
Farida Mangube, Morogoro
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kuanza rasmi matumizi ya Mfumo Jumuishi wa Usimamizi wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani (IDRAS) kuanzia Februari 9, mwaka huu, mfumo ambao utaendesha huduma zake kwa saa 24 kwa siku.
Lengo la kuanzishwa kwa mfumo huo ni kuwa na mfumo mmoja jumuishi utakaosaidia kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi na kulinda haki za walipakodi, sambamba na kuboresha utunzaji wa kumbukumbu za kodi.
Akizungumza Mjini Morogoro wakati wa utoaji elimu ya mfumo huo kwa njia ya Redio Ofisa mwandaminzi wa usimamizi wa Kodi kutoka TRA Makao makuu Musa Otieno amesema IDRAS ni mfumo wa kisasa unaolenga kuboresha utoaji wa huduma kwa walipakodi.
Amesema mfumo huo utaongeza ufanisi, kuleta usawa na kuondoa usumbufu kwa walipakodi, kwani huduma zitapatikana kwa saa 24 kwa siku, siku saba za wiki.
Ameeleza kuwa mfumo huo utajumuisha huduma zote zilizokuwa zinapatikana kwenye mifumo mbalimbali ya TRA, ikiwemo usajili wa walipakodi, matumizi ya taarifa za kodi, ulipaji wa kodi, mawasiliano pamoja na usimamizi wa madai mbalimbali.
“Huu mfumo unakwenda kutenda haki kwa walipakodi kwa sababu utakuwa na taarifa nyingi zitakazotuwezesha kutoa makadirio sahihi. Pia utaungana na mifumo mingine, kwani una uwezo wa kuungana na mifumo zaidi ya 500; kwa kuanza tutaunganisha mifumo 60,” alisema Otieno
Aliongeza kuwa IDRAS utakuwa njia kuu ya mawasiliano kati ya TRA na walipakodi, ambapo barua zote zitawasilishwa na majibu kupokelewa kupitia mfumo huo. Aidha, mfumo huo umeunganishwa na mfumo wa forodha, hivyo kuwezesha ufuatiliaji wa bidhaa zilizouzwa, zilizobaki pamoja na mapato yaliyopatikana.
Mfumo huo pia utawezesha utunzaji bora wa kumbukumbu za walipakodi, akibainisha kuwa serikali imewekeza katika mfumo huo ili kuwawezesha walipakodi kufanya biashara zao kwa ufanisi bila kuonewa au kugandamizwa kutokana na ukosefu wa kumbukumbu sahihi.
Kwa upande wake,Olais Laizer Ofisa mwandaminzi wa usimamizi wa Kodi, amesema mfumo wa IDRAS unahusisha walipaji wa kodi za ndani, na kuwataka washauri wa kodi kuuelewa kikamilifu, akisisitiza kuwa matumizi ya mfumo huo ni jambo lisiloweza kuepukika kwa yeyote anayehitaji ufanisi katika masuala ya kodi




No comments:
Post a Comment