JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


JAFO ASISITIZA UKAMILISHAJI WA DARAJA KITOMONDO KUCHOCHEA MAENDELEO KISARAWE

Share This

Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Jimbo la Kisarawe mkoani Pwani, Dkt. Selemani Jafo, ametangaza mpango wa kuweka kambi maalum katika eneo la ujenzi wa Daraja la Kitomondo lililopo katika barabara ya Mzenga–Gwata, akilenga kuharakisha ukamilishaji wa mradi huo na kuondoa adha wanazokumbana nazo wananchi hasa nyakati za mvua.

Dkt. Jafo alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kata za Mzenga na Mafizi ndani ya Jimbo la Kisarawe, ambapo alikagua maendeleo ya mradi huo na kusikiliza changamoto za wananchi wanaotegemea daraja hilo kwa shughuli za kila siku.

Daraja la Kitomondo linajengwa na kampuni ya Neloyt Tanzania Limited kwa gharama ya shilingi milioni 359.67 chini ya usimamizi wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), hata hivyo ujenzi wake umechelewa kukamilika hali inayosababisha usumbufu mkubwa kwa wakazi wa Mzenga na Mafizi.

Mbunge huyo amesema daraja hilo ni kiungo muhimu kwa wakazi wa kata hizo na vijiji vya Mafizi, Nyani, Gwata na Ving’andi, akieleza kuwa kuchelewa kwake kumeathiri shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo usafiri wa wanafunzi, wagonjwa na wafanyabiashara.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa daraja hilo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao na bidhaa, hivyo kuchochea maendeleo katika Jimbo la Kisarawe.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Kisarawe, Eng. Africano Orota, amemhakikishia Dkt. Jafo kuwa wataongeza usimamizi na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad