JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


NBC Yahitimisha Kampeni ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ Mtwara, Yakabidhi Trekta Kwa TANECU

Share This

Katika hatua inayoonyesha dhamira yake ya dhati ya kuinua sekta ya kilimo nchini, Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imehitimisha kwa mafanikio makubwa msimu wa nne wa kampeni yake ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’, kwa kukabidhi zawadi kuu ya trekta kwa mshindi mkuu – Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU).

Kampeni hiyo iliyozinduliwa mwezi Septemba mwaka jana wilayani Tandahimba ililenga kuhamasisha wakulima wa zao la korosho kuongeza uzalishaji kupitia huduma za kifedha zilizo rafiki na bunifu, sambamba na kuwazawadia washiriki kwa vitendea kazi vya kisasa vinavyochochea maendeleo ya kilimo.

Mbali na trekta, kampeni hiyo iliwapatia washindi zawadi mbalimbali ikiwemo simu janja (smartphone), pampu za kupulizia dawa, pikipiki, kompyuta mpakato (laptop) pamoja na mizani za kidijitali—zote zikilenga kuongeza tija kwa mkulima.

Hafla ya kukabidhi trekta hilo ilifanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa 31 wa TANECU uliofanyika wilayani Tandahimba, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Kanali Michael Mntenjele, huku ikihudhuriwa na viongozi wa ushirika, wakulima na maofisa wa NBC wakiongozwa na Meneja wa NBC Tawi la Lindi, Iovin Mapunda, pamoja na Meneja wa Tawi la Tandahimba, Billygraham Minja.

Akizungumza katika hafla hiyo, Kanali Mntenjele aliipongeza NBC kwa mchango wake mkubwa katika kuleta mageuzi ya kweli kwenye kilimo cha korosho wilayani humo.

“Kampeni hii imekuwa kama ukombozi kwa wakulima wetu. Imefungua fursa za kupata mikopo ya zana za kisasa kama matrekta, pembejeo na mitaji ya awali. Hizi si zawadi tu—ni uwekezaji wa moja kwa moja katika kuongeza uzalishaji,” alisema.

Aliongeza kuwa juhudi za NBC zinaendana kikamilifu na mkakati wa Serikali wa kuongeza uzalishaji wa korosho na kukuza uchumi wa wakulima, huku akisisitiza umuhimu wa wataalamu wa kilimo kuendelea kuwafikia wakulima kwa elimu ya kisasa.

Kwa upande wake, Meneja wa NBC Tawi la Lindi, Iovin Mapunda, alisema kampeni hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa benki hiyo kuunga mkono dira ya maendeleo ya taifa, hususan katika sekta ya kilimo.

 

“Kupitia ‘NBC Shambani’, tumerahisisha huduma za kifedha kwa wakulima—ikiwemo akaunti zisizo na makato ya mwezi, mikopo ya zana za kilimo, na mikopo kwa vyama vya ushirika kwa ajili ya pembejeo. Lengo letu ni kuunga mkono jitihaza za serikali za kuongeza uzalishaji kwenye sekta hii kutoka asilimia 5 hadi 10 ifikapo 2030,” alieleza.

Alisisitiza kuwa NBC inaona sekta ya kilimo kama uti wa mgongo wa uchumi wa taifa, hasa ikizingatiwa kuwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanategemea sekta hiyo kwa ajira na kipato.

Naye Meneja wa NBC Tawi la Tandahimba, Billygraham Minja, alisema kampeni hiyo imeleta mapinduzi makubwa kwa wakulima wa Tandahimba na Newala kwa kuwapatia vitendea kazi muhimu vinavyorahisisha shughuli za kilimo.

“Tumeona mabadiliko halisi. Wakulima wameongeza ushiriki wao kwenye huduma za kifedha na wameanza kuendesha shughuli zao za kilimo kwa kutumia zana za kisasa zaidi. TANECU kushinda trekta ni uthibitisho wa mafanikio ya kampeni hii,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TANECU, Karimu Chipola, alieleza shukrani zake kwa NBC, akibainisha kuwa zawadi ya trekta itasaidia kuongeza tija na kufikia malengo ya kuongeza uzalishaji wa korosho mkoani Mtwara.

“Hii ni hatua kubwa kwetu. Tutalitumia trekta hili kuongeza uzalishaji na tutaendelea kushirikiana na NBC kwa kupitisha miamala yetu kupitia ‘NBC Shambani’ ili kufaidika zaidi,” alisema.

Aidha, aliwahimiza wakulima wenzake kuzingatia nidhamu ya fedha, kuhifadhi mapato yao benki na kuwekeza kwenye kilimo cha kisasa ili kujijengea uchumi imara.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara , Kanali Michael Mntenjele, (alieketi kwenye trekta) akishuhudia makabidhiani ya trekta baina ya Meneja wa benki ya NBC Tawi la Lindi, Iovin Mapunda, (kushoto kwake) kwenda kwa Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU), Karimu Chipola,( kulia kwake) ikiwa ni zawadi iliyotolewa na benki hiyo kwa chama hicho  baada ya kuibuka mshindi wa jumla wa kampeni ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ ya benki hiyo iliyokuwa mahususi  kwa wakulima wa Korosho mkoani humo. Wanaoshuhudia ni pamoja na viongozi wa chama hicho, wakulima na maofisa wa NBC.

Mkuu wa Wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara , Kanali Michael Mntenjele, (katikati alieshika mkasi) akikata utepe kuashiria hitimisho rasmi la msimu wa nne wa kampeni ya ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ ya benki ya NBC na makabadhiano rasmi ya zawadi ya trekta iliyotolewa na benki hiyo kwenda Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU)baada ya chama hicho kuibuka mshindi wa jumla wa kampeni hiyo iliyokuwa mahususi kwa wakulima wa Korosho mkoani humoWanaoshuhudia ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Newala, Alhaji Rajabu Kundya (wa pili kulia), viongozi wa ushirika, wakulima na maofisa wa NBC.

Maofisa wa Benki ya NBC wa mikoa ya Lindi na Mtwara wakiongozwa na Meneja wa NBC Tawi la Lindi, Iovin Mapunda (wa kwanza kulia) wakifuatilia Mkutano Mkuu wa 31 wa TANECU uliofanyika wilayani Tandahimba jana muda mfupi kabla ya hafla ya kukabidhi trekta kwa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU)baada ya chama hicho kuibuka mshindi wa jumla wa kampeni ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ ya benki ya NBC iliyokuwa mahususi kwa wakulima wa Korosho mkoani humo.


Baadhi ya wadau wa kilimo cha Korosho mkoani Mtwara wakifuatilia Mkutano huo ulioambatana na hafla ya kukabidhiwa trekta kwa Chama Kikuu cha Ushirika Tandahimba na Newala (TANECU)baada ya chama hicho kuibuka mshindi wa jumla wa kampeni ‘Wekeza NBC Shambani Ushinde’ ya benki ya NBC iliyokuwa mahususi kwa wakulima wa Korosho mkoani humo.


Burudani zikiendelea.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad