Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Waziri wa Viwanda naii Biashara, Judith Kapinga, ameielekeza Tume ya Ushindani (FCC) kuendelea kutoa elimu kwa walaji ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuimarisha ushindani wa soko nchini.
Waziri Kapinga alitoa kauli hiyo wakati wa kilele cha kufunga maadhimisho ya Siku ya Mlaji Duniani, yaliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa walaji wanapaswa kulindwa kwa kuhakikisha wanapata bidhaa na huduma zilizo bora, salama na zenye viwango vinavyokubalika katika ushindani wa soko.
“Ni muhimu kwa FCC kuendelea kusimamia haki za walaji kwa kuhakikisha wanapata bidhaa bora na huduma zinazokidhi viwango vinavyotakiwa, sambamba na kujenga mazingira ya ushindani wa haki sokoni,” amesema Waziri Kapinga.
Aidha, ameitaka FCC kuendelea kukutana na wadau mbalimbali, wakiwemo wazalishaji na wafanyabiashara, kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi unaolenga kuboresha mazingira ya biashara na ulinzi wa mlaji.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa fursa muhimu ya kuwakutanisha wadau mbalimbali na kuwapatia elimu kuhusu haki za mlaji katika kujenga ushindani imara sokoni.
Amesema FCC itaendelea kulinda soko kwa kuhakikisha mlaji anapata huduma na bidhaa bora zinazokidhi viwango vinavyohitajika.
“FCC itaendelea kuwa nguzo muhimu katika kusimamia haki za walaji pamoja na kuimarisha ushindani wa soko kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa taifa,” amesema Ngasongwa.
Aidha, ameongeza kuwa tume hiyo itaendelea kuwa daraja kati ya wazalishaji, wafanyabiashara pamoja na walaji kwa lengo la kuhakikisha utoaji wa huduma na bidhaa bora unazingatiwa wakati wote.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la FCC, Aggrey Mulimuka, amesema baraza hilo litaendelea kutoa ushauri wa kitaalamu kwa lengo la kulinda ushindani wa soko unaozingatia maslahi ya mlaji.
Dkt. Mulimuka amesema dhamira ya baraza ni kuhakikisha kuwa ushindani wa soko unakuwa chachu ya upatikanaji wa huduma bora, bidhaa zenye ubora na mazingira rafiki kwa walaji.
Baraza litaendelea na ikiendelea ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine katika kujenga soko lenye ushindani wa haki na manufaa kwa taifa
Maadhimisho hayo yamebeba Kauli Mbiu ya Bidhaa Salama,Imani kwa mlaji ikiwa ni kuimarisha uelewa wa walaji juu ya haki zao.
Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga akizungumza wakati akifunga Kilele cha Maadhimisho Siku ya Mlaji yaliyoratibiwa na Tume ya Ushindani (FCC) jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga akizundua namba ya maalumu ya mawasiliano kwa wateja kuwasiliana na FCC wakati akifunga Kilele cha Maadhimisho Siku ya Mlaji jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC) Khadija Ngasongwa akitoa maelezo kuhusiana na maadhimisho ya siku ya mlaji hadi kufikia kilele chake yaliyofanyika ,jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa Baraza la FCC Dkt Aggrey Mulimuka wakati wa Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mlaji jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Viwanda na Biashara Judith Kapinga akizungumza wakati akifunga Kilele cha Maadhimisho Siku ya Mlaji yaliyoratibiwa na Tume ya Ushindani (FCC) jijini Dar es Salaam.



No comments:
Post a Comment