Na: Calvin Gwabara – Morogoro.
Wakulima wa kilimo cha mpunga
kinachotegemea mvua nchini wamewashukuru watafiti wa Mradi wa Mpunga Himilivu
kwa Mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira barani Afrika (CERA) kwa
jitihada walizozianzisha kuzalisha mbegu bora ya mpunga unaohimili changamoto
za hali ya hewa ili kuinua kipato cha wakulima wa zao hilo Afrika.
| Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Dkt. Atugonza Bilaro akifafanua jambo kwa wakulima wakati wa zoezi hilo Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro. |
Hayo yamebainishwa na wakulima
kutoka mikoa ya Morogoro, Shinyanga na Songwe wakati wa zoezi la ukusanyaji wa
takwimu za awali na taarifa mbalimbali muhimu zitakazosaidia watafiti hao
kuweza kujua changamoto wanazokabiliana nazo katika kilimo hicho ili kuweza
kusaidia wao kuzalisha mbegu mpya zilizoboreshwa ambazo zitaweza kuhimili
mabadiliko hayo ya tabia nchi.
Ukusanyaji huo wa takwimu
umefanyika kwa ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) na Taasisi
ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), katika vijiji nane ukishirikisha wakulima
wapatao 258.
Akizungumza na watafiti hao mkulima
Bwana Maroja Shana kutoka Kijiji cha Silela kata ya Shilela Halmashauri ya
Wilaya ya Msalala Mkoani Shinyanga amesema kuwa ujio wa mradi huo ni ukombozi
kwa wakulima wengi wa mpunga nchini ambao wanalima kwa kutegemea mvua na hasa
kwenye wilaya yao ambayo zao kubwa la bishara na chakula ni mpunga.
“Zamani tulikuwa tunategemea mvua
za msimu ambazo zilikuwa zinanyesha kwa utaratibu unaotabirika, lakini sasa
hali imebadilika kabisa maana mvua zinachelewa kuanza au zinanyesha kwa vipindi
vifupi sana na kusababisha maji kukosekana mashambani. Hali hii imeathiri sana
uzalishaji wangu wa mpunga kwa sababu zao hili linahitaji maji ya kutosha ili
likue vizuri. Mara nyingi hulazimika kupanda mara kadhaa bila mafanikio, jambo
linaloniongezea gharama na kunipunguzia kipato” alieleza Bwana Shana.
Aliongeza “kutokana na ukame huu
wa mara kwa mara, maisha yangu na familia yangu yamekuwa magumu zaidi kwani mavuno
yanapopungua, hata chakula cha nyumbani kinakuwa hakitoshi, na wakati mwingine
nalazimika kununua chakula ambacho ningepaswa kukizalisha mwenyewe. Pia
nashindwa kumudu gharama za pembejeo bora kama mbegu na mbolea, jambo
linaloendelea kudidimiza uzalishaji wangu na hali hii inanifanya nitafakari
njia mbadala za kilimo, lakini bado nahitaji msaada wa kitaalamu na mbegu bora
ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kuendelea kujikimu
kupitia kilimo cha mpunga”.
Kwa upande wake Zilpa Simchimba,
mkulima mwanamke wa mpunga kutoka Wilaya ya Momba Mkoani Songwe amesema kuwa
mvua zimekuwa hazitabiriki. Wakati mwingine hazinyeshi kabisa au zinanyesha kwa
muda mfupi usiotosha kukua kwa mpunga hali ambayo husababisha mashamba kukauka
mapema na kuathiri ukuaji wa zao hilo linalotegemewa sana na familia yake kwa
chakula na kipato.
“Nikiwa kama mama, changamoto
hizi zinaniumiza zaidi kwa sababu nabeba jukumu la kuhakikisha familia inapata
milo ya kila siku na ninapopata mavuno kidogo hulazimika kugawanya chakula kwa uangalifu
au wakati mwingine kupunguza idadi ya milo kwa siku ili kukidhi mahitaji ya
watoto wangu. Pia huwa nalazimika kuuza sehemu ya mazao kidogo ninayopata ili
kukidhi mahitaji mengine muhimu kama ada za shule na huduma za afya, jambo
linalozidi kupunguza akiba ya chakula nyumbani” alieleza Zilpa.
Aliongeza “ninaamini kuwa
jitihada hizi za watafiti za kutafiti na kuzalisha mbegu za mpunga zinazoweza
kuhimili ukame na mabadiliko ya tabia nchi, zinaweza kubadilisha maisha yetu na
ya wakulima wengine wanawake, lakini nasisitiza pia tupewe elimu sahihi ya
kupambana na changamoto hii wakati tukisubiria kazi hii kubwa waliyoianza
watafiti wa mradi huu wa CERA”.
Akizungumza na wakulima wa Wilaya
ya Kilosa Mkoani Morogoro wakati wa zoezi la ukusanyaji wa taarifa za awali za
utafiti, Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa CERA, Prof. Suzan Nchimbi Msolla kutoka
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), amesema kuwa mradi huo unalenga
kuimarisha ustahimilivu wa zao la mpunga dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi,
hususan ukame, kwa wakulima wa Tanzania na Kenya.
![]() |
| Mtafiti Mkuu wa Mradi huo wa CERA, Prof. Suzan Nchimbi Msolla kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) akizungumza malengo ya zoezi hilo na Mradi wa CERA kwa wakulima wa Mpunga Afrika. |
Prof. Msolla ameeleza kuwa miongoni mwa malengo makuu ni pamoja na kupunguza pengo la kijinsia kwa kuwawezesha zaidi wakulima wanawake, hasa wanaoongoza kaya, kupitia uelewa wa mazingira yao na namna jamii zinavyokabiliana na ukame.
“Mradi huu utajikita pia
katika kuendeleza mbegu bora za mpunga zinazoweza kuhimili ukame kwa kuingiza
sifa za ustahimilivu kwenye mbegu zinazopendwa na wakulima na zinazokidhi
mazingira ya ndani. Sambamba na hilo, watafiti watatekeleza mbinu bora za
kilimo katika maeneo yenye ukame, ikiwemo matumizi ya upandaji wa moja kwa moja
na kilimo cha mzunguko ili kupunguza matumizi ya maji na uzalishaji wa gesi
chafuzi na kujenga uwezo wa taasisi za ndani kupitia mafunzo na uwekezaji
katika miundombinu ya utafiti” Alifafanua Prof. Msolla.
Kwa mujibu wa Prof. Msolla, matokeo
yanayotarajiwa ni pamoja na kuimarika kwa usalama wa chakula na kupungua kwa
athari za ukame kwa wakulima, hasa kupitia matumizi ya mbegu zinazostahimili
ukame na mbinu bora za kilimo.
Aidha amesema mradi huo
utachangia kuongeza uzalishaji na kipato kwa wakulima, huku ukipunguza matumizi
ya maji na kulinda mazingira. Pia, mradi utaimarisha ushirikiano wa kikanda na
kimataifa katika utafiti wa mpunga na kusaidia taasisi za ndani kuwa na uwezo
endelevu wa kufanya tafiti na kuzalisha teknolojia zitakazowanufaisha wakulima
kwa muda mrefu.
Mradi huu unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Mpunga (IRRI), Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (KALRO), na Chuo Kikuu cha Copenhagen kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Denmark (DANIDA).
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA ZOEZI HILO LA UKUSANYAJI WA TAKWIMU
| Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi huo Dkt. Emanuel Malisa akizungumza na wakulima kuhusu zoezi hilo la ukusanyaji wa takwimu linavyofanyika. |
| Wakulima wa kilimo cha mpunga kinachotegemea Mvua wakifuatilia maelezo ya watafiti kabla ya kuanza zoezi la udodosaji. |
| Mtafiti kutoka SUA Bi. Rehema Mollel akizungumza na mkulima wa mpunga kwenye kijiji cha Madoto Wilayani Kilosa. |



No comments:
Post a Comment