake. Safari hiyo ya kifahari inatarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu.

Kampeni hiyo inakuja wakati taasisi nyingi za kifedha duniani zikiongeza jitihada za kuhamasisha matumizi ya miamala ya kidijitali, huku watumiaji wakizidi kutafuta huduma za malipo zilizo salama, za haraka na zenye unyumbufu zaidi.

Raymond alisisitiza kuwa mbali na zawadi kubwa ya safari, watumiaji wa kadi za NBC Visa wanaendelea kunufaika na manufaa mbalimbali yanayoambatana na matumizi ya kadi hizo, ikiwemo kuimarishwa kwa usalama wa fedha zao, urahisi wa kufanya malipo popote duniani pamoja na kupata punguzo na ofa maalum kupitia ushirikiano wa kimataifa wa Visa.

“Matumizi ya kadi hupunguza hatari zinazoweza kujitokeza kutokana na kubeba fedha taslimu, huku yakitoa urahisi mkubwa kwa wateja wanapofanya manunuzi, kusafiri, kulipa bili au kufanya miamala mtandaoni. Aidha, wateja wetu wanaweza kufaidika na punguzo mbalimbali katika hoteli, tiketi za ndege, huduma za utalii pamoja na maduka mbalimbali duniani,” aliongeza.

Alifafanua kuwa, kupitia matumizi ya kadi za NBC Visa, wateja watanufaika na punguzo mbalimbali ikiwemo hadi asilimia 40 katika huduma za CIP Lounge, hadi asilimia 20 kwenye hoteli, shopping na vivutio vya utalii jijini Paris, hadi asilimia 15 London na hadi asilimia 25 Thailand, sambamba na huduma maalum za kipekee katika maeneo hayo.

“Aidha, watumiaji wa kadi ya Platinum Business watanufaika na punguzo la hadi asilimia 50 kwenye safari, hoteli na manunuzi pamoja na huduma za bima na matibabu wanapokuwa nje ya nchi. Wateja pia watapata punguzo maalum kupitia mashirika ya ndege ya Ethiopian Airlines, Emirates, Kenya Airways na Qatar Airways.’’ alitaja

Zaidi, alibainisha kuwa kampeni hiyo inaendana na mkakati wa muda mrefu wa NBC wa kuharakisha mageuzi ya kidijitali katika sekta ya huduma za kifedha, kwa kupanua upatikanaji wa huduma bunifu za kifedha na kuwahamasisha Watanzania wengi zaidi kutumia mifumo rasmi ya kibenki inayotumia teknolojia.

“Kadiri huduma za benki za kidijitali zinavyoendelea kubadilisha taswira ya sekta ya fedha nchini Tanzania na duniani kote, sisi tunaendelea kuwa na dhamira ya kuanzisha suluhisho zinazomlenga mteja ambazo zinarahisisha huduma za kila siku za kibenki huku zikitoa uzoefu wenye manufaa kwa wateja wetu,” alihitimisha.




Maofisa waandamizi wa benki ya NBC akiwemo Mkuu wa Idara ya Manunuzi Bi Sesaria Rusimbi (katikati), Mkuu wa Idara ya Masoko Bw Davidi Raymond (kushoto) na Mkuu wa Idara ya Miamala wa NBC, Bw Mangire Kibanda (kulia) wakijipongeza wakati wakizindua kampeni inayofahamika kama “Shinda Trip ya Mauritius”, yenye lengo la kuhamasisha matumizi mapana ya mifumo ya malipo ya kidijitali kupitia kadi za NBC Visa sambamba na kuwapa wateja wake fursa ya kujishindia safari ya kipekee ya kutembelea visiwa vya Mauritius. Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo jijini Dar es Salaam.






Maofisa waandamizi wa benki ya NBC akiwemo Mkuu wa Idara ya Manunuzi Bi Sesaria Rusimbi (katikati), Mkuu wa Idara ya Masoko Bw Davidi Raymond (wan ne kushoto) na Mkuu wa Idara ya Miamala wa NBC, Bw Mangire Kibanda (wanne kulia) wakijipongeza wakati wakizindua kampeni inayofahamika kama “Shinda Trip ya Mauritius”, yenye lengo la kuhamasisha matumizi mapana ya mifumo ya malipo ya kidijitali kupitia kadi za NBC Visa sambamba na kuwapa wateja wake fursa ya kujishindia safari ya kipekee ya kutembelea visiwa vya Mauritius. Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo jijini Dar es Salaam.






Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Idara ya Masoko wa NBC, David Raymond (pichani) alisema kampeni hiyo ya miezi mitatu inalenga kuwahamasisha wateja kutumia zaidi mifumo ya malipo ya kidijitali kwa kufanya manunuzi na miamala mbalimbali kupitia kadi zao za NBC Visa ndani na nje ya Tanzania.













Hafla ya uzinduzi huo ilihudhuriwa na waandishi wa habari, viongozi, wafanyakazi pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya huduma za kifedha.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad