KAMPUNI ya Miracle Concierge imetangaza kufungua kituo kipya cha abiria chenye huduma maalum kiitwacho Uhuru Terminal & Lounge katika uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro kuanzia Julai 1, 2026, hatua inayolenga kuboresha uzoefu wa safari kwa wageni wanaotumia ukanda wa utalii wa kaskazini mwa Tanzania.
Kituo hicho kinatajwa kuwa miongoni mwa vituo vya kwanza vya binafsi katika kanda ya Kaskazini mwa Tanzania, kikilenga kuwapatia wasafiri huduma ya faragha na urahisi zaidi tofauti na vituo vikuu ya abiria.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, kituo hicho kitatoa huduma maalum zikiwemo usajili wa safari (check-in), msaada wa huduma za uhamiaji pamoja na taratibu za kupanda ndege, hali itakayowezesha wageni kuepuka msongamano wa abiria katika kituo kikuu.
Mradi huo hivi karibuni ulitembelewa na kufanyiwa ukaguzi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo, pamoja na Mkurugenzi wa Kiwanja cha ndege cha Kilimanjaro, Injinia Rehema Myeya, wakiongozana na viongozi wengine wa uwanja huo wakati ujenzi ukiendelea.
Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro ni lango muhimu kwa watalii wanaotembelea vivutio vikuu vya utalii kaskazini mwa Tanzania ikiwemo Mbuga ya wanyama ya Serengeti, Hifadhi Ngorongoro na Mlima Kilimanjaro. Miracle Concierge imesema ujenzi wa Kituo hiyo unalenga kurahisisha safari kwa kupunguza ucheleweshaji na kuongeza faraja kwa abiria wanaowasili na wanaoondoka.
Kituo hicho kitakuwa na muundo wa ghorofa mbili uliobuniwa kwa kuzingatia mandhari ya utamaduni wa Tanzania. Ndani yake kutakuwa na maeneo ya mapumziko yenye vinywaji, vyumba vya kuoga na sehemu tulivu za kukaa.
Pia kutakuwepo vyumba binafsi vya kupumzikia, vyumba vya mikutano na maeneo ya uratibu kwa waendeshaji wa utalii na washirika wa safari.
Akizungumza Aprili 8, 2026, Mwanzilishi na Mtendaji Mkuu wa Miracle Collection, Hasnain Sajan, alisema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kuboresha safari za wageni wanaotembelea Tanzania.
Alisema lengo lao ni kuondoa changamoto katika safari za wasafiri na kuhakikisha kila hatua ya safari inakuwa rahisi, ya faragha na yenye mpangilio mzuri tangu mgeni anapowasili.
Aidha,Kituo cha Uhuru ni sehemu ya mtandao unaokua wa huduma za ukarimu unaoendeshwa na Miracle Collection nchini, ukiwemo Boma Lounge iliyopo Arusha na Ziwani Lounge iliyopo Ziwa Manyara, huku kituo kingine cha aina hiyo kikitarajiwa kujengwa Dar es Salaam.
Huduma za kituo hicho zitapatikana kupitia vifurushi vinavyohitaji kuweka nafasi mapema, huku idadi ya watumiaji ikidhibitiwa kulingana na muda na nafasi zilizopo.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, vifurushi hivyo vitajumuisha msaada wa huduma za uhamiaji, urahisishaji wa ukaguzi wa usalama, matumizi ya lounge, vinywaji, vyumba vya kuoga, maeneo ya kuchezea watoto pamoja na sehemu tulivu za kupumzika.
Gharama za huduma zitajumuisha kodi ya ongezeko la thamani (VAT), huku watoto walio chini ya miaka miwili wakiruhusiwa kutumia huduma hizo bila malipo.
Miracle Concierge imesema ujenzi wa mradi huo unaendelea vizuri na unatarajiwa kukamilika kwa wakati ili uzinduliwe rasmi Julai 2026.
.jpeg)



No comments:
Post a Comment