
Na John Mapepele
Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema kuwa ushirikiano madhubuti kati ya Serikali na Washirika wa Mfuko wa Pamoja wa Afya (Health Basket Fund) umeendelea kuwa chachu ya maboresho makubwa katika utoaji wa huduma za afya nchini.
Akizungumza katika mkutano wa nchi washirika wa Mfuko huo Machi 2, 2026 jijini Dar es Salaam Mhe. Mchengerwa alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuiwezesha Tanzania kufikia hatua ya kufanya majadiliano muhimu kuhusu mustakabali wa sekta ya afya. Alisisitiza kuwa pale washirika wa sekta ya afya wanapoungana kwa uwazi, dhamira na malengo ya pamoja, maisha ya wananchi huboreshwa kwa haraka zaidi.
“Mkutano huu si wa kawaida. Ni wakati wa kimkakati wa kuimarisha ushirikiano na kuthibitisha upya wajibu wetu wa pamoja wa kutoa huduma bora za afya kwa Watanzania,” alifafanua.
Mfuko wa Pamoja wa Afya Waimarisha Huduma za Msingi nchini
Waziri Mchengerwa alieleza kuwa tangu kuanzishwa kwa Mfuko wa Pamoja wa Afya mwaka 1999, zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.3 zimechangishwa kusaidia utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya sekta ya afya. Asilimia 90 ya fedha hizo zimeelekezwa katika huduma za Afya ya Msingi zinazosimamiwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Alibainisha kuwa kuanzia mwaka 2017, fedha za Mfuko zilianza kupelekwa moja kwa moja katika zaidi ya vituo 7,345 vya afya kupitia utaratibu wa ufadhili wa moja kwa moja kwa Vituo vya Afya, hatua iliyoongeza uwazi na ufanisi katika matumizi ya rasilimali.
“Kwa pamoja tumeimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba muhimu, tumepunguza vifo, na kuongeza uzazi salama katika Vituo vya Afya. Mageuzi haya yameweka msingi imara wa mfumo wa afya wenye ustahimilivu,” alisisitiza.
Msukumo Mpya: Bima ya Afya kwa Wote na Afya Kidijitali
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa alisema Tanzania ipo katika kipindi cha mageuzi makubwa, huku lengo kuu likiwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Alifafanua kuwa wakati bima hiyo ikipanua ulinzi wa kifedha kwa wananchi, Mfuko wa Pamoja wa Afya unabaki kuwa mhimili wa kuhakikisha huduma bora na zenye usawa zinapatikana kwa wote.
Aidha, Waziri huyo alitoa wito kwa washirika kuunga mkono utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Afya Kidijitali uliounganishwa, akisisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo mmoja wa kitaifa unaounganisha taarifa zote za afya.
“Huwezi kusimamia usichokiona, na huwezi kuboresha usichokipima. Mfumo wa kidijitali uliounganishwa ni mageuzi ya utawala, ufanisi na uaminifu,” alisema.
Kujenga Uwezo wa Ndani na Usalama wa Afya
Akizungumzia dira ya muda mrefu, Mhe. Mchengerwa alisema Tanzania inalenga kupunguza utegemezi mkubwa wa bidhaa za afya kutoka nje kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani wa dawa, vifaa tiba na teknolojia za afya.
“Hili si suala la uchumi pekee, bali ni suala la usalama wa afya ya taifa. Mfumo imara wa afya lazima uunganishe ustahimilivu wa kifedha, kidijitali, rasilimali watu pamoja na uzalishaji na ugavi,” alifafanua.
Ushirikiano wa Kushinda kwa Pamoja
Waziri huyo alieleza kuwa mandhari ya maendeleo duniani yanabadilika, huku nchi zikielekea kwenye ushirikiano wa thamani ya pande zote na uendelevu wa muda mrefu.
“Tunaamini mustakabali wa ushirikiano haujengwi juu ya utegemezi, bali ubunifu wa pamoja na uwekezaji. Ushirikiano wenye busara haufiche changamoto; hujifunza kutoka kwake na hubuni mifumo bora zaidi,” alisema.
Alikiri kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa wakati, akieleza kuwa Serikali inafanya kazi kwa karibu na Wizara nyingine ikiwa ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI na Wizara ya Fedha ili kuondoa vikwazo vya kiutendaji na kuimarisha uwazi katika usimamizi wa fedha.
Mabalozi wampongeza Rais Samia kwa kazi kubwa kwenye Sekta ya Afya
Akizungumza kwa niaba ya timu ya mabalozi walioshiriki katika kikao hicho, Mheshimiwa Elke Wisch, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mratibu wa Wadau wa Mfuko wa Pamoja wa Afya alimshukuru Rais Samia kwa kazi kubwa katika kuokoa vifo vya mama wajawazito na mtoto wakati wa kujifungua.
Mhe. Wisch aliihakikishia Serikali ya Tanzania kuendelea kuchangia katika sekta ya afya.
Aidha, walisifu juhudi zilizofikiwa katika kuimarisha huduma bora za afya katika kipindi kifupi cha Serikali chini ya Rais Samia.
Shukrani kwa Washirika wa Maendeleo
Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mchengerwa alitoa shukrani kwa Washirika wote wa Mfuko wa Pamoja wa Afya kwa ushirikiano wao thabiti. Aliitambua kwa kipekee UNICEF kama Mratibu wa Mfuko, pamoja na mchango wa Benki ya Dunia na wadau wengine wa maendeleo.
Waheshimiwa mabalozi walioshiriki kwenye mkutano huo ni pamoja na Mheshimiwa Nicole Providoli, Balozi wa Uswisi,
Mheshimiwa Nicola Brennan, Balozi wa Ireland,
Mheshimiwa Emily Burns, balozi wa Canada,
Mheshimiwa Marianne Young, balozi wa Uingereza,
Mheshimiwa Eunju Ahn, Balozi wa Korea,
Mheshimiwa Nathan Bellete, Mwakilishi wa Benki ya Dunia nchini
Mheshimiwa Mark Bryan Schreiner, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA),
Mheshimiwa Elke Wisch, Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Mratibu wa Wadau wa Mfuko wa Pamoja wa Afya.
Mhe. Mchengerwa alisisitiza kuwa mafanikio hayapimwi kwa kiasi cha fedha kilichotolewa, bali kwa maboresho yanayopimika katika afya na ustawi wa jamii.
“Tanzania iko tayari kushirikiana, tayari kuvumbua, na tayari kusonga mbele kwa njia mpya inayozingatia uwajibikaji wa pamoja na matokeo yanayopimika,” alihitimisha.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, kuimarisha mifumo ya afya si tu kuboresha huduma, bali ni kulinda jamii, kuongeza tija ya taifa, kuimarisha taasisi na kujenga mustakabali wenye afya na usalama zaidi kwa nchi.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, Katibu Mkuu, Dkt. Seif Shekhalaghe, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia eneo la Dawa, Emmanuel Tayari, Mganga Mkuu na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Maghembe.

Pembezoni mwa kikao hicho Mheshimiwa Mchengerwa alifanya balozi wa Uingereza, Canada na Marekani.
Ushirikiano baina ya Tanzania Uingereza na Canada
Mhe. Mchengerwa alifafanua kuwa Uingereza na Tanzania zina ushirikiano wa muda mrefu katika sekta ya afya, uliojengwa juu ya miongo kadhaa ya kazi ya pamoja ya kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kuimarisha mifumo ya afya, na kukabiliana na changamoto kuu za kiafya. Ushirikiano huu unahusisha misaada ya kiserikali, msaada wa kitaalamu, ushirikiano wa tafiti, pamoja na msaada kupitia taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Uingereza.
Naye Balozi wa, Uingereza Mhe. Young alisema nchi yake huchangia kwa kiasi kikubwa katika taasisi za kimataifa za afya kama Gavi, Mfuko wa Dunia (Global Fund), na Shirika la Afya Duniani (WHO) zinazofanya kazi nchini Tanzania na itaendelea kufanya hivyo
Mhe. Mchengerwa alifafanua kuwa kwa sasa, sekta ya afya inalenga maeneo yafuatayo ya kipaumbele ambayo ni pamoja na Kusaidia kuanzisha na kutekeleza mifumo ya Bima ya Afya kwa Wote ili kupunguza pengo la upatikanaji wa huduma;
Kuboresha huduma za mkoba, rufaa na huduma bingwa katika ngazi zote za utoaji huduma;
Kuimarisha huduma za uchunguzi, kinga, tiba, ukarabati na huduma za kupunguza maumivu katika ngazi zote;
Kuimarisha afya ya uzazi, mama na mtoto;
Kuimarisha kinga, udhibiti na usimamizi wa magonjwa yasiyoambukiza (NCDs);
Kuimarisha maandalizi na mwitikio wa dharura dhidi ya magonjwa ya milipuko;
Kuboresha utekelezaji wa tiba mtandao (telemedicine) na mifumo ya kielektroniki ya taarifa za afya katika ngazi zote;
Kusaidia utekelezaji wa tiba asili na mbadala nchini; na
Kuwekeza katika uzalishaji wa ndani wa chanjo, bidhaa na vifaa tiba
Kwa upande wake Balozi wa Canada nchini Mhe. Burn alisema ameridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Tanzania na ipo tayari kuendelea kuchangia katika sekta ya afya.



No comments:
Post a Comment