JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


Kili Trust Yaandaa Warsha ya Kuwajengea Uwezo Wanufaika Wake

Share This

 

Kwa uongozi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita, Dkt. Omar Sukari ( pichani), wadau (ikiwemo GGML, TACAIDS, LGAs, na washirika wengine)  wanaratibu mbinu zitakazokuwa za kijamii, endelevu na zenye matokeo yanayopimika.
Majadiliano ya kimkakati yakiendelea ili kubuni afua mahsusi zitakazowafikia wachimbaji wadogo katika Mkoa wa Geita, kundi lenye changamoto na hatari za kipekee katika mapambano dhidi ya VVU.







*Ili.Kuimarisha Uwajibikaji na Uhakiki wa Kina

Na Mwandishi Wetu
GEITA Gold Mining Limited kupitia mpango wake wa Kilimanjaro Challenge Against HIV and AIDS Trust (Kili Trust) imeandaa warsha ya kuwajengea uwezo wanufaika wake, inayofanyika jijini Mwanza kuanzia Februari 16–20, 2026. Warsha hiyo inawakutanisha wanufaika, wadau wa utekelezaji, washirika na wadhamini kwa lengo la kuimarisha utawala bora, uwajibikaji wa kifedha na kuongeza matokeo chanya ya programu.

Warsha hii ni hatua muhimu ya kiutawala kabla ya utoaji wa fedha kupitia Kili Grants Portfolio ya mwaka 2024/2025, inayolenga kusaidia miradi ya uwezeshaji wa kiuchumi, uimarishaji wa afya za jamii na mipango endelevu. Kupitia mpango huo, jumla ya watu 2,309 wananufaika moja kwa moja na 19,690 kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika mikoa sita ya Tanzania.

Kama sehemu ya kuimarisha mfumo wa utawala na uwajibikaji, Kili Trust inazitaka taasisi zote zitakazonufaika kupitia mchakato wa uhakiki wa kina (due diligence), mafunzo elekezi kabla ya kuanza utekelezaji wa miradi, mafunzo ya usimamizi wa ruzuku, usimamizi wa fedha pamoja na ufuatiliaji na tathmini kabla ya kupokea fedha. Hatua hizi zinalenga kuhakikisha fedha zinatumika kwa uwazi, ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyokusudiwa.

Kili Challenge ilianzishwa mwaka 2002 na Geita Gold Mining Limited na imekua kuwa miongoni mwa mipango mikubwa ya sekta binafsi nchini Tanzania katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) ili kuimarisha usimamizi na mwafaka wa kitaalamu.

Akizungumza katika warsha hiyo, Meneja wa Kili Trust, Bw. Stephen Mhando, amesema Kili Challenge ya kila mwaka si tukio la kuchangisha fedha pekee, bali ni wito wa kitaifa wa kuchukua hatua unaowaunganisha washirika, jamii na watu binafsi kusimama pamoja na watu wanaoishi na VVU na UKIMWI. Amesema kupitia rasilimali zinazokusanywa kila mwaka, Trust inaendelea kupanua afua zenye kuleta mabadiliko chanya kwa kuwezesha kiuchumi, kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na kupunguza unyanyapaa, ili kuhakikisha matokeo endelevu katika jamii zinazonufaika.

Mwaka huu, programu imepanua wigo kwa kuwajumuisha wachimbaji wadogo kama kundi lenye hatari zaidi ya maambukizi ya VVU kutokana na uhamahama, mazingira yasiyo rasmi ya kazi na upatikanaji mdogo wa huduma za afya. Afua maalum zitalenga kuongeza uelewa, kuimarisha kinga, upimaji, uunganishaji wa matibabu pamoja na kujenga ustahimilivu wa jamii katika maeneo ya uchimbaji.

Kili Challenge inaendelea kufadhili afua mbalimbali zikiwemo uwezeshaji wa kiuchumi kwa watu wanaoishi na VVU, mipango ya usalama wa chakula, huduma za kinga na matibabu zinazotolewa katika jamii, kupunguza unyanyapaa na kutoa msaada wa kisaikolojia, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya na mitandao ya rufaa. Kwa kuimarisha uzingatiaji wa masharti, uwazi na matokeo yanayopimika, Trust inalinda imani ya wafadhili na kuhakikisha kila shilingi inayokusanywa inaleta matokeo halisi kwa jamii.

Wakati maandalizi ya Kili Challenge 2026 yakishika kasi, Trust inazihimiza kampuni, taasisi na watu binafsi kushiriki katika kampeni ya mwaka huu ya uchangishaji fedha kwa lengo la kuchangisha Dola za Kimarekani milioni 1 mwaka 2026, ili kuendeleza azma ya Tanzania na UNAIDS ya kutokomeza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad