JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Sika Tanzania Yaadhimisha Miaka 10 kwa Kuzindua Mitambo ya Kisasa Dar es Salaam na Mwanza

Share This
Balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Nicole Providoli akishirikiana na viongozi mbalimbali wa Kampuni ya Sika Tanzania wakikata Utepe kuashiria usheherekeaji wa miaka 10 ya kampuni hiyo pamoja na uzinduzi wa mitambo mipya ya kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza. 


KAMPUNI ya kimataifa ya uzalishaji wa kemikali maalum za ujenzi, Sika Tanzania, imeadhimisha miaka 10 ya uwepo wake nchini kwa kuzindua mitambo mipya ya kisasa katika miji ya Dar es Salaam na Mwanza. Hatua hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji wa ndani, kuongeza ajira na kuchochea maendeleo endelevu katika sekta ya ujenzi.

Akizungumza katika hafla ya maadhimisho hayo, Meneja Mkuu wa kampuni hiyo, Dennis Ott, alisema uwekezaji huo unaashiria hatua mpya ya ukuaji wa viwanda na ubunifu nchini. Alieleza kuwa upanuzi wa kiwanda cha Dar es Salaam utaongeza uwezo wa uzalishaji na ufanisi wa shughuli za kampuni.

Ott aliongeza kuwa kiwanda kipya cha Mwanza kimejengwa kimkakati ili kuhudumia Kanda ya Ziwa na maeneo ya Magharibi mwa Tanzania, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa bidhaa za ujenzi na kuimarisha usambazaji wake katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, uwekezaji huo utaongeza uzalishaji wa ndani, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kufungua nafasi mpya za ajira katika sekta za uzalishaji na teknolojia za ujenzi.

Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, Sika Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya ujenzi nchini kupitia teknolojia za kuunganisha, kuziba na kuzuia maji pamoja na suluhisho za kisasa za zege zinazotumika katika miradi mikubwa ya miundombinu.

Kupitia programu ya mafunzo ya Sika Academy, kampuni hiyo imefanikiwa kufundisha zaidi ya mafundi na wakandarasi 5,000 wa ndani, hatua iliyosaidia kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa sekta ya ujenzi nchini.

Aidha, kampuni hiyo imeshiriki katika zaidi ya miradi 100 mikubwa ya miundombinu na biashara nchini, ikiwemo Julius Nyerere Hydropower Project, Standard Gauge Railway na Kijazi Interchange.

Wakati huo huo, Balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Nicole Providoli, amesema Serikali ya Tanzania inaendelea kuunganisha nguvu za wadau mbalimbali kulinda mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza sera na mikakati ya nishati safi, uhifadhi wa rasilimali za asili na matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira ili kulinda ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wake, Meneja wa Usalama Mahali pa Kazi wa Sika Tanzania, Doto Damian, ambaye pia ni mshindi wa tuzo ya usalama mahali pa kazi, amesema kutambuliwa kwake kupitia tuzo hiyo ni motisha kubwa katika kuendelea kuhimiza utamaduni wa usalama kazini. Amesema mafanikio hayo yanatokana na juhudi za pamoja za wafanyakazi na uongozi wa kampuni katika kuhakikisha mazingira ya kazi yanakuwa salama na yenye tija.

Aidha, Damian amesema ameendelea kutoa elimu kwa mafundi na wadau wa sekta ya ujenzi kuhusu matumizi ya teknolojia ya Kiswisi katika ujenzi wa madaraja hapa nchini. Ameeleza kuwa teknolojia hiyo inasaidia kuongeza ubora, uimara na usalama wa miundombinu ya madaraja, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia kanuni za usalama na matumizi sahihi ya vifaa vya kisasa katika miradi ya ujenzi.

Picha ya Pamoja ya Balozi wa Switzerland nchini Tanzania, Nicole Providoli na washindi wa tuzo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad