JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


SERIKALI YAJIPANGA KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WA CSR SEKTA YA MADINI

Share This

Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi wa utekelezaji wa wajibu wa kampuni kwa jamii (Corporate Social Responsibility – CSR) katika Sekta ya Madini, kufuatia kuwepo kwa mfumo maalum wa kisheria uliowekwa kupitia Kanuni za CSR za mwaka 2023 zinazolenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na ushirikiano miongoni mwa wadau.

Akifungua kikao kazi cha wataalam kutoka Wizara ya Madini, Tume ya Madini pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI (OWM-TAMISEMI) kilichofanyika leo Aprili 22, 2026 jijini Dodoma kwa lengo la kujadili masuala mtambuka ya utekelezaji wa CSR, Kamishna wa Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, amesema kanuni hizo zilibuniwa mahsusi kupunguza migogoro iliyokuwa ikijitokeza kati ya Serikali za Mitaa na wamiliki wa leseni za madini kuhusu utekelezaji wa miradi ya CSR.

Dkt. Numbi amesema kuwa pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2025, bado kuna changamoto zinazoathiri utekelezaji wa kanuni hizo, zikiwemo matarajio makubwa ya jamii zinazozunguka migodi kulinganisha na uwezo wa wachimbaji, uelewa mdogo wa kanuni kwa baadhi ya wamiliki wa leseni, pamoja na mivutano ya wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa na watendaji wa halmashauri.

Amesema kuna umuhimu wa kuandaliwa kwa jukwaa pana la kitaifa litakalowakutanisha wadau wote ili kujadili mafanikio, changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha utekelezaji wa miradi ya CSR nchini.

“Jukwaa hilo litawakutanisha wamiliki wa leseni za madini, watendaji wa halmashauri, waratibu wa CSR wa mikoa, Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa, pamoja na wadau kutoka OWM-TAMISEMI na Wizara ya Fedha,” amesema Dkt. Numbi.

Amesisitiza kuwa madini ni rasilimali isiyorejea, hivyo usimamizi madhubuti wa miradi ya CSR ni muhimu ili kuhakikisha jamii zinazozunguka migodi zinapata manufaa stahiki na kuchangia maendeleo ya taifa.

“Tusipojipanga vizuri kama taasisi za Serikali kusimamia utekelezaji wa miradi ya CSR, jamii hazitanufaika ipasavyo na hatimaye taifa litapoteza fursa muhimu za maendeleo,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Alfao Sanga, amesema uwepo wa Kanuni na Miongozo ya CSR umeleta mafanikio makubwa katika uratibu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye halmashauri mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hadi kufikia mwezi Februari 2026, miradi ya CSR yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 28 ilikuwa imetekelezwa katika sekta mbalimbali, ambapo Sekta ya Madini pekee imechangia takribani Shilingi bilioni 19.7.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha mchango mkubwa wa Sekta ya Madini katika maendeleo ya jamii na ustawi wa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka shughuli za uchimbaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad