Na Mwandishi Wetu, WMTH – Mtumba, Dodoma
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb.), amewatak Watumishi wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuimarisha ushirikiano kati ya wafanyakazi na Menejimenti ili kuhakikisha haki, motisha na tija vinatimizwa.
Amebainisha hayo tarehe 24 Februari, 2026 wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Kwanza la Wafanyakazi wa Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/2026 lililofanyika jijini Dodoma. Aliongeza kuwa Baraza la Wafanyakazi ni kiungo muhimu kati ya Menejimenti na watumishi, likiwa na jukumu la kutoa ushauri kuhusu utendaji, kusimamia maslahi ya wafanyakazi, na kupitisha mipango ya mapato na matumizi ya Wizara.
Alisisitiza kuwa “hakuna haki bila wajibu,” na kwamba wafanyakazi wanapaswa kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha Wizara inatoa huduma bora kwa wananchi. Aidha, Naibu Waziri Mkama alitoa pongezi kwa watumishi wa wizara kwa bidii yao mwaka jana na kuhimiza motisha na mafunzo yanayolenga kuboresha ufanisi kazini.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, alieleza kuwa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi ni utekelezaji wa Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Waraka Na. 1 wa Mwaka 1970 linalolenga kuanzisha mabaraza ya wafanyakazi katika taasisi za umma ili kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi mahala pa kazi, pamoja na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utawala bora.
Bw. Abdulla pia alieleza mafanikio ya Wizara katika Mwaka wa Fedha 2025/2026, ikiwemo: kukamilika kwa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano kama ilivyopangwa; utekelezaji wa Mradi wa Minara 636 ya Mawasiliano Vijijini kufikia asilimia 71 ifikapo Desemba 2025; kuongezeka kwa uwezo wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutoka 200 Gbps hadi 2,000 Gbps kwenye njia kuu, pamoja na kuimarishwa kwa maunganisho ya mipakani; na mtandao kuongezeka hadi kufikia kilometa 15,066 na kuunganisha wilaya 119 kati ya 139 zilizopangwa.
Aidha, Bw. Abdulla alibainisha miradi mingine inayoendelea kutekelezwa ikiwemo uratibu wa Mradi wa Satelaiti Ndogo ya Mafunzo (KIBOCUBE), maandalizi ya ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Dodoma na Zanzibar, utekelezaji wa Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali 2024–2034, ujenzi wa Chuo Mahiri cha TEHAMA (DTI) katika eneo la Nala, pamoja na uandaaji wa nyaraka za kitaifa za usimamizi wa TEHAMA.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Baraza la Wafanyakazi Taifa kwa Mkoa wa Dodoma, Bw. Maulid Kipeneku, aliwafikishia wajumbe salamu za Baraza na kuwashukuru wafanyakazi kwa ushirikiano wao, akisisitiza umuhimu wa kushirikiana na viongozi wa Wizara katika kuleta maendeleo endelevu ya sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari nchini.
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment