Na Mwandishi Wetu
MASHABIKI wa soka nchini Tanzania wanatarajiwa kushuhudia mchezo mkubwa wa kimataifa siku ya Jumamosi, tarehe 31 Januari 2026, ambapo klabu ya Young Africans SC (Yanga) itavaana na mabingwa wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly ya Misri, katika mchezo wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF).
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuanzia saa 10:00 jioni, ukiwa ni miongoni mwa michezo inayobeba hadhi kubwa barani Afrika kutokana na historia na ubora wa timu hizo mbili.
Kuelekea mchezo huo, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama limetangaza kuimarisha ulinzi kabla, wakati na baada ya mchezo huo ili kuhakikisha usalama na amani vinaendelea kutawala.
Jeshi la Polisi limetambua kuwa mchezo huo ni wa kimataifa na ni fursa muhimu ya kuitangaza na kujenga heshima ya Taifa, hivyo limeahidi kusimamia kikamilifu hali ya usalama ili kuzuia vitendo vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Kupitia taarifa iliyotolewa, Jeshi la Polisi limewahakikishia wananchi, wanachama, mashabiki na wapenzi wa soka kuwa wataendelea kushirikiana nao kuhakikisha mchezo huo unachezwa katika mazingira ya amani na usalama.
Aidha, wananchi na mashabiki wametakiwa kufika uwanjani mapema ili kuepuka msongamano, huku wakikumbushwa kuwa hairuhusiwi kuingia uwanjani na vitu hatarishi ikiwemo silaha au vifaa vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watu wengine.
Jeshi la Polisi pia limetoa onyo kali kwa mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kutumia mchezo huo kama fursa ya kufanya vitendo vinavyokiuka sheria, likisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivyo.
Vilevile, madereva wa vyombo vya moto wameonywa kutochukulia mchezo huo kama sababu ya kuvunja au kutotii sheria za usalama barabarani, kwani kutakuwepo na idadi kubwa ya askari wa usalama barabarani watakaosimamia utekelezaji wa sheria, na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, ambaye amewataka wananchi wote kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha mchezo huo unakuwa wa kihistoria na wa amani.



No comments:
Post a Comment