
KAMPUNI ya Uchimbaji wa Madini ya Dhahabu ya Geita (GGML) imetambulisha tamasha la michezo kwa watumishi litakalofanyika kila baada ya miezi mitatu ili kuimarisha utendaji na mahusiano kazini.
Kaimu Mkurugenzi wa Raslimali Watu GGML, Dominick Marandu alitoa taarifa hiyo juzi katika uzinduzi wa tamasha kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya wasichana Nyankumbu Geita.
Alisema tamasha hilo litafahamika kwa jina la Geita Sports Club Bonanza linalenga kuwawezesha watumishi kupata nafasi ya kujumuika, kufurahi na kufanya mazoezi ya afya mwili na akili.
“Tunafahamu michezo ni afya, lengo si kushindana bali ni kuimarisha afya na mahusiano hivo ni jambo ambalo tumelianza sasa na litakuwa endelevu kila baada ya miezi mitatu” alisema.
Alisema, dhamira ni kuwaleta pamoja wadau, wafanyakazi, wakandarasi na kujenga mahusiano baina ya GGML, taaasisi na kampuni tofauti kutoka ndani na nje ya Manispaa ya Geita.
Mwenyekiti wa GGML Sports Club, Valence Ibrahimu alisema Geita Sports Club Bonanza imekuja ikiwa ni maazimio ya wafanyakazi na viongozi matarajio ikiwa ni kuleta matokeo chanya kazini.
Alisema bonanza hilo la michezo litafanyika mara nne kwa mwaka ili kuimarisha mahusiano mahala pa kazi pamoja na afya ya mwili na akili kwa watumishi wa Idara tofauti ndani ya GGML.
“Kila robo mwaka tutakuwa tunafanya mara moja, kwa kuanza tumeshirikisha watumishi kutoka wakandarasi wa kampuni tofauti zilizopo GGML na wengine kutoka Manispaa ya Geita”, alisema
Katibu Msaidizi wa GGML Sports Club, Irene Mfwele alisema tamasha limezinduliwa kwa michezo tofauti ikiwemo mbio ndefu na mbio fupi, mpira wa miguu, mpira wa pete na kikapu.
“Tamasha hili limekutanisha wafanyakazi wa Idara na kampuni tofauti, imetusaidia kujenga mahusiano kati ya kampuni moja na nyingine, na mahusiano baina ya mtu na mtu.
“Kampuni ina watu wengi hivo siyo rahisi kuonana na kukutana, lakini kwa tamasha hili limeweza kutukutanisha pamoja kwa ajili ya kushauriana na kutengeneza urafiki”, alisema Irene

.jpeg)


No comments:
Post a Comment