JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


ADEM YAHITIMISHA MAFUNZO KWA MAAFISA ELIMU WA MIKOA 26 TANZANIA BARA

Share This
Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu - ADEM umeendesha mafunzo maalumu ya siku tano kwa Maafisa Elimu wa Mikoa 26 kutoka Tanzania Bara kuanzia tarehe 8-12 Machi, 2026 jijini Arusha.

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo viongozi hao wa kuimarisha uongozi na usimamizi wa sekta ya elimu katika maeneo mbalimbali ikiwemo uandaaji wa Mpango Mkakati wa elimu katika ngazi ya mkoa, utafutaji na usimamizi wa rasilimali katika elimu, utambuzi na usimamizi wa changamoto za afya ya akili kwa watumishi wa kada ya elimu, mbinu bora za kushughulikia malalamiko, kufanya ufunzaji na uatamizi, na kuimarisha usimamizi saidizi katika sekta ya elimu.

Akifunga mafunzo hayo, Kamishna wa Elimu nchini, Dkt. Lyabwene M. Mtahabwa, amesisitiza umuhimu kwa viongozi wote wa elimu kuanzia ngazi ya kitaifa hadi shule kuweka mbele haki za watoto katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema kuwa watoto ndio msingi wa uwepo wa nafasi za uongozi katika sekta ya elimu, hivyo viongozi wanapaswa kuhakikisha wanawalinda na kuwapatia mazingira bora ya kujifunzia.

Aidha, Dkt. Mtahabwa amewataka Maafisa Elimu wa Mikoa kuacha mtindo wa uongozi unaolenga kutafuta makosa kwa nia ya kuwaadhibu wanaowaongoza na badala yake, amewahimiza kutumia mbinu za kutoa msaada wa kitaaluma na kitaalamu kwa watumishi wa elimu, kama walivyojifunza wakati wa mafunzo hayo.

“Ni muhimu viongozi wa elimu kuwa washauri na wawezeshaji kwa wale wanaowaongoza, badala ya kuwa wakaguzi wanaotafuta makosa,” Amesisitiza Dkt. Mutahabwa

Kamishna wa elimu pia, amesisitiza kuwa Serikali pamoja na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia taasisi zake ikiwemo ADEM, imejipanga kuhakikisha mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora katika mazingira salama.

Amesema ili kufikia lengo hilo, kila kiongozi wa elimu anapaswa kusimamia kikamilifu majukumu yake katika eneo analoliongoza.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali kuendelea kuimarisha uwezo wa viongozi wa elimu ili kuboresha utoaji wa elimu nchini.

Jumla ya Maafisa Elimu wa Mikoa 26 kutoka katika Mikoa yote ya Tanzania Bara wameshiriki mafunzo hayo yaliyoendeshwa na ADEM kwa ufadhili wa mradi wa Shule Bora.












No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad