JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


RAIS DKT. SAMIA APOKEA UJUMBE MAALUM KUTOKA KWA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA

Share This

 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tarehe 11 Machi 2026 amepokea salamu maalum kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, zilizowasilishwa kwake na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu huyo, Bw. Parfait Onanga-Anyanga, katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Mjumbe huyo maalum yuko nchini Tanzania kwa ziara ya kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali na kutathmini hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha utulivu wa kisiasa, mshikamano wa kitaifa na kuendeleza misingi ya utawala wa sheria kufuatia matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea kabla na wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Akizungumza baada ya kukutana na Rais Samia, Bw. Onanga-Anyanga amesema Umoja wa Mataifa unatambua na kupongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania kufuatia matukio hayo, hususan uamuzi wa kuunda Tume Huru ya Uchunguzi pamoja na dhamira ya kufanya mazungumzo jumuishi ya kitaifa na kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya Katiba.

Ameeleza kuwa Tanzania inaendelea kutambuliwa na Umoja wa Mataifa kama nchi yenye historia ya muda mrefu ya amani, utulivu wa kisiasa na mshikamano wa kitaifa, huku pia ikithaminiwa kwa mchango wake katika juhudi za kulinda na kuimarisha amani barani Afrika.

Katika ziara yake nchini, Bw. Onanga-Anyanga amekutana na viongozi wa taasisi mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahakama ya Tanzania, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.

Aidha, amefanya mazungumzo na Mwenyekiti na wajumbe wa Tume Huru ya Uchunguzi pamoja na wadau wengine wa kisiasa na kijamii ili kupata maoni na mitazamo tofauti kuhusu matukio yaliyotokea na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali.

Bw. Onanga-Anyanga amesema mashauriano hayo yatauwezesha Umoja wa Mataifa kupata taswira halisi ya matukio ya Oktoba 29, 2025 pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika kutatua changamoto zilizojitokeza wakati na baada ya uchaguzi huo.

Ameongeza kuwa hatua hizo zina mchango muhimu katika kuimarisha maridhiano ya kitaifa, kurejesha imani ya wananchi na kuendelea kujenga taasisi imara za kidemokrasia nchini. Aidha ameahidi kuwasilisha tathmini ya mashauriano hayo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuendelea kuimarisha mashauriano kati ya Umoja wa Mataifa na Tanzania.

Kwa upande wake, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa salamu za shukrani kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa kutuma ujumbe maalum nchini Tanzania ili kupata uelewa wa kina kuhusu hali ya nchi na kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali.

Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imejizatiti kuhakikisha mchakato wa kufuatilia matukio hayo unafanyika kwa kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na haki, huku ikiendelea kulinda amani, umoja wa kitaifa na utulivu wa kisiasa ambao umekuwa msingi muhimu wa maendeleo ya nchi.

Aidha, amesema Serikali iko tayari kupokea na kuyafanyia kazi mapendekezo yatakayowasilishwa na Tume Huru ya Uchunguzi mara baada ya kukamilika kwa kazi yake, akieleza kuwa mapendekezo hayo yatakuwa sehemu muhimu ya kuimarisha maridhiano ya kitaifa na mchakato wa marekebisho ya Katiba.

Rais Samia pia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Mataifa pamoja na jumuiya nyingine za kimataifa katika kukuza demokrasia, utawala bora na maendeleo jumuishi kwa manufaa ya wananchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad