Katika kufanya maboresho na kuongeza thamani ya Tuzo za wanamichezo bora nchini zinazotolewa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kamati ya uratibu ya Utaoji Tuzo hizo imesema itaendelea kuwa na kipengele cha Tuzo ya Mchezaji Bora Chaguo la watu “People’s Choice Award” ikiwa ni utekelezaji wa maoni ya wadau wa sekta ya michezo waliyoyatoa kuhusu tuzo hiyo.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo Prof. Mkumbukwa Mtambo amesema katika kipengele hicho, wadau na wananchi watapata nafasi ya kumchagua mchezaji bora wanayempenda na kuona anafaa kupata Tuzo hiyo kwa kuandika jina la Mchezaji huyo na kulituma kwa namba ya whatsup ya +255-689525363.“Lengo la kipengele hiki ni kuwapa nafasi wadau kushiriki mchakato wa kumchagua mchezaji Bora ambaye wanaona amefanya vizuri kwa mwaka 2025 hivyo natoa wito kwa wapenzi wa michezo mbalimbali kuwapigia kura wanamichezo ambao wanaona wamefanya vizuri ili waweze kupata tuzo: amesisitiza Prof. Mtambo.
Ameongeza kuwa Kamati ya usimamizi wa Tuzo itafanya kazi kwa karibu na vyama na mashirikisho ya kitaifa katika kutambua washindi wa vipengele mbalimbali vya tuzo pamoja na kutambua timu na wanamichezo waliofanya vizuri katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwa mwaka 2025.
Prof. Mtambo ametoa wito kwa wadau mbalimbali yakiwemo makampuni, taasisi za serikali na binafsi na watu mmoja mmoja wanaopenda maendeleo ya michezo nchini kujitokeza kuipa nguvu BMT katika kutekeleza jukumu hili zito na muhimu la kutoa tuzo ili kuendelea kuwapa hamasa wanamichezo ya kufanya vizuri zaidi, kwani mafanikio hayo ni ya watanzania kwa ujumla wetu.



No comments:
Post a Comment