Na: Calvin Gwabara – Morogoro Tanzania.
Mradi
wa Mpunga Himilivu kwa mabadiliko ya Tabianchi na Rafiki kwa Mazingira Barani
Afrika (Climate-resilient and Eco-friendly Rice for Africa) (CERA) umechukua
hatua muhimu katika kuboresha kilimo cha mpunga kwa kuendesha mafunzo maalum
kwa wakusanyaji takwimu katika utafiti unaotarajia kufanyika kwenye Mikoa ya
Morogoro, Shinyanga na Songwe nchini Tanzania.
![]() |
| Mtafiti Mkuu wa mradi Prof. Suzana Nchimbi Msolla akizungumza na watafiti hao kabla ya kuanza zoezi hilo. |
Mafunzo
hayo yamewaleta pamoja washiriki ambao watakuwa mstari wa mbele katika
ukusanyaji wa taarifa kutoka kwa wakulima, hatua inayotarajiwa kusaidia kufanya
maamuzi sahihi ya kisayansi kwenye utekelezaji wa mradi huo wa utafiti.
Akizungumza
na watafiti hao wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mtafiti Mkuu wa mradi Prof.
Suzana Nchimbi Msolla alitumia nafasi hiyo kueleza kwa kina kuhusu mradi wa
CERA, akieleza malengo, muda wake pamoja na matarajio yake hasa katika kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Prof.
Msolla ameeleza kuwa mradi huo unalenga kuzalisha mbegu za mpunga
zinazostahimili ukame pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbinu rafiki kwa
mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoleta athari
kubwa katika uzalishaji wa mazao hasa zao la mpunga nchini Tanzania.
Aidha,
amesisitiza umuhimu wa wa watafiti hao kwenda kuzingatia usawa wa kijinsia kwa
kueleza kuwa mradi unalenga kuwafikia zaidi wakulima wanawake katika maeneo
yenye ukame ili kuhakikisha wanufaika wote wanashirikishwa.
Mtafiti
huyo pia alizungumzia suala la kujenga uwezo kwa taasisi za ndani kwa kutoa
mafunzo kwa watafiti na kuboresha miundombinu ya utafiti wa kilimo.
“Ubora
wa takwimu mtakazokusanya ndio utakaoamua mafanikio ya mradi huu na utekelezaji
wake hivyo nisihi kutumia utaalamu mlionao na huu mtakaopewa kwenye mafunzo
haya kuhakikisha mnapata taarifa sahihi kutoka kwa wakulima,” alisisitiza Prof.
Msolla.
Kwa
upande wake Mtafiti Mkuu Msaidizi wa mradi huo Dkt. Emanuel Malisa, ambaye aliwasilisha
mada kuhusu wajibu, maadili na mwenendo wa wakusanyaji takwimu katika kazi za
utafiti amesema wakusanyaji takwimu wanapaswa kuwa waaminifu, wasiwe na
upendeleo, walinde siri za washiriki, na wahakikishe wanapata ridhaa ya
washiriki kabla ya kuanza mahojiano.
Dkt.
Malisa aliongeza kuwa wakusanyaji takwimu hao wanawakilisha mradi mbele ya
jamii, hivyo wanapaswa kuzingatia heshima na weledi wa hali ya juu katika kazi
zao kwenye kila eneo mabalo watapita kwakuwa tamaduni na mila za maeneo
zinatofautiana hivyo wahakikishe wanazingatia mambo hayo ili waweze kupata
ushirikiano kwa wakulima na jamii watakayoikuta.
Mafunzo
hayo pia yalijumuisha mbinu za kufanya mahojiano, matumizi ya teknolojia ya
ukusanyaji takwimu kama KoboToolbox,
pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto za washiriki kutokutoa taarifa.
Washiriki
walipata fursa ya kufanya mazoezi kwa vitendo kupitia uigaji wa hali halisi ya
kazi (simulation), hatua iliyowawezesha kujiandaa vizuri kabla ya kwenda
kukusanya takwimu halisi kwa wakulima.
Matokeo
ya Utafiti ya mradi wa CERA yanatarajiwa kutoa mchango mkubwa katika kuongeza
uzalishaji wa mpunga, kuimarisha ustahimilivu wa kilimo dhidi ya mabadiliko ya
tabianchi, na kuboresha usalama wa chakula nchini Tanzania na barani Afrika kwa
ujumla.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA MAFUNZO HAYO.







No comments:
Post a Comment