JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


ALLIANCE ONE YAONGOZA MAPAMBANO YA KUREJESHA MISITU NZEGA

Share This

Na Mwandishi Wetu,Nzega

Halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora imeipongeza Kampuni ya Tumbaku ya Alliance One kwa kuwa kinara wa juhudi za upandaji miti ili kurejesha misitu iliyoharibiwa kutokana na shughuli za kibianadamu wilayani humo.

Akiongea katika hafla ya upandaji miti iliyoadaliwa na Kampuni hiyo katika shule ya msingi Ngukumo na Ikiniziwa, Mwakilishi wa Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega Farida Hamis amesema mchango wa Alliance One ni muhimu katika kufanikisha maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan yanayoitaka kila Halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.

Bi. Hamis amesema kuwa Wilaya ya Nzega imekuwa miongoni mwa maeneo yaliyoathirika kwa kiasi kikubwa na uharibifu wa misitu kutokana na shughuli za kibinadamu, hususan ukataji miti kwa ajili ya kuni, uchomaji mkaa pamoja na shughuli za ukaushaji wa tumbaku.


Amesema juhudi za Kampuni ya Alliance One zimekuja wakati muafaka katika kurejesha uoto wa asili na kulinda mazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Ameeleza kuwa ushirikiano kati ya Halmashauri na Kampuni hiyo umeongeza kasi ya upandaji miti pamoja na utoaji wa miche katika maeneo mbalimbali, hususan mashuleni, hatua inayosaidia kujenga msingi wa mabadiliko ya tabia kwa jamii kuanzia kwa wanafunzi.

“Kupitia wanafunzi hawa, tunajenga kizazi chenye uelewa wa thamani ya mazingira, ambacho kitaendelea kutunza miti hii hadi ikue na kutoa manufaa,” amesema.

Kwa upande wake, Mratibu wa masuala ya miti kutoka Kampuni ya Alliance One, Rashid Salum, amesema kampeni ya upandaji miti ilianza mwaka 2023 ikiwa na lengo la kurejesha misitu iliyoharibiwa na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa kuni hususan katika sekta ya tumbaku.

Amesema kuwa hadi sasa, kampuni hiyo imefanikiwa kupanda miti katika eneo la hekta 818 wilayani Nzega, huku pia wakipanua juhudi hizo katika Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma ambapo zaidi ya hekta 800 zimepandwa miti.

Ameongeza kuwa wanashirikiana kwa karibu na Halmashauri pamoja na wananchi wa maeneo husika, ambapo baadhi yao hupata ajira za muda kupitia shughuli za upandaji na utunzaji wa miti.

Salum amesisitiza kuwa moja ya mikakati yao mikubwa ni kuhakikisha miti inayopandwa inalindwa na kukua, ndiyo maana wameanza kuhusisha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili kujenga tabia ya kuitunza.

“Kwa leo hii tumepanda miche 300 katika Shule ya Msingi Ngukumo na miche 200 katika Shule ya Sekondari Ikiniziwa. Wanafunzi wenyewe kwa kushirikiana na walimu wao wameipanda, jambo linalowajengea uwajibikaji wa kuitunza hadi ikue,” amesema.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo ni endelevu katika maeneo yote yanayozalisha tumbaku, ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na rasilimali ya kuni ya uhakika bila kuendelea kuharibu misitu ya asili. Pia ametoa wito kwa wananchi kuendelea kupanda miti katika maeneo yao binafsi ili kuongeza juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Kwa upande wao, wanafunzi wa Shule ya Msingi Ngukumo, Sada Maganga na Baraka Amoni, wameishukuru Kampuni ya Alliance One kwa kuwapatia miche ya miti na kuwashirikisha moja kwa moja katika zoezi la upandaji.

Wamesema kuwa wamejifunza umuhimu wa miti katika kuhifadhi mazingira na wameahidi kuitunza miti waliyoipanda ili iweze kukua na kuleta faida kwa shule yao na jamii kwa ujumla. “Tutailinda miti hii kwa sababu tumejua umuhimu wake. Itatupatia kivuli, hewa safi na hata kuni hapo baadaye,” wamesema kwa pamoja.

Hatua hiyo inaonekana kuwa mwanzo wa mabadiliko chanya ya kimazingira wilayani Nzega, huku ushirikiano kati ya sekta binafsi, Serikali na jamii ukiendelea kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha uhifadhi endelevu wa misitu.

Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Nzega Bi Farida Hamis akipanda moja ya miti katika shule ya msingi Ngukumo wilayani Nzega, miti ambayo imetolewa na kampuni ya Tumbaku Alliance One kwa ajili kuchangia zoezi upandaji miti milioni 1.5 wilayani humo sambamba na agizo la serikali.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Ngukumo wilayani Nzega,Bw Edmund Sinkonda, akipanda moja ya miti iliyotolewa na kampuni ya Tumbaku Alliance One kwa ajili kuchangia zoezi upandaji miti milioni 1.5 wilayani humo sambamba na agizo la serikali.
Batuli Hemedi Mtendaji wa Kijiji cha Ngukumo wilayani Nzega akipanda moja ya miti iliyotolewa na kampuni ya Tumbaku Alliance One kwa ajili kuchangia zoezi upandaji miti milioni 1.5 wilayani humo sambamba na agizo la serikali.
Mwanafunzi wa Darasa la Sita katika shule ya Msingi Ngukumo wilayani Nzega, Lucia Fidelis, akipanda mmoja ya miti shuleni hapo miti iliyotolewa na kampuni ya Tumbaku Alliance One kwa ajili kuchangia zoezi la upandaji miti milioni 1.5 wilayani humo sambamba na agizo la serikali.

Baraka Amon, Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Ngukumo wilayani Nzega, akipanda moja ya miti iliyotolewa na kampuni ya Tumbaku Alliance One kwa ajili kuchangia zoezi upandaji miti milioni 1.5 wilayani humo sambamba na agizo la serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad