JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Tanzania Yajenga Uchumi wa Ubunifu Kupitia Teknolojia ya Anwani za Makazi

Share This

 

SERIKALI imezidisha kasi ya kujenga uchumi wa kidijitali kwa kusisitiza matumizi mapana ya mfumo wa anwani za makazi, hatua inayolenga kurahisisha utoaji wa huduma, kuimarisha utambuzi wa wananchi na kuongeza ufanisi wa shughuli za kiuchumi nchini. Wito huo umetolewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki, akizihimiza wizara na taasisi zote za umma kuutumia kikamilifu mfumo huo kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya kisasa.

Akizungumza jijini Dar Es Salaam leo Januari 08, 2026 katika kilele cha Wiki ya Anwani za Makazi na Maonyesho ya Teknolojia ya Posta jijini Dar es Salaam, Kairuki ameeleza kuwa mfumo huo ni mhimili wa kutambua makazi ya wananchi, kurahisisha huduma za kijamii na kiuchumi pamoja na kuboresha ukusanyaji wa mapato ya serikali. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wakiwemo Hassan Juma, Anne Semamba Makinda na Profesa Joyce Mzalishako.

Waziri Kairuki amebainisha kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na mifumo ya kidijitali ili kuiwezesha Tanzania kufikia uchumi unaotegemea ubunifu, teknolojia na maarifa. Alisema hadi sasa anwani za makazi takribani milioni 12.9 zimeshasajiliwa, huku mifumo 29 kutoka taasisi 23 za umma na binafsi ikiunganishwa ili kuboresha utoaji wa huduma.

Ameeleza kuwa manufaa ya mfumo huo yameonekana katika sekta za elimu, fedha, usalama, biashara mtandao na huduma za dharura, ambapo taasisi kama Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na Jeshi la Zimamoto zimeongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao. Pia mfumo umeisaidia serikali kufikisha misaada kwa haraka wakati wa majanga kwa kutambua kaya zilizoathirika.

Kwa upande wa ushiriki wa sekta binafsi, Kairuki amezihimiza benki, kampuni za mawasiliano na taasisi za fedha kuutumia mfumo wa anwani za makazi katika utambuzi wa wateja, hatua itakayorahisisha huduma za kifedha na kuongeza ujumuishi wa wananchi katika uchumi rasmi. Sambamba na hilo, wizara ilikabidhi zaidi ya vishikwambi 5,000 kwa watendaji wa mitaa, kata na vijiji ili kuharakisha uingizaji na usasishaji wa taarifa za makazi.

Aidha, ameipongeza TAMISEMI, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar na Wizara ya Ardhi kwa ushirikiano uliofanikisha utekelezaji wa mradi huo kwa muda mfupi. Amesisitiza kuwa Wiki ya Anwani za Makazi itaadhimishwa kila Februari 8 kama jukwaa la tathmini, ubadilishanaji uzoefu na uhamasishaji wa matumizi ya teknolojia katika huduma za posta na mawasiliano.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Hamisa Abdullah, amesema mfumo wa anwani za makazi ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuimarisha utambuzi wa makazi na kurahisisha huduma za serikali na sekta binafsi. Aliongeza kuwa mfumo huo uliobuniwa na wataalamu wa ndani unapatikana kupitia tovuti na programu ya simu ya NAPA, huku idadi ya watumiaji ikiongezeka kwa zaidi ya asilimia 70 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hassan Juma, amesisitiza dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza ushirikiano katika utekelezaji wa mfumo huo Unguja na Pemba. Alisema licha ya changamoto za awali za uelewa mdogo, elimu kwa umma na ushiriki wa viongozi wa mitaa umeongeza matumizi ya huduma za kidijitali, zikiwemo mikopo ya elimu, huduma za benki na utambuzi sahihi wa makazi.








No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad