JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Vifo 556 hadi 104: Jinsi Tanzania ilivyopunguza vifo vya uzazi kwa kinamama

Share This

 


Mwandishi Wetu,
Dar es Salaam. 
TAKWIMU kutoka cha Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa Afrika (CDC-Afrika) zinaonyesha kuwa, vifo vya uzazi Tanzania vimepungua kwa asilimia 80 kutoka 556 katika kila vizazi hai 100000 mwaka 2016 hadi 104 katika kila vizaizi hai 100000 mwaka 2022.

Katika mgawanyo wa vifo 556 katika kila vizazi hai 100,000, kwa mwaka ni sawa na vifo 2 kila siku vinavyotokana na uzazi kwa kinamama.

Laiti ingekuwa basi la moja la abiria kila linapokwenda katika safari zake linapata ajali na kuua watu wawili kila siku, basi hilo lingetazamwa kama janga kubwa kwa taifa na maswali mengi angehojiwa dereva na mmiliki wa basi.

Na hali hiyo ndiyo iliyosababisha serikali kuamua kulivalia njuga suala la vifo vya uzazi kwa kinamama.

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Irene Barongo, vifo vya uzazi kwa kinamama vilikuwa saba katika mwaka wa fedha, 2023/2024 na mwaka jana, kulikuwa na vifo vitatu tu.

“Kuna mengi yamefanywa, kwa kupitia ‘Mama Samia Sponsorship’ madaktari bingwa wamesomeshwa ambao wanarudi katika hospitali, hali ambayo imechangia kupunguza vifo vya uzazi kwa kiasi kikubwa,” amesema.

Kwa upande wa watoto kadhalika, Hospitali ya Mwananyamala imepunguza vifo vya Watoto. Daktari Bingwa wa Watoto Makena Kato anasema, awali walikuwa wakitegemea vifaa vya kupumulia kwa watoto wenye changamoto kupumua(sipap).

Dk Kanto anasema, awali walikuwa wakitegemea ‘sipap’ moja tu na sasa serikali imeongeza machine zaidi ya 20.

“Kwa mfano mtoto amezaliwa na changamoto ya upumuaji labda kwa sababu alizaliwa kabla ya wakati au njiti, halafu hospitali ina sipap moja, basi hapo ni kupanga foleni, kusubiri mtoto aliyewekwa atoke. Kwa hali ile ni rahisi Watoto kufariki.” anasema

Lakini Dk Kanto anaongelea umuhimu wa afya na uhai wa mama wakati wa kujifungua na kusema, Mungu amemuumba mwanamke kwa namna ya kipekee ili alete uhai duniani, hivyo kupoteza maisha wakati wa kitendo hicho si haki.

Mganga Mfawidhi Mwananyamala, Dk Barongo anafafanua zaidi jinsi ambavyo Mwananyamala wameingilia kati vifo vya uzazi kwa kinamama na kusema kampeni kubwa imefanyika katika suala la kukusanya damu salama,jambo ambalo limepunguza vifo vya uzazi.

Anasema kwa mwaka hospitali inazalisha wanawake kuanzia 5000 mpaka 6000, na vifo vinavyotokea kwa kiasi kikubwa havisababishwi na ukosefu wa damu.

Akiuzungumzia mwezi wa maadhimisho ya wanawake duniani, Dk Barongo anasema, hakuna jambo gumu kama pale ambapo mjamzito anajifungua na kisha anafariki dunia na kumuacha mtoto.

“Lazima ndani ya saa 24, lazima tukae, tuitane, tuulizane nini kimetokea, tunaiita ‘mortality review’ tunaangalia tumekosea wapi. Cha muhimu kusiwepo na vifo vya wanawake wakati wa uzazi, kwa sababu mama kama kiumbe anayeleta uhai duniani, hastahili kufa”anasema na kuongeza:

“Kikitokea kifo cha mwanamke wakati wa kujifungua na akabaki mtoto salama, tunajiuliza maswali mengi, huyu mtoto atabaki na nani, atanyonya nini? Atalelewa na nani? Ni vifo vinavyoumiza sana”

Dk Barongo anasema katika kupunguza vifo vya uzazi hata wauguzi na madaktari wanasimamiwa katika kubadili mitazamo na kuondoa lugha chafu kwa wagonjwa wakiwamo wajawazito.

Anaongeza kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilibeba suala la afya ya uzazi kwa kinamama kama mama akitambua nafasi ya uzazi kwenye jamii.

“Kwa kweli katika awamu hii tumeona, yule ni mama na ninavyoona katika uongozi wake ameamua kumuangalia mama na mtoto, na kiuhalisia katika uwekezaji uliowekwa kwenye sekta ya afya, hakuna kifaa ambacho tutakiomba tukanyimwa na hiyo imesaidia sana kupunguza vifo vya kinamama,” anasema na kuongeza:

‘Kila mahali mama Samia amewekeza kwenye afya ya mama na mtoto, kwa kweli kama ni kutajwa kuwa kinara wa afya ya mama na mtoto anastahili,”

Malengo ya Maendeleo Endelevu(SDG) inataka nchi za Afrika kupunguza vifo vya uzazi hadi kufikia 70 katika kila vizazi hai 100,000. Lakini Tanzania bado haijafikia lengo hilo ingawa jitihada za dhati na matokeo yameonekana kwa asilimia 80.

HOSPITALI YA AMANA
Mkunga Mbobezi, Joyce Njenga wa Hospitali ya Rufaa ya Amana anasema, miaka mitano iliyopita, Amana ilikuwa ina idadi kubwa ya vifo vya uzazi kwa kinamama, kwa mfano mwaka 2023, kinamama 12 walifariki kwa mwaka kwa sababu ya uzazi na mpaka mwaka jana kulikuwa na vifo viwili tu.

“Hii inatokana na kuongezwa kwa vifaa tiba ikiwamo machine ya ‘ultrasound’ kingine ni ushirikiano katika kufanya kazi, akifika tu anaangaliwa anahitaji huduma gani, kwa wanaohitaji upasuaji, ndani ya nusu saa anaandaliwa na kupelekwa chumba cha upasuaji” anasema

Anasema katika hospitali ya Amana kuna madaktari bingwa wa nane wa masuala ya uzazi na wakunga wabobezi watatu.

“Zamani mkunga mmoja anazalisha Watoto sita hadi saba peke yake, sasa hivi huduma za afya zimeimarishwa zaidi katika hospitali za pembezoni na kusaidia kupunguza mzigo wa wagonjwa katika hospitali za rufaa” anasema.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Amana, Dk Bryson Kiwale anasema vifo 556 ni sawa na mabasi kadhaa ya abiria yaanguke na yasababishe vifo.

Anasema, kama mabasi hayo yangeanguka na kuua, pengine ungetangazwa msiba mzito kwa taifa lakini kwa sababu ni msiba unaoikuta familia moja, na sehemu nyingine familia moja, watu hawaoni ukubwa wa vifo hivi.

“Ni dhamira ya kweli ya serikali na wala hakuna muujiza, serikali imeamua kuwekeza katika afya ya msingi, ikiwamo mafunzo na utayari wa watoa huduma katika sekta ya afya,” anasema

Daktari Bingwa wa Watoto, Hospitali ya Amana, Grace Mhando anasema ingawa vifo vya watoto bado ni changamoto lakini vimepungua.

Anasema kwa sasa Tanzania inazungumzia vifo vya Watoto 24 katika kila vizazi hai 1000 hali ambayo bado tunaweza kusema bado hatujafikia lengo la kidunia la kupunguza vifo hivyo hadi kufikia 12 katika kila vizazi hai 1000.

“Lakini tumeona juhudi za serikali, kwa kupitia ‘Mama Samia Sponsorship’ madaktari bingwa wanaendea mpaka vijijini kuwahudumia Watoto ambao wana hali ya chini.

Ripoti iliyochapishwa Januari mwaka 2025 na Jarida la Afya la Uingereza, imeonyesha kuwa program zilizofanyika zikihusisha serikali, taasisi za afya na wataalamu wa afya, zimewezesha kupunguza kwa asilimia 75 vifo vya uzazi katika kipindi cha miaka mitatu.

Utafiti huo ulifanywa katika vituo 30 vya afya vinavyopokea wagonjwa wengi Tanzania na matokeo yalibainisha kuwa maelfu ya kinamama waliepuka vifo vya uzazi kwa kutumia program zilizowekwa na vifaa tiba vilivyotolewa na serikali na wadau wa maendeleo.

Februari mwaka jana, Taasisi ya Gates, ilimpa Rais Samia Suluhu tuzo maalum ya Goalkeepers ya kutambua mchango wake katika kuboresha afya ya mama na mtoto na lishe. Rais aliitoa tuzo hiyo kwa wafanyakazi wote wa sekta ya afya kwa mchango wao katika kupunguza vifo hivyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad