Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi za Benki ya Dunia, jijini Washington D.C Nchini Marekani, katika Mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na IMF (2026 IMF/WBG Spring Meetings) inayofanyika, Jijini humo, ambapo Balozi Omar alishukuru uamuzi wa Benki ya Dunia, Kupitia Bodi yake ya Wakurugenzi, kuidhinishia Tanzania dola za Marekani milioni 550 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya kimkakati katika sekta za elimu na kusaidia kaya masikini.
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
BENKI ya Dunia, Kupitia Bodi yake ya Wakurugenzi, imeiidhinishia Tanzania dola za Marekani milioni 550 sawa na zaidi ya shilingi trilioni 1.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya kimkakati katika sekta za elimu na kusaidia kaya masikini.
Uamuzi huo wa Benki umetangazwa na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini, Dkt. Ndiame Diop, alipokutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, pembezoni mwa Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, Makao Makuu wa Taasisi hizo Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Kati ya fedha hizo, dola za Marekani milioni 300 zitatumika kusaidia program ya elimu ya kuongeza ujuzi hususana kwa vijana na kiasi kingine cha dola za Marekani milioni 250 kitatumika kwa ajili ya kusaidia program ya kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF
Dkt. Diop alisema kuwa uamuzi huo unafuatia uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na Benki hiyo pamoja na utekelezaji mzuri wa miradi inayofadhiliwa na Benki, pamoja na usimamizi mzuri wa sera zake za uchumi na fedha.
Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia aliahidi kuwa Benki inaendelea kuchakata miradi mingine ya kimkakati iliyowasiliashwa na Tanzania kwa ajili ya kupata ufadhili wa Benki ikiwemo sekta ya nishati, kilimobiashara, miradi ya afya Zanzibar na mingine ili kuiwezesha Tanzania kufikia malengo iliyojiwekea katika kukuza uchumi na maisha ya wananchi.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, aliishukuru Benki ya Dunia kwa kupitisha miradi hiyo miwili ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi pamoja na majadiliamo yenye tija kwenye maeneo ya miradi muhimu ya maendeleo kwacnchi.
“Pia tumejadili kuhusu maendeleo ya ushoroba wa usafirishaji ambao ni suala muhimu pia ambapo tumeangazia namna korido ya usafirishaji ambayo nchi imewekeza kiasi kikubwa cha fedha ikiwemo reli ya SGR inavyoweza kuchochea uchumi kujumishi na endelevu” alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake, Mwakilishi Mkaazi wa Benki ya Dunia anayemaliza muda wake Bw. Nathan Belete, alisema kuwa kikao cha Mhe. Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Mdiame Diop kilikuwa cha manufaa makubwa na kinaendelea kuonesha namna Benki inavyothamini mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii yanayoendelea nchini Tanzania.
“Ninaondoka Tanzania nikiwa na furaha kubwa na nimaamini uhusiano wa Benki na Tanzania utaendelea kuwa imara na nchi itaendelea kuwa moja ya nchi kubwa kiuchumi katika bara la Afrika kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo” alisema Bw. Belete.
Uwekezaji wa Benki ya Dunia nchini Tanzania Kupitia Dirisha la IDA umefikia dola za Marekani bilioni 8.96 ukihusisha miradi 35 ambapo miradi 32 yenye thamaniya dola za Marekani ni ya kitaifa na miradi mitatu yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 0.18 ni ya kikanda.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Fedha na Mipango kutoka Ofisi ya Rais-Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Mipango, ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Tausi Kida, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Bw. Aboud Hassan Mwinyi, na Viongozi wengine waaandamizi wa Taasisi za Serikali.





No comments:
Post a Comment