JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WAZIRI MKUU AZINDUA SERA YA TAIFA YA USIMAMIZI WA UGAVI

Share This

Awataka waliopewa dhamana ya usimamizi wazingatie misingi ya utawala bora

 
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ameziagiza Mamlaka, Taasisi na Wadau wote waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 wabadilike na wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na utawala wa sheria ili kufikia malengo na shabaha zilizoainishwa katika Sera hiyo.

Amesema taarifa za ukaguzi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma zinaonesha kuwa changamoto katika ununuzi wa umma siyo Sera, Sheria wala Kanuni, bali ni waliopewa dhamana ya kusimamia Sera, Sheria, Kanuni na Taratibu za Ununuzi.

Waziri Mkuu amesema kuwa sehemu kubwa ya shughuli za ununuzi zinaathiriwa zaidi na mitazamo, hulka na tabia za wataalamu na watendaji ikilinganishwa na upungufu wa masuala ya kisera na kisheria, hivyo amewataka  wadau wa Sekta Binafsi waweke mikakati ya kuimarisha mifumo ya ushirikiano na sekta ya umma ili kunufaika kikamilifu na fursa zilizobainishwa katika Sera hiyo.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Aprili 8, 2026) alipozindua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. “Leo tunaweka alama muhimu katika historia ya usimamizi wa mali na rasilimali za Taifa letu”.

Amesema hatua hiyo ya kisera inalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira na kipato, pamoja na kujenga uchumi jumuishi na shindani unaomilikiwa na Watanzania walio wengi. “Kwa ujumla, fursa hizi zinalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza uzalishaji wa bidhaa, Utoaji wa huduma pamoja na kukuza uwiano wa upatikanaji wa bidhaa na huduma”.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kwa mara ya kwanza, Tanzania inakuwa na mwongozo mmoja wa kisera unaounganisha na kufungamanisha mtazamo wa kimfumo na hatua zote muhimu katika mnyororo wa ugavi, kuanzia ununuzi, ugomboaji, upokeaji, urejeshaji, uhifadhi, matumizi, usambazaji hadi uondoshaji wa mali za umma”.

Waziri Mkuu amesema Sera hiyo inaweka mkazo katika matumizi ya malighafi na wataalamu wa ndani, kukuza viwanda vya ndani, kuimarisha miundombinu ya kiteknolojia, pamoja na kuzingatia hifadhi ya mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. “Kwa kufanya hivyo, mnyororo wa ugavi umeimarishwa na kuwa chombo cha kimkakati cha kuongeza uzalishaji na ugavi wa bidhaa na huduma pamoja na uendelevu na ushindani wa Taifa katika Masoko ya kikanda na kimataifa”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amezitaka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wadau wa Sekta Binafsi watekeleze Sera hiyo kwa Weledi, Uwazi na Uwajibikaji.

Amesema kufikiwa kwa malengo na shabaha za Sera hiyo kutategemea zaidi dhamira, fikra, mtazamo, uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji wa wadau wote katika ngazi zote za usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi.

Pia, Waziri Mkuu amezisisitiza Mamlaka zote zinazohusika zihakikishe kuwa utekelezaji wa Sera hii unaimarisha ushiriki wa wazalishaji wa ndani, wafanyabiashara wadogo na wa kati, pamoja na makundi maalumu ya kijamii ili kufikia malengo jumuishi na usawa miongoni mwa washiriki.

Amesema Wizara na Taasisi zote za umma zinapaswa kufanya Mapitio ya Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayokinzana na misingi ya Sera hii ili kuwa na mazingira rafiki katika usimamizi wa shughuli za Mnyororo wa Ugavi.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Fedha na Mipango, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Profesa Elisante Ole Gabriel ambaye amemuwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mashimba Ndaki aliyemuwakilisha Spika wa Bunge, Wakuu wa Mkoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala wa Wilaya.





 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad