Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Dkt Mwigulu Nchemba, ametoa onyo kali kwa watu wanaodaiwa kuwa na njama za kuvuruga amani ya nchi, akiwataka Watanzania wote kuendelea kuwa walinzi wa kwanza wa utulivu na mshikamano wa taifa. Amesema kuwa amani ya Tanzania si jambo la kubahatisha, bali ni tunu inayopaswa kulindwa kwa nguvu zote na kila mwananchi.
Akizungumza jijini Dodoma, katika wilaya ya Chamwino, Dkt Mwigulu alionyesha msimamo thabiti wa serikali katika kuhakikisha hakuna mtu au kundi litakaloruhusiwa kuchezea amani ya nchi. Amesisitiza kuwa vyombo vya dola viko macho na vitachukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayebainika kuhatarisha usalama na utulivu wa taifa.
Mbali na hilo, Waziri Mkuu ameelekeza ujumbe kwa viongozi wa umma, akiwataka kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na uwajibikaji wa hali ya juu. Amekemea vikali vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka, akisisitiza kuwa serikali haitamvumilia kiongozi yeyote atakayekiuka maadili ya utumishi wa umma.
Amefafanua kuwa anafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo nchini ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana kwa wananchi. “Kila mradi ninaangalia, kila hatua inafuatiliwa. Atakayekwenda kinyume, hatabaki salama kwenye nafasi yake,” alisisitiza, akionyesha dhamira ya serikali kusimamia rasilimali za umma kwa umakini mkubwa.
Dkt Mwigulu amegusia pia suala la haki kwa wananchi, akionya kuwa hatasita kuwachukulia hatua wale wote wanaowaonea wengine au kukandamiza haki za wananchi. Kauli yake ya, “Wale wanaowaonea wengine nitashughulika nao, msiwe na mashaka — upele umepata mkunaji,” ilizua hisia za matumaini kwa wananchi kuhusu hatua madhubuti zitakazochukuliwa dhidi ya vitendo vya dhuluma.
Aidha, amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na serikali katika kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha maendeleo yanawafikia wote kwa usawa. Amesisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani, nidhamu na uwajibikaji wa pamoja.
Kauli hizo zinakuja wakati serikali ikiendelea kuimarisha misingi ya utawala bora, kupambana na rushwa, na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo kwa lengo la kujenga taifa lenye uchumi imara na ustawi wa wananchi wake.
.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)



No comments:
Post a Comment