JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


SERIKALI YAWEKEZA KIMKAKATI SEKTA YA UZALISHAJI WA DAWA, YAANZISHA VITUO MAALUMU MLOGANZILA NA KIBAHA

Share This
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetangaza uwekezaji mkubwa wa kimkakati katika sekta ya uzalishaji wa dawa, ikiwemo kuanzishwa kwa vituo maalumu vya uzalishaji na utekelezaji wa sera zitakazohakikisha uwepo wa soko la uhakika kwa wazalishaji wa ndani watakaokidhi viwango vya kimataifa.
Akizungumza katika Jukwaa la Uwekezaji wa Uzalishaji wa Dawa Tanzania lililofanyika Dar es Salaam Januari 19, 2026, Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa, alisema Serikali imeamua kuifanya sekta hiyo kuwa kipaumbele cha kitaifa kutokana na mchango wake katika usalama wa afya, maendeleo ya viwanda na heshima ya taifa kimataifa.

“Uzalishaji wa dawa si mradi wa kawaida wa viwanda. Ni uwekezaji wa kimkakati katika afya ya wananchi, uchumi wa taifa na nafasi ya Tanzania katika mfumo wa kimataifa wa usalama wa afya,” alisema Waziri Mchengerwa.

Alieleza kuwa Serikali itaanzisha Vituo vya Uzalishaji wa Dawa (Pharmaceutical Manufacturing Hub Clusters) katika maeneo ya Mloganzila na Kibaha. Vituo hivyo vitafanya kazi kama mifumo jumuishi itakayowaunganisha wazalishaji, taasisi za udhibiti, miundombinu ya tafiti pamoja na huduma za usafirishaji, hatua itakayochochea ukuaji wa viwanda vya dawa nchini.
Kwa mujibu wa Waziri, mfumo wa ‘cluster’ umetumika kwa mafanikio katika nchi mbalimbali duniani na umeonekana kupunguza gharama za uzalishaji, kuharakisha taratibu za udhibiti na kusaidia viwanda kufikia na kudumisha viwango vya ubora vinavyotambulika kimataifa, ikiwemo WHO-GMP.

Katika kuimarisha mpango huo, Serikali imetangaza uwekezaji wa dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha Maabara ya Pamoja ya Dawa itakayohudumia vituo vyote viwili. Maabara hiyo itatoa huduma za upimaji wa ubora, tafiti za bio-equivalence na msaada wa kitaalamu katika masuala ya udhibiti wa bidhaa za dawa.

Hatua hiyo inalenga kupunguza vikwazo kwa wawekezaji, kuharakisha muda wa bidhaa kufika sokoni na kuhakikisha dawa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vya Shirika la Afya Duniani (WHO).

Kuhusu uhakika wa soko, Waziri Mchengerwa alisema Serikali itaweka mfumo wa sera utakaolinda na kukuza uwekezaji wa wazalishaji wa ndani mara tu watakapokidhi viwango vya kimataifa.

“Mara wazalishaji wa ndani watakapofikia viwango vinavyotambulika kimataifa, Serikali itaelekeza sera za manunuzi ya umma, kodi na udhibiti ili kuzipa kipaumbele bidhaa zinazozalishwa nchini zenye ubora unaokubalika,” alisema.

Alisisitiza kuwa lengo la Serikali si kuzuia uagizaji wa dawa kutoka nje ya nchi, bali kuhakikisha uagizaji huo hauathiri ushindani wa haki wala kudhoofisha uwekezaji wa ndani unaozingatia ubora.

Mpango huu unatekelezwa kupitia Kikosi Kazi cha Kuharakisha Uwekezaji wa Dawa (Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce – PIAT), ambacho kimeundwa mahsusi kuharakisha maamuzi ya uwekezaji katika sekta ya dawa. PIAT kinajumuisha viongozi waandamizi kutoka sekta za afya, fedha, biashara, uwekezaji, ardhi, nishati, udhibiti na manunuzi ya umma, na kina mamlaka ya kushughulikia vibali, leseni na masuala ya miundombinu kwa pamoja.

“Sekta ya dawa haiwezi kusubiri taratibu za kawaida. Kupitia PIAT, wawekezaji watapata maamuzi ya haraka, wazi na yanayotabirika,” alisema Waziri.

Sambamba na jukwaa hilo, Serikali imetoa wito kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa kuwasilisha maombi ya Expression of Interest (EOI) kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya, ambapo tarehe ya mwisho ya kuwasilisha maombi hayo ni Machi 2, 2026.

Serikali imesema mkakati huu unalenga kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi, kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma za afya, pamoja na kuiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa kitovu cha uzalishaji na usambazaji wa dawa katika Afrika Mashariki na bara la Afrika kwa ujumla.














 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad