Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ametoa wito kwa Wizara zinahusiana na Sekta ya Mazingira, kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuwa na mpango wa pamoja utakaowezesha uhifadhi endelevu wa mazingira.
Makamu wa Rais ametoa wito huo, wakati akifanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Ashatu Kijaji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhandisi Hamad Masauni, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Festo Dugange, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Richard Muyungi pamoja na wataalamu kutoka Wizara hizo, katika kikao kilichofanyika mkoani Dodoma.Amesema Wizara hizo zinategemea zaidi uhifadhi wa Mazingira, mathalani Wizara ya Maji itafanya kazi kwa ufanisi kama vyanzo vya maji havitaaribiwa, vilevile mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia utawezesha kuokoa ukataji miti ovyo na hivyo kulinda misitu iliyopo.
Makamu wa Rais amewasihi Viongozi wa Wizara hizo, kuongeza jitihada ili kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika kulinda na kuhifadhi mazingira kwa kuwa ina misitu ya kutosha pamoja na wataalamu wenye uwezo wa kufanikisha hilo.
Amesema tayari Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua mpango wa kukijanisha nchi, pamoja na kutoa hamasa za mara kwa mara za upandaji miti, ikiwemo kutumia siku yake ya kuzaliwa kuhamasisha upandaji miti kitaifa, hivyo ni vema watendaji wote kuongeza bidii katika kuhakikisha Tanzania inakua kinara wa uhifadhi wa mazingira.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amewahimiza Viongozi hao, kuandaa mpango ambao utawezesha kukabiliana na changamoto za kuhifadhi miti baada ya kupandwa ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Makamu wa Rais, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuwa na mpango wa upandaji miti Kitaifa ambao unakwenda sambamba na Siku ya Misitu Duniani.


.jpeg)



No comments:
Post a Comment