Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, akizungumza leo Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026.
Na Mwandishi Wetu
WATANZANIA wameendelea kuongoza katika umiliki wa miradi ya uwekezaji nchini, hatua inayoonesha kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya taifa.
Akizungumza leo Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, amesema Watanzania wanamiliki zaidi ya asilimia 57 ya miradi iliyosajiliwa ikijumuisha miradi ya wazawa na ile ya ubia kati ya Watanzania na wawekezaji wa nje.

Amesema katika kipindi hicho TISEZA imesajili miradi 177 inayotarajiwa kuwekeza mtaji wa dola za Marekani milioni 1,122.09 na kuzalisha ajira 19,750 katika sekta mbalimbali za uchumi ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, miundombinu na kilimo.
Kwa mujibu wa Teri, kati ya miradi hiyo, Watanzania wanamiliki miradi 63 sawa na asilimia 35.59 huku miradi 38 ikiwa ya ubia kati ya Watanzania na wawekezaji wa nje, jambo linalofanya uwekezaji wenye ushiriki wa Watanzania kufikia zaidi ya asilimia 57 ya miradi yote iliyosajiliwa.
Amesema hali hiyo inaonesha kuongezeka kwa uelewa wa Watanzania kuhusu umuhimu wa uwekezaji na fursa zilizopo nchini, sambamba na jitihada za Serikali kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande wa mitaji, Teri ameeleza kuwa uwekezaji wa ndani umeendelea kukaribia ule wa wawekezaji wa nje, ambapo mitaji ya wawekezaji wa kigeni imefikia dola za Marekani milioni 565 huku mitaji ya wawekezaji wa ndani ikifikia dola milioni 556 katika kipindi hicho.
Aidha, sekta ya uzalishaji viwandani imeendelea kuongoza kwa kuvutia uwekezaji kwa kusajili miradi 91 sawa na asilimia 51 ya miradi yote, huku ikitarajiwa kuzalisha zaidi ya asilimia 63 ya ajira zote zitakazotokana na miradi hiyo.
Kwa upande wa maeneo, mikoa ya Dar es Salaam na Pwani imeendelea kuwa vinara wa kuvutia uwekezaji kutokana na uwepo wa miundombinu muhimu ya kiuchumi ikiwemo bandari, reli, barabara na huduma nyingine wezeshi kwa shughuli za uzalishaji.
Teri ametoa wito kwa wawekezaji wa ndani kuendelea kusajili miradi yao kupitia TISEZA ili waweze kunufaika na vivutio mbalimbali vinavyotolewa na Serikali kupitia sheria ya uwekezaji na maeneo maalum ya kiuchumi ya mwaka 2025 pamoja na huduma za kitaalamu zinazotolewa katika utekelezaji wa miradi ya uwekezaji.

.jpeg)
.jpeg)




No comments:
Post a Comment