JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Vijana 50,000 Kunufaika na Mpango wa Serikali wa Uwekezaji ifikapo 2030

Share This

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo akizungumza na wananchi wakati wa uzinduzi wa  Kituo cha Pamoja cha Kuwezesha Manunuzi na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Centre) katika eneo maalum la uwekezaji la Benjamin William Mkapa SEZ lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam, uzinduzi huo umefanyika leo Machi 14, 2026.

 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo akishirikiana na viongozi wengine kukata utepe kuashiria uzinduzi wa  Kituo cha Pamoja cha Kuwezesha Manunuzi na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Centre) katika eneo maalum la uwekezaji la Benjamin William Mkapa SEZ lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam, uzinduzi huo umefanyika leo Machi 14, 2026.

Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imezindua programu maalumu inayolenga kuwaunganisha vijana na masoko ya kimataifa kupitia mafunzo ya uwekezaji na ujasiriamali, hatua inayotarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi wa viwanda na biashara ya kimataifa.

Akizindua programu hiyo Machi 14, 2026 pamoja na Kituo cha Pamoja cha Kuwezesha Manunuzi na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Centre) katika eneo maalum la uwekezaji la Benjamin William Mkapa SEZ lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais–Mipango na Uwekezaji, Kitila Mkumbo, amesema lengo la mpango huo ni kuwajengea vijana uwezo wa kuzalisha bidhaa zenye ushindani katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesema kupitia programu hiyo vijana watapatiwa mafunzo ya ujasiriamali, uzalishaji wa viwandani pamoja na mbinu za kufikia masoko ya ndani na nje ya nchi, huku wakitumia miundombinu ya maeneo maalum ya kiuchumi kujifunza viwango vya uzalishaji vinavyokubalika kimataifa.

Kwa mujibu wa waziri huyo, amesema awamu ya kwanza itahusisha vijana kati ya 30 hadi 50 watakaopatiwa mafunzo kwa muda wa wiki nane, yakijumuisha elimu ya biashara, mbinu za kuongeza thamani ya bidhaa na uelewa wa mifumo ya biashara ya kimataifa.

Ameeleza kuwa katika hatua ya mwanzo programu hiyo itajikita katika uzalishaji wa bidhaa za chakula zilizokaushwa kama matunda, mboga na viungo, huku washiriki wakitarajiwa kuunganishwa na masoko ya nje ikiwemo Dubai, China na Turkey.

Kitila Mkumbo amesema ifikapo mwaka 2030 mpango huo unatarajiwa kuwawezesha vijana kati ya 50,000 hadi 100,000 kuanzisha na kuendesha biashara mbalimbali, sambamba na kuanzishwa kwa takribani biashara 5,000 ndani ya maeneo maalum ya kiuchumi nchini.

Aidha, amesema utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kuchochea ajira kati ya milioni moja hadi tatu za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kupitia shughuli za uzalishaji, usindikaji na huduma zinazohusiana na viwanda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, amesema mpango huo umeundwa ili kuwapa vijana mafunzo ya vitendo yanayofanyika moja kwa moja katika mazingira ya uzalishaji viwandani.

Amesema mfumo huo utawawezesha washiriki kujifunza kwa kutumia miundombinu iliyopo katika maeneo maalum ya kiuchumi, hatua itakayosaidia kukuza ujuzi wa uzalishaji, kuongeza thamani ya bidhaa na kuimarisha ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la kimataifa.

Teri pia amebainisha kuwa moja ya changamoto zinazoathiri uzalishaji ni pamoja na ukosefu wa viwango vya kitaifa kwa baadhi ya bidhaa pamoja na uhusiano hafifu kati ya wazalishaji na masoko, hali ambayo programu hiyo inalenga kuirekebisha kwa kuimarisha mfumo wa uzalishaji unaozingatia mahitaji ya soko.

Ameongeza kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho cha pamoja kumetokana na juhudi za serikali katika kuvutia uwekezaji, akitaja ziara ya Kassim Majaliwa nchini China kuwa miongoni mwa hatua zilizoleta ushirikiano huo, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa pamoja ili kufanikisha maendeleo ya kiuchumi.

Aidha, ametoa shukrani kwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara nchini, jambo linalochangia kuvutia wawekezaji na kuimarisha ukuaji wa sekta ya viwanda.

Licha ya uzinduzi wa Kituo cha Pamoja cha Kuwezesha Manunuzi na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Centre) pamoja na Programu ya Mafunzo ya Wawekezaji Vijana katika eneo maalum la uwekezaji la Benjamin William Mkapa SEZ lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam pia amezindua programu ya mawasiliano ya Ongea na Waziri Kitila Mkumbo moja kwa moja  ambayo itakuwa ikifanyika kila wiki kwa masaa matatu kupitia namba ya simu pamoja na mitandao ya kijamii. Ambapo mwananchi ataweza kupiga simu, kuuliza maswali, kutoa ushauri pamoja na kutoa maoni mbalimbali kuhusiana na mambo ya uwekezaji nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri,  akizungumza wakati wa tukio la uzinduzi wa  Kituo cha Pamoja cha Kuwezesha Manunuzi na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Centre) katika eneo maalum la uwekezaji la Benjamin William Mkapa SEZ lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam, uzinduzi huo umefanyika leo Machi 14, 2026.




No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad