JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


JUKWAA LA UWEZESHAJI WANAWAKE HANDENI MJI KUZINDULIWA MACHI 5

Share This
 

Na Mwandishi Wetu

KATIKA kuelekea kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Halmashauri ya Mji Handeni imejipanga kutekeleza shughuli mbalimbali ikiwamo uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Handeni, Maryam Ukwaju, amesema halmashauri hiyo inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Amesema Machi 5, 2026 kutafanyika kongamano la wanawake litakaloenda sambamba na uzinduzi wa Jukwaa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi la Halmashauri ya Mji Handeni, linalolenga kuwaunganisha wanawake ili kubadilishana uzoefu, kupata taarifa za fursa za kiuchumi na kuimarisha shughuli zao za ujasiriamali.

Ukwaju amesema kongamano hilo pia litaambatana na maonesho ya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wanawake wajasiriamali, hatua inayolenga kuonesha ubunifu wao pamoja na juhudi wanazofanya katika kujikwamua kiuchumi.

Ameongeza kuwa katika kongamano hilo litakalofanyika katika ukumbi wa CCM Wilaya ya Handeni, washiriki watapatiwa elimu mbalimbali ikiwemo masuala ya umiliki wa ardhi na mirathi, malezi na makuzi ya watoto, ujasiriamali na biashara, elimu ya ushirika na SACCOS pamoja na kilimo bora na ufugaji wa kisasa.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Machi 6, 2026 halmashauri itatoa msaada kwa baadhi ya kaya zinazoishi katika mazingira hatarishi ikiwa ni sehemu ya kuonesha mshikamano na kusaidia jamii zenye uhitaji.

Kadhalika amesema kilele cha maadhimisho hayo kwa ngazi ya Halmashauri kitafanyika Machi 7, 2026 katika viwanja vya Shule ya Msingi Kwenjugo, ambapo kutafanyika ugawaji wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike pamoja na utoaji wa vyeti kwa vikundi vinne vya wanawake vilivyotekeleza miradi yao kwa mafanikio na kurejesha mikopo ya asilimia 10 kwa wakati. Amesema mgeni rasmi katika shughuli hizo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese.

Ukwaju amesema maadhimisho hayo yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana; Msingi Jumuishi kufikia Dira 2050,” huku halmashauri ikiendelea kuhamasisha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kuimarisha usawa wa kijinsia na kuchochea maendeleo jumuishi kwa wanawake na wasichana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad