Na Mwandishi Wetu

UWEKEZAJI wa fedha Sh..bilioni 280 unaofanywa na Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO ) katika vituo na njia za kusafirisha umeme, utaimarisha na kuleta utulivu wa upatikanaji wa umeme katika Jiji la Dar es Salaam.

Hayo yamesemwa leo Januari 6,2026 na Waziri wa Nishati Deo Ndejembi alipotembelea na kukagua transfoma mpya na mitambo ya kufua umeme katika vituo vya kupoza umeme vya Gongo la Mboto, Kinyerezi, Mabibo, Tabata Segerea na eneo la Chuo cha Usafiri.
“Dar es Salaam pekee kwa sasa inatumia megawati 750 kwa siku,mkoa wa Pwani unatumia megawati 100, matumizi yanayochangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za viwanda, hali iliyosababisha changamoto ya umeme kutokaa sawa.”

Akifafanua zaidi amesema mahitaji ya umeme yameongezeka kwa kasi na ndio maana Serikali imewekeza katika transfoma kubwa za kisasa zitakazosaidia kuwa na umeme wa uhakika kwa matumizi ya majumbani na viwandani,” amesema Ndejembi.
Amesema zilizowekwa katika vituo vya Gongo la Mboto na Kinyerezi zina uwezo mara tatu zaidi ikilinganishwa na transfoma zilizokuwepo awali, hatua itakayoongeza uthabiti wa umeme katika maeneo hayo.
Kuhusu kituo cha Mabibo, Waziri Ndejembi ameeleza kituo hicho ni muhimu kimkakati kwa kuwa awali jiji la Dar es Salaam lilitegemea kituo cha Ubungo kama kituo kikuu, lakini sasa Mabibo kitakuwa kitovu kikuu cha kupokea na kusambaza umeme, ikiwemo umeme kutoka Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere.
Waziri Ndejembi amesema lengo kuu la Serikali ni kuhakikisha wakazi wa Dar es Salaam wanapata umeme wa uhakika, huku kituo cha Mabibo kikitarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange, amesema mahitaji ya umeme yanaendelea kuongezeka na hivyo shirika hilo halitaki umeme kuwa kikwazo kwa biashara na ukuaji wa uchumi.“Tunataka umeme uendelee kuwa kiungo muhimu cha biashara na uchumi kwa ujumla.”
Hata hivyo amesema moja ya changamoto kubwa ni uharibifu wa miundombinu unaofanywa na baadhi ya watu wanaojihusisha na biashara ya vyuma chakavu. “TANESCO tumefanya vikao na viongozi wa Serikali za mitaa na tuna matumaini changamoto hiyo itapungua.





No comments:
Post a Comment