JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


ADEM, TET KUSHIRIKIANA KUINUA VIWANGO VYA MAFUNZO YA WALIMU

Share This
WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu nchini (ADEM) kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) wamefanya warsha maalumu ya kuhakiki Matini ya uendeshaji wa Jumuiya za Kujifunza za walimu na viongozi wa elimu (JzK), ikiwa ni hatua muhimu ya kukusanya maoni ya wadau kwa ajili ya kuboresha nyenzo hiyo.

Warsha hiyo imelenga kuhakikisha matini inayotarajiwa kutumika kuzijengea uwezo Jumuiya za Kujifunza inakuwa bora, shirikishi na yenye kukidhi mahitaji halisi ya walimu na viongozi wa elimu nchini.

Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania, Dkt. Aneth Komba, amesisitiza umuhimu wa taasisi hizo mbili kuweka mpango madhubuti wa utekelezaji wa matumizi sahihi ya matini hizo ili kufanikisha lengo la kuimarisha Jumuiya za Kujifunza.

Ameeleza kuwa maandalizi ya matini hiyo ni jukumu muhimu la kitaifa, hivyo wadau walioshiriki wanapaswa kutoa maoni na ushauri wa kitaalamu utakaosaidia kuboresha nyenzo hiyo na kuhakikisha inaleta matokeo chanya yaliyokusudiwa.

“Niwapongeze sana mliochaguliwa kuandaa matini hii, nina imani mmeitekeleza kazi hii kwa weledi na ufanisi mkubwa. Ni muhimu pia kwa wadau wote kushiriki kikamilifu katika uhakiki huu ili kupata matini bora itakayosaidia kufikia malengo yaliyowekwa,” amesema Dkt. Komba.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, amewashukuru wataalamu na wadau wote waliohusika katika uandaaji wa matini hiyo kwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na kwa viwango vinavyohitajika.

Amesema matini hiyo itakuwa mwongozo muhimu wa utekelezaji wa shughuli za Jumuiya za Kujifunza nchini, sambamba na kusaidia kufikia azma ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya kuboresha mafunzo ya walimu na viongozi wa elimu kazini.

Aidha, amewahimiza wadau walioshiriki warsha hiyo kuendelea kutoa mchango wao kwa weledi ili kuhakikisha matini hiyo inakuwa na ubora unaokusudiwa.

Warsha hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wataalamu kutoka programu ya Shule Bora, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Taasisi ya Elimu Tanzania, pamoja na viongozi wa idara za elimu kutoka Halmashauri ya Mji Bagamoyo na Manispaa ya Singida. Wadau wengine walioshiriki ni pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za CAMFED na Project Zawadi.

















No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad