JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


“Ushirikiano wa WCF na NIT Kuleta Mapinduzi Sekta ya Usafirishaji”

Share This

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma, amesema kuwa ushirikiano kati ya WCF na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) utasaidia kupunguza ajali za barabarani na kulinda nguvu kazi ya Taifa.Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ushirikiano (MoU) iliyofanyika tarehe 31 Machi 2026 jijini Dar es Salaam, Dkt. Mduma alisema kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha usalama barabarani pamoja na kuongeza uelewa kwa madereva ambao ni wadau wakuu wa Mfuko huo.

“Ushirikiano huu utatuwezesha kuimarisha usalama barabarani na kuongeza uelewa kwa madereva, ambao ni sehemu muhimu ya wadau wetu,” alisema Dkt. Mduma.

Alieleza kuwa WCF ilianzishwa kwa lengo la kushughulikia fidia kwa wafanyakazi wanaopata ajali au magonjwa yatokanayo na kazi, lakini tathmini zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya madai yanatokana na ajali za barabarani, hali inayohitaji juhudi za pamoja kupambana nayo.

“Sehemu kubwa ya madai tunayopokea yanatokana na ajali za barabarani, hivyo kuna umuhimu wa wadau kushirikiana kupunguza tatizo hili,” aliongeza.
Akizungumza zaidi, Dkt. Mduma alisema kuwa kupitia mkataba huo, taasisi hizo mbili zitashirikiana katika maeneo muhimu ikiwemo utoaji wa mafunzo na elimu kuhusu usalama wa usafirishaji, kufanya tafiti, kubadilishana taarifa pamoja na kujengeana uwezo wa kitaalamu.

“Makubaliano haya yatajikita katika mafunzo, tafiti, ubadilishanaji wa taarifa na kujengeana uwezo wa kitaalamu ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa ushirikiano huo utaongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila taasisi na kusaidia kufikia malengo ya pamoja ya kupunguza ajali pamoja na kuboresha ustawi wa wafanyakazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Mhandisi Dkt. Prosper Mgaya, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya usafirishaji waliokuwepo, walishuhudia utiaji saini wa makubaliano hayo ambayo yanatarajiwa kuleta mageuzi chanya katika sekta ya usafirishaji nchini.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka taasisi mbalimbali zikiwemo LATRA, Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, TANROADS, TARURA, pamoja na vyama vya wamiliki wa mabasi na malori.



 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad