Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wamepitisha kiasi cha 45,136,269,016.60 kwa ajili ya rasimu wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.
Afisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Happy Masatu akisoma mpango huo wa makisio ya bajeti leo amesema umelenga kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya elimu, afya, maendeleo ya jamii, kilimo na mifugo.
Amesema mpango huo wa rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/2027 umeandaliwa kwa kuzingatia sheria, sera, mikakati ya halmashauri na miongozo ya kiserikali.
"Mpango umelenga muongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka 2026/2027, hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan akifungua Bunge la 13, ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi (CCM) na vipaumbele vya halmashauri," amesema Masatu.
Amesema mapato ya ndani ya halmashauri hiyo yameongezeka maeneo ya ushuru wa mchanga, mazao ya biashara na chakula, minada, masoko, stand ya magari, kodi ya huduma, ushuru wa trekta na uuzaji wa viwanja.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Kaleiya Melita Mollel ameeleza kwamba madiwani washirikiane na watumishi wa halmashauri katika kuteketeza miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Watu kule kwenye kata zetu wanamatarajio makubwa katika kupata huduma za umuhimu kupitia bajeti ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na mengineyo," amesema Mollel.
Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Dominika Ngaleka amewashukuru madiwani hao kwa kupitisha mpango huo wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.
"Tunatarajia watumishi wa halmashauri watashirikiana na madiwani wetu ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/2027 unatekelezeka ipasavyo," amesema Ngaleka.
Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Simanjiro Tumaini Sebastian, ameeleza kwamba ofisi ya DC inaelekeza suala la changamoto ya madawati, viti na meza katika shule za msingi na sekondari zipewe kipaumbele kwenye bajeti hiyo.
Katibu wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro Wambura Igembya amewapongeza madiwani hao kwa kupitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/2027.
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Dkt Frank Oleleshwa akitoa salamu za Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, amwelezea kwamba Bajeti ya 2026/2027 ilenge pia katika utatuzi wa migogoro ya ardhi.
Diwani wa Kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga Mardadi amesema anatarajia mwaka huu wa bajeti changamoto mbalimbali ikiwemo ukarabati wa barabara na vyumba vya madarasa na vitapatiwa ufumbuzi.
Diwani wa Kata ya Komolo, Saning'o Somi amesema mpango wa bajeti hiyo ni mzuri kwani utachangia maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo.



No comments:
Post a Comment