
SHAHIDI wa tisa katika kesi hiyo, Ofisa wa Jeshi la Polisi ASP Geofrey Lutufye (47), ameieleza Mahakama kuwa vijana wawili waliokamatwa walikiri kushawishika na maneno ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, na kuamua kuunga mkono wito wa kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Renatus Mkude, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akishirikiana na Jaji James Karayamaha na Jaji Ferdinand Kiwonde, shahidi huyo alieleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa katika kijiwe cha bajaji eneo la Mrombo, Arusha.
ASP Lutufye alidai kuwa Aprili 3, 2025, akiwa kwenye doria na kikosi chake chenye askari tisa wakitumia gari la polisi aina ya Toyota Land Cruiser, alipokea maelekezo kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Upelelezi, ASP Bonny Mgogo, kwenda eneo hilo kufuatilia taarifa za vijana wanaopanga kuzuia uchaguzi.
“Nilipofika eneo la Mrombo nilikuta vijana wakila njama za kuzuia uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” alidai.
Alisema waliwakamata vijana wawili waliotajwa mahakamani kama P4 na P7 na kuwapeleka Kituo cha Polisi Murieti mkoani Arusha kwa hatua zaidi.
ASP Lutufye alieleza kuwa wakiwa njiani aliwahoji watuhumiwa hao kuhusu tuhuma hizo.
“Niliwauliza kwa nini wanahusika kula njama za kuzuia uchaguzi mkuu wa 2025. Wote walikiri kuwa wanamuunga mkono Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, kutokana na kauli aliyoitoa mtandaoni kwamba atazuia uchaguzi, ataleta uchochezi na atakinukisha,” alidai shahidi huyo.
Mahakamani hapo, alieleza kuwa aliagizwa kuwapeleka watuhumiwa hao katika Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa na baadaye kuanzisha jalada la uchunguzi lenye namba ARS/D/CID/B/40/2025.
Aidha, alidai kuwa alipokea maelekezo ya kuwahoji zaidi watuhumiwa hao, maelekezo ambayo aliyatekeleza kwa kushirikiana na askari wengine, huku yeye akiandika maelezo yake ya ushahidi Aprili 18, 2025.
Kabla ya kueleza tukio hilo, ASP Lutufye aliitambulisha Mahakama kuhusu taaluma na uzoefu wake, akisema alihitimu mafunzo ya awali ya polisi katika Chuo cha Polisi Moshi Aprili 28, 2003 na kumaliza Novemba mwaka huo. Pia alipata mafunzo ya nyota ya kwanza mwaka 2013 katika chuo hicho, na baadaye mafunzo ya cheo cha Mrakibu Msaidizi wa Polisi katika Chuo cha Polisi Dar es Salaam (Police Academy), aliyohitimu Novemba 2023.
Alisema ana uzoefu wa miaka 15 katika majukumu ya upelelezi, akianzia Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam kama askari wa kawaida (general duty), kabla ya kuhamishiwa Ofisi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Geita na baadaye Mkoa wa Arusha, ambako kwa sasa ni kiongozi wa kikosi cha Anti Robbery.
Shahidi huyo alieleza kuwa majukumu yake ni pamoja na kufanya doria, kukamata watuhumiwa, kufanya upelelezi na kuwafikisha mahakamani.... Kesi inaendela


No comments:
Post a Comment