VIWANDA vitatu vya bidhaa za Twyford vinavyofanya kazi chini ya KEDA (T) Ceramics Co. Ltd, vinavyojumuisha uzalishaji wa vigae na kioo, vinaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda nchini Tanzania. Kiwanda cha vigae kipo Chalinze, huku viwanda viwili vya kioo vikiwa Mkuranga. Kwa pamoja, viwanda hivi vinaajiri zaidi ya wafanyakazi 3,000 wa Kitanzania. Kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya uzalishaji wa kiotomatiki, viwanda hivi vinazalisha bidhaa bora, imara na za kudumu.
Mbali na kuboresha maisha ya wafanyakazi kupitia ajira na fursa za kiuchumi, viwanda hivi pia vinachangia maendeleo ya jamii zinazovizunguka. Aidha, bidhaa zinazozalishwa zina mchango mkubwa katika kubadilisha sekta ya ujenzi kwa kutoa vifaa vya viwango vya juu vinavyoimarisha uimara na kuongeza mvuto wa majengo, hivyo kuboresha mandhari ya mazingira kwa ujumla. Hayo yamebainishwa na Manager: Biashara na Miradi wa kampuni hiyo John Chimwejo, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii, mjini Mkuranga, mkoani Pwani, hivi karibuni.
Bwana Chimwejo amesema kuwa ushahidi wa mandhari nzuri ya majengo yaliyopendeza kwa vigae na vioo vya Twyford unaonekana wazi ukitembelea maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Katika hospitali, shule, pamoja na majengo ya serikali, taasisi za umma na binafsi, majengo mengi ya kisasa yamepambwa na vigae na vioo vya Twyford vinavyoboresha muonekano wake kwa kiasi kikubwa.
Kabla ya uwepo wa viwanda hivi nchini, vifaa vingi vya ujenzi kama vigae na vioo kwa majengo makubwa vilikuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi. Hata hivyo, kwa sasa vinazalishwa ndani ya Tanzania kupitia viwanda vya Twyford, hatua ambayo imechangia kupunguza gharama za ujenzi kwa kiasi kikubwa. Aidha, uzalishaji wa ndani umefanya vifaa hivi kupatikana kwa gharama nafuu huku ubora ukiendelea kuwa wa hali ya juu.
Wafanyakazi wa kiwanda cha vioo (glass) cha kampuni ya KEDA (T) Ceramics Co. Ltd kinachozalisha vioo (float glass) vya Twyford kilichopo eneo la Msufini, Kidete Mbezi, wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani. Ajira pia inazingatia usawa wa kijinsia, hakuna kazi ya kiume, wala kazi ya kike, kwao kazi ni kazi.
Bwana Chimwejo ametolea mfano wa Wodi ya Watoto Wachanga katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ambayo sakafu safi na ang’avu zilizowekwa vigae vya ubora wa juu vya Twyford. Hata katika Hospitali ya Rabininsia iliyopo Tegeta, vigae vinavyotumika ni vya Twyford. Aidha, vigae vya Twyford vimewekwa katika Jengo la Halmashauri ya Mji wa Mbinga Kusini, na kulifanya jengo hilo la ofisi ya serikali kuwa na muonekano wa kisasa na wa kuvutia.
Chimwejo ametaja Eneo la Viwanda la Chalinze, lililopo kilomita 70 kutoka jijini Dar es Salaam, ndipo kilipo kiwanda cha kisasa cha vioo na vigae vya Twyford kinachofanya kazi kwa saa 24, kikizalisha vigae kwa ajili ya soko la Tanzania na soko la nchi za Afrika.
Mbali na kiwanda kilichopo Chalinze, viwanda vingine viwili vya kioo vipo umbali wa takribani kilomita 100 kutoka Dar es Salaam katika maeneo ya Mbezi, Kidete Msufini na Mkiu, Nyamato, Wilaya ya Mkuranga, ambapo viwanda hivyo vikubwa vya kioo vinafanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Viwanda hivi vinatumia tanuru zenye joto la zaidi ya nyuzi joto 1,000 za Selsiasi, ambapo kioo kilichoyeyushwa huundwa kuwa mabamba ya maumbo mbalimbali kupitia mitambo ya kisasa inayojiendesha kwa mfumo wa otomatiki unaodhibitiwa na kompyuta. Bidhaa za Twyford Glass hazitumiki tu katika miradi ya ujenzi ndani ya Tanzania, bali pia husafirishwa kwenda masoko mbalimbali ya nje ya nchi.
Akizungumzia historia ya viwanda hivyo, Manager: Biashara na Miradi wa kampuni hiyo John Chimwejo, amesema kiwanda cha uzalishaji wa vigae vya Twyford nchini Tanzania kilianza uzalishaji mwaka 2017, na kuongeza uwekezaji kwa kasi, ndani ya miaka michache tu, kimeanzisha vituo vya uzalishaji vinavyohusisha sekta zote mbili za kauri na kioo, sio tuu kwa matumizi ya soko la Tanzania pekee, bali soko la Afrika Mashariki, Afrika nzima na nje ya Afrika. 
Mtaalamu wa Kichina na wataamu wazalendo wa Kitanzania, wakiwa kwenye chumba cha kuendeshea mitambo ya uzalishaji vioo (Control room) inayojiendesha yenyewe ki atomatikali (automated) kwa kutumia compyuta kuzalisha vioo (float glass) kwenye kiwanda cha KEDA (T) Ceramics Co. Ltd kilichopo eneo la Mbezi wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani.
Viwanda hivi vitatu vya kisasa vya vifaa vya ujenzi, vimejenga msingi muhimu kwa sekta ya ujenzi, kwa upatikanaji wa vifaa bora, imara na vya gharama nafuu kwa Tanzania na nchi za Afrika ambapo, zamani vifaa hivi viliagizwa kutoka nje ya nchi. Bidhaa hizi husambazwa si tu kwa soko la ndani la Tanzania lakini pia husafirishwa kwenda nchi kadhaa ikiwa ni pamoja na Madagaska, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Uganda, Malawi, Sudan Kusini, Afrika Kusini, na Mauritius, na kuifanya chapa ya Twyford, kuwa ni chapa yenye ushawishi mkubwa wa vigae na vioo kwa Tanzania, Afrika Mashariki na kwingine Afrika.
Leo, Twyford Tanzania inaendesha viwanda vitatu vya uzalishaji nchini Tanzania, ikiwa na kiwanda kimoja cha vigae na viwanda viwili vya kioo. Kiwanda cha uzalishaji wa vigae kilichopo Chalinze kina ukubwa wa takribani hekta 93 na kimeajiri karibu wafanyakazi 1,000. Kiwanda hiki kimewekewa mitambo ya kisasa ya uzalishaji inayojiendesha kwa mfumo wa otomatiki, inayowezesha uzalishaji wa kiwango kikubwa kwa muda mfupi. Mchakato wa uzalishaji huanzia usindikaji wa malighafi, ukandamizaji, uchomaji hadi ufungashaji wa bidhaa.
Viwanda viwili vya uzalishaji wa vioo vya Twyford Tanzania vilivyopo Mbezi na Nyamato, Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, vina ukubwa wa takribani hekta 120 kwa pamoja na vimeajiri zaidi ya wafanyakazi 2,000. Viwanda hivi huzalisha vioo vya ubora wa hali ya juu, vyenye uwezo wa kuyeyusha zaidi ya tani 1,100 za malighafi ya kioo kila siku. Vinazalisha aina mbalimbali za vioo vya ujenzi kwa unene na maumbo tofauti kuanzia milimita 3 hadi 12, ikiwa ni pamoja na kioo cha kawaida (clear glass), kioo chenye rangi, kioo kinachoakisi mwanga, pamoja na aina nyingine za vioo vya matumizi mbalimbali.
Kutokana na ubora wa bidhaa na uwezo mkubwa wa uzalishaji, Vioo vya Twyford husafirishwa kwenda zaidi ya nchi na maeneo 43 duniani, yakiwemo Afrika Mashariki, Afrika Kaskazini, Afrika Kusini, Mashariki ya Kati, Amerika na Ulaya.
Ndani ya Tanzania, Twyford Tanzania imeanzisha mtandao wa mauzo wa kitaifa, kuanzia Dar es Salaam, Dodoma hadi mikoa mingine, ikifikia miji, maeneo ya vijijini, na hata visiwa vya Zanziba na Pemba. Kampuni hiyo inafanya yote haya ili kuhakikisha kwamba vifaa bora vya ujenzi vinapatikana kwa urahisi zaidi kuwahudumia watumiaji wa ndani na nje ya nchi. Twyford Tanzania pia imetoa faida kubwa za kiuchumi kwa Tanzania. Kwa upande mmoja, biashara hiyo inachangia mapato makubwa ya kodi kwa serikali kila mwaka; kwa upande mwingine, inazalisha mapato muhimu ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya bidhaa nje ya nchi.
Hii inayofanywa na viwanda vya vigae na vioo vya Twyford Tanzania inaweza kuonekana kwa jicho la kawaida kama ni uzalishaji wa vifaa vya ujenzi tu. Hata hivyo, kwa mtazamo mpana na wa kina, Twyford Tanzania haizalishi tu vifaa vya ujenzi, bali inachangia kwa kiasi kikubwa kubadilisha taswira ya uchumi wa Tanzania. 
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mkiu wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea msaada wa madawati, viti na vitabu uliotolewa na KEDA (T) Ceramics Co. Ltd kwa lengo la kuboresha mazingira yao ya kujifunzia.
Kampuni hii inasaidia kuihamisha Tanzania kutoka kuwa nchi inayotegemea uagizaji wa bidhaa kutoka nje (import-dependent country) hadi kuwa nchi inayozalisha na kusafirisha bidhaa nje (export-oriented country), na hivyo kuwa kitovu cha uzalishaji wa vifaa vya ujenzi vinavyouzwa katika masoko ya kimataifa. Kupitia mabadiliko haya, taifa linapata ongezeko la mapato ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa nchi kwa ujumla.
Kwa miaka mingi, Twyford Tanzania imeendelea kuboresha teknolojia yake ya uzalishaji kupitia uboreshaji wa ubunifu wa michanganyiko ya malighafi na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ubora. Hatua hizi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ubora na ufanisi wa bidhaa zake. Wakati huohuo, kampuni imeongeza matumizi ya malighafi zinazopatikana ndani ya nchi, jambo ambalo limepunguza gharama za uzalishaji na kupunguza utegemezi wa uagizaji wa malighafi kutoka nje ya nchi. Hii ni faida kubwa kwa taifa, kwani inasaidia kuongeza uzalishaji wa ndani unaotegemea rasilimali za nchini.
Ukiondoa faida kwa Tanzania na Watanzania kutokana na upatikanaji wa bidhaa bora, zenye ubora wa juu na gharama nafuu kutoka viwanda vya Twyford Tanzania, uwepo wa viwanda hivi pia umechangia kwa kiasi kikubwa katika ajira kwa Watanzania waliopata ajira rasmi katika shughuli za uzalishaji.
Aidha, mamia kwa maelfu ya Watanzania wananufaika kupitia mnyororo wa thamani ikiwemo usambazaji, uuzaji na ununuzi wa bidhaa hizo bora. Zaidi ya hayo, jamii zinazozunguka viwanda hivi zimeendelea kunufaika kupitia utekelezaji wa sera ya uwajibikaji kwa jamii (CSR), ambayo imekuwa ikiunga mkono maendeleo ya kijamii na kuboresha maisha ya wananchi wa maeneo husika.


No comments:
Post a Comment