JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


CEOrt, TWCC kushirikiana ushiriki wa wanawake katika kukuza uchumi wa biashara

Share This

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEO Roundtable of Tanzania-CEOrt) B. Santina Benson (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Dkt. Mwajuma Hamza  wasaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kushirikiana katika kuwawezesha wafanyabishara wanawake kukua kiuchumi kupitia mpango wa CEOrt unaojulikana kama ‘Think Equal, Lead Smart (TELS), ulioanzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation.Hafla hiyo imefanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Ijumaa Februari 6, 2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini (CEO Roundtable of Tanzania-CEOrt) B. Santina Benson (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) Dkt. Mwajuma Hamza, mara baada ya kusaini Hati za Makubaliano (MoU) kwa ajili ya kushirikiana katika kuwawezesha wafanyabishara wanawake kukua kiuchumi kupitia mpango wa CEOrt unaojulikana kama ‘Think Equal, Lead Smart (TELS), ulioanzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation. Hafla hiyo imefanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam Ijumaa Februari 6, 2026.

Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Sandra Oswald, akisisitiza  jambo wakati wa mwendelezo wa mkutano wa program ya Jukwaa la Watendaji Wakuu nchini ( CEO Roundtable of Tanzania- CEOrt)  inayojulikana kama ‘Think Equal, Lead Smart (TELS), ilioanzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, kwa lengo la kukuza usawa wa fursa kwa wanawake katika uongozi, biashara na nafasi za maamuzi.

Na Mwandishi Wetu
JUKWAA  la Wakurugenzi Wakuu Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania-CEOrt) na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) kwa pamoja wamesaini Hati ya Makubaliano (MoU) ili kurasimisha ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuharakisha uongozi na ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi hapa nchini.

Ushirikiano huo utatekelezwa kupitia mpango wa CEOrt unaojulikana kama ‘Think Equal, Lead Smart (TELS), ulioanzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na Vodacom Tanzania Foundation, kwa lengo la kukuza usawa wa fursa kwa wanawake katika uongozi, biashara na nafasi za maamuzi.

Kupitia ushirikiano huu, CEOrt na TWCC zitafanya kazi kwa pamoja kuimarisha biashara za wanawake ,ikiwemo biashara ndogo, ndogo sana na za kati (MSMEs)—kwa kuwajengea wanawake ujuzi wa uongozi, biashara na matumizi ya teknolojia za kidijitali, kuongeza utayari wa kukua kifedha, na kushughulikia vikwazo katika kijamii vinavyokwamisha maendeleo yao kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya utiaji saini iliyofanyika katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Bi. Santina Benson, alisisitiza umuhimu wa kushughulikia changamoto za kimfumo zinazoendelea kuzuia ushiriki kamili wa wanawake katika masuala ya kiuchumi na uongozi.

“Think Equal, Lead Smart imebuniwa kuunganisha wajasiriamali wanawake na mifumo ya sera, uwekezaji na uongozi na ushirikiano huu kati ya CEOrt na TWCC unaimarisha uwezo wetu wa kuwasaidia wanawake wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi katika mikoa mbalimbali na kuhakikisha wanawake wanajumuishwa kikamilifu katika mifumo ya maendeleo na uongozi wa Tanzania,” alisema .Santina

Hata hivyo alibainisha kuwa MoU hiyo itafungua njia za upatikanaji wa mitaji, masoko na ushauri wa kibiashara kupitia wanachama wa CEOrt na washirika wa kimkakati. Miunganisho hiyo inatarajiwa kuongeza fursa kwa wanawake kupata mitaji, kuingia katika minyororo ya thamani ya juu zaidi, na kunufaika na mwongozo wa kibiashara pamoja na mitandao ya sekta mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Dkt. Mwajuma Hamza, alisema kuwa ushirikiano huo unashughulikia changamoto halisi zinazowakabili wanawake wajasiriamali nchini.

“Wanachama wetu bado wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa mitaji, masoko, ushauri wa kitaalamu na nafasi za maamuzi. Ushirikiano huu na CEOrt unatoa fursa za vitendo kwa wanawake kujenga biashara endelevu, kupata nafasi za uongozi na kushindana kikamilifu katika uchumi,” alisema.

Ushirikiano huo ulitanguliwa na kikao cha kwanza cha maarifa cha Think Equal, Lead Smart, kilichowakutanisha viongozi wa biashara, washirika wa maendeleo, watunga sera na wanawake wajasiriamali jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kilifanyika katika Hoteli ya Serena chini ya kaulimbiu “Mustakabali wa MSMEs Zinazoongozwa na Wanawake: Ushirikishwaji, Changamoto na Fursa. Lengo ni kuwawezesha wanawake wajasiriamali kushiriki kikamilifu katika ajenda ya maendeleo ya muda mrefu chini ya Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 (DIRA 2050).

Jukwaa la TELS lilibuniwa kukuza ushiriki jumuishi wa kiuchumi kwa kuhimiza majadiliano kati ya sekta binafsi, taasisi za kifedha, watunga sera na MSMEs zinazoongozwa na wanawake. Kupitia ubadilishanaji wa maarifa na majadiliano yanayoongozwa na sera, mpango huu unalenga kuwaweka wanawake wajasiriamali kama wahimili muhimu wa mabadiliko ya kiuchumi nchini.

Akizungumza katika jukwaa hilo, Meneja wa Vodacom Tanzania Foundation, Sandra Oswald, alisisitiza umuhimu wa kujenga mifumo itakayowezesha biashara zinazoongozwa na wanawake kukua, kurasimishwa na kushindana kwa uendelevu.

“MSMEs zinazoongozwa na wanawake ndizo mhimili wa uchumi wa Tanzania, zikichangia kwa kiasi kikubwa ajira, kipato cha kaya na ubunifu wa ndani. Hata hivyo, bado zinakabiliwa na vikwazo vya kimfumo vinavyozuia ukuaji wao. Ili Tanzania ifikie malengo ya Dira ya 2050, wanawake wajasiriamali lazima wajumuishwe kikamilifu katika mkakati wa ukuaji wa uchumi wa taifa,” alisema.

Kikao hicho kilitoa fursa kwa wanawake wajasiriamali kueleza wazi changamoto wanazokumbana nazo, ikiwemo ukosefu wa mitaji nafuu, changamoto za matumizi ya teknolojia za kidijitali, vikwazo vya kisheria na kiutawala, upungufu wa masoko na mifumo dhaifu ya msaada wa biashara.

Sandra alieleza kuwa kuoanisha majadiliano ya TELS na Dira ya 2050 kunazitambua MSMEs zinazoongozwa na wanawake kama nguzo muhimu za mabadiliko ya kiuchumi, ubunifu na ukuaji jumuishi.

Ikiwa katika hatua kwanza katika mipango mbalimbali iliyopangwa katika utekelezaji wake, jukwaa la maarifa la Think Equal, Lead Smart litaendelea kuwakutanisha wadau kwa ajili ya kubadilishana mawazo yanayotekelezeka, suluhisho za vitendo na mikakati inayooana na sera za kitaifa. Vikao vijavyo vinatarajiwa kufanyika katika mikoa na sekta mbalimbali, vikisisitiza nafasi ya MSMEs zinazoongozwa na wanawake kama wachangiaji wakuu wa ustawi wa taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad