MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka, amesema vijana wengi wanashindwa kufanikiwa katika kujiajiri si kwa kukosa taaluma, bali kwa kukosa maarifa mapana ya uendeshaji wa biashara.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Februari 20, 2026, Mtumba jijini Dodoma, Prof. Sedoyeka alieleza kuwa pamoja na vijana wengi kuwa na ubunifu na ujuzi katika fani mbalimbali kama teknolojia na utoaji huduma, changamoto huanza wanapokutana na masuala ya fedha na usimamizi.
Alifafanua kuwa ukosefu wa uelewa wa upangaji wa bajeti, usimamizi wa mapato na matumizi, pamoja na mbinu za kuongoza rasilimali watu, umekuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji na uimara wa biashara za vijana.
“Wapo vijana wenye mawazo mazuri na bidhaa zenye ubora, lakini wanaposhindwa kusimamia fedha na mifumo ya kiutawala, biashara zao hushindwa kudumu,” alisisitiza.
Kwa mujibu wake, biashara nyingi huanzishwa kwa ari na matumaini makubwa, lakini hukosa misingi imara ya kiutawala na kifedha inayoweza kuziwezesha kukua na kushindana sokoni.
Akizungumzia suluhisho, Prof. Sedoyeka alisema IAA imeandaa mkakati wa kitaaluma kupitia programu ya “Degree 360”, unaolenga kuwajengea wanafunzi uelewa jumuishi unaohusisha masuala ya fedha, uongozi, usimamizi wa rasilimali watu na mikakati ya biashara.
Alisema lengo la programu hiyo ni kuwaandaa vijana kuwa na uwezo wa kuanzisha na kuendesha miradi au taasisi kwa ufanisi na uendelevu.
Aidha, aliwahimiza vijana kutambua kuwa mafanikio katika kujiajiri yanahitaji zaidi ya kipaji au taaluma pekee; yanahitaji nidhamu ya kifedha, uongozi bora na maarifa sahihi ya biashara.






No comments:
Post a Comment