JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


TPSC Yawajengea Vijana Misingi ya Maadili na Uzalendo Kuelekea Maadhimisho ya Miaka 25

Share This

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Kuelekea maadhimisho ya miaka 25 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Mkurugenzi wa chuo hicho Kampasi ya Dar es Salaam, Mussa Lugembe, amewataka wanafunzi wa vyuo na shule za sekondari kuwa waadilifu na wazalendo ili kujenga msingi imara wa utumishi wa umma wenye uwajibikaji nchini.

Lugembe alitoa wito huo alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Azania jijini Dar es Salaam, ambapo alisema chuo hicho kimeanza kutoa elimu ya maadili na uzalendo kwa vijana ili kuwajengea uelewa mapema kuhusu misingi ya utumishi wa umma kabla hawajaingia rasmi katika ajira za serikali.

Alieleza kuwa lengo la mpango huo ni kuwaandaa watumishi wa umma wa baadaye wanaotambua wajibu wao kwa taifa, wanaozingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na uzalendo wanapokuwa katika nafasi mbalimbali za utumishi wa umma.

“Tunataka vijana waanze kujifunza mapema kuhusu maadili ya utumishi wa umma ili wanapopata nafasi za ajira wawe tayari kulitumikia taifa kwa uadilifu, uwajibikaji na uzalendo,” alisema Lugembe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Azania, Melsius Kayombo, aliipongeza TPSC kwa kuandaa programu hiyo ya utoaji elimu kwa wanafunzi akisema itawasaidia kujenga misingi imara ya maisha na kuwalea kuwa viongozi na watumishi wa umma wenye maadili katika siku zijazo.

Naye mwanafunzi wa Azania, Faidh Mussa, alisema elimu hiyo imewasaidia wanafunzi kuelewa umuhimu wa uzalendo, uwajibikaji na maadili katika kujenga taifa lenye maendeleo.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Mwishehe Ming’uno, alisema mafunzo hayo yanawapa motisha wanafunzi kuzingatia maadili ya kazi na kujiandaa kuwa watumishi wa umma watakaolitumikia taifa kwa ufanisi na uadilifu.

Aidha, Lugembe alibainisha kuwa katika kuadhimisha miaka 25 ya chuo hicho, Kampasi ya Dar es Salaam tayari imeshatembelea shule mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Benjamin Mkapa, Jangwani, Tambaza na Azania, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu maadili, uzalendo na umuhimu wa kuwajibika kwa taifa.












 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad