JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


MIRIAM ODEMBA FOUNDATION YAMSHEREHESHA MIRIAM ODEMBA NA WATOTO WENYE MAHITAJI JESHI LA WOKOVU

Share This

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANAMITINDO maarufu wa kimataifa, Miriam Odemba, ameungana na watoto wa Shule ya Msingi ya Jeshi la Wokovu inayohudumia watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum jijini Dar es Salaam kusherehekea siku yake ya kuzaliwa, hatua iliyobeba ujumbe wa upendo na uwajibikaji kwa jamii.

Tukio hilo liliambatana na hafla fupi iliolenga kuinua misaada kwa kituo hicho kinachohudumia wanafunzi walio katika mahitaji maalum na ulemavu.

Odemba ametimiza umri wa miaka 44, Alianza safari yake ya uanamitindo akiwa na umri wa miaka 14 tu na tangu wakati huo amekuwa mfano wa kuigwa kwa wengi ndani na nje ya Tanzania, akilitangaza taifa kupitia mafanikio yake katika majukwaa ya kimataifa.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Rahma Omary alimshukuru Miriam Odemba kwa kuwakumbuka na kusherehekea nao siku hiyo muhimu, akisema kitendo hicho kimewaletea furaha na kuwapa matumaini mapya.

Naye, Miriam Odemba akiwa mbashara kutoka Paris, amezungumza na kufuatilia tukio zima kwa njia ya mtandao, na kusema kuwa ameguswa na furaha ya watoto hao na kuahidi kuwa atakaporejea nchini atakutana nao tena ana kwa ana pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali.

“Napenda sana watoto, na ndiyo maana natumia muda wa kutosha kuwa na mtoto yeyote yule ninayekuwa naye karibu. Watoto wa kituo hiki wanastahili upendo mwingi zaidi kutokana na changamoto wanazopitia. Sherehe hii ndogo si anasa kwao, bali ni jambo wanalolitamani, kusherehekea siku ya kuzaliwa na dada yao mkubwa. Namshukuru Mungu kwa kunitumia kuwa sehemu ya furaha ya watoto wa shule hii,” alisema Miriam Odemba.

Miriam anaamini kuwa ulemavu si kikwazo cha kufikia ndoto na malengo ya maisha, akibainisha kuwa watoto hao wana uwezo mkubwa wa kufanya mambo yatakayoshangaza dunia iwapo watapatiwa mazingira rafiki na msaada stahiki.

Kutokana na mchango wake endelevu kwa shule hiyo, uongozi umemtunuku tuzo maalumu ya kutambua juhudi zake za kusaidia jamii.

Kaimu Mkuu wa Shule hiyo ya Matumaini, alisema kuwa Odemba amekuwa akiitembelea shule hiyo mara kwa mara na kutoa misaada mbalimbali.

Miriam Odemba Foundation imesimamia utaratibu wote wa kukusanya, kusimamia na kukabidhi, mahitaji mbalimbali yaliyotolewa na Marafiki, jamaa na wadau walio kwenye kampeni ya Saidia na Odemba, na kufanikisha kutolewa kwa sukari, unga, mchele, maharage, sabuni, nepi na mahitaji mengine muhimu kwa wanafunzi.

Marafiki, wadau na wageni waliohudhuria walikuwakilisha kwa pamoja Miriam Odemba kwa kukata keki na kushiriki chakula cha jioni pamoja na watoto hao, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano huo.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Bi. Jennifer Fred Mteleke, alisema kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa kurejesha kwa jamii na kuimarisha ustawi wa watoto wenye mahitaji maalumu.

Alibainisha kuwa taasisi inatarajia kuanzisha mradi wa pamoja na kituo hicho cha Jeshi la Wokovu utakaolenga kuongeza kiwango cha misaada na kuboresha maisha ya masomo kwa wanafunzi hao.

“Tuna mipango endelevu ya kuhakikisha watoto wanapatiwa misaada ya mahitaji yao yote. Kila hitaji la mtoto ni muhimu. Watoto wanalelewa vizuri, wanafanya pia vizuri sana, wanastahili kupata mahitaji yote muhimu. Tunaamini hili linawezekana kwa msaada wa wadau wote wanaoendelea kujumuika nasi, Watanzania kwa ujumla, asasi mbalimbali pamoja na Serikali,” alisema Mkurugenzi huyo.

Matroni wa shule hiyo, Capt. Consolata Magesa, alisema sherehe hiyo imekuwa baraka kubwa kwa wanafunzi na kupongeza msaada unaotolewa na Odemba na taasisi yake. Hata hivyo, alieleza kuwa shule inaendelea kukabiliwa na changamoto ya uhaba wa mahitaji ya msingi na kutoa wito kwa wadau kujitokeza kusaidia.

Mama mzazi wa Odemba, Magreth John, alimshukuru Mungu kwa binti yake kutimiza miaka 44 na kueleza faraja yake kuona anatumia mafanikio yake kuwajali watoto wenye mahitaji maalumu.

Maadhimisho hayo yameacha ujumbe mzito kwa jamii kuhusu umuhimu wa upendo, mshikamano na kuwajali watu wenye mahitaji maalumu, huku Odemba akiendelea kuwa mfano wa kutumia umaarufu wake na Taasisi kuleta mabadiliko chanya katika jamii.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad