JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


WADAU WA MTANDAO WA VITUO VYA UBUNIFU NCHINI WAPONGEZWA.

Share This

 KATIKA kutambua mchango wa wadau waliochangia maendeleo ya ubunifu nchini, Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN), umeandaa hafla rasmi ya kuwapongeza wadau waanzilishi wa ubunifu sambamba na mkutano mkuu wa mwaka wa mtandao huo.

Akizungumza katia hafla hiyo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao huo, Bw. Kiko Kiwanga alisema mtandao huo ulioanzishwa mwaka 2020, unaunganisha vituo zaidi ya 62 Tanzania Bara na Visiwani kwa kujumuisha vituo vya ubunifu kutoka vyuoni, mashirika, vilivyo chini ya serikali na vituo binafsi.

“Siku ya leo ni siku maalumu sana kwetu, kwasababu tangu tulipoanza huu ni mkutano wetu wa kwanza wa mwaka ukianza tokea asubuhi ambako mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi wa Tume ya ICT, Dk.Nkundwe Mwasaga na sasa tunafanya kitu tofauti sana katika mtandao wetu katika kuwatambua wadau walioweka mchango mkubwa katika kuendeleza ubunifu na kufanya vituo hivi vinapiga hatua.

“Michango ya wadau hawa imekuwa ikitambuliwa kila mara, lakini leo kwa mara ya kwanza tunafanya hafla hii tukiwatambua wadau waanzilishi walioweka juhudi kubwa katika kuhakikisha wabunifu wachanga pamoja na biashara changa za ubunifu zinapiga hatua na kupata msaada katika mtandao wetu”, alisema Bw. Kiwanga.

Akizungumzia kuhusu Mtandao wa THN, mkurugenzi huyo alisema tokea umeanzishwa umekuwa mstari wa mbele katika kujenga mfumo wa ubunifu kwa kuviwezesha vituo vya ubunifu katika kuwasaidia wabunifu pamoja na wajasiriamali kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Tunatoa wito kwa serikali kama mtandao ambao tunawawezesha vijana waweze kufikia malengo yao katika masuala ya ubunifu na kuweza kuanzisha kampuni zao ambazo zina uwezo mkubwa wa kutoa ajira, kutatua changamoto mbalimbali katika jamii, kuona namna ya kuongeza uwekezaji ili kuwawezesha vijana waweze kufikia malengo yao ya kiubunifu”, akaongeza kuwa vituo hivi vya ubunifu vimefanya kazi kubwa katika kuwaandaa vijana kwani kuna wengine wanakwenda bila kuwa na wazo lolote, hivyo wanawezeshwa hadi kufikia mawazo halisi.

Akizungumza katika hafla hiyo, mmoja wa wadau wa ubunifu, aliyepokea tuzo katika hafla hiyo, Dk. Moses Ismail, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mratibu wa Ubunifu kupitia Kituo cha Ubunifu cha chuo hicho (UDICTI), alisema licha ya chuo kufanya mambo ya ufundishaji, utafiti, huduma kwa jamii, ushauri, huku ubunifu na ujasiriamali kwa miaka mingi ikifundishwa kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza, lakini mwaka 2010 kupitia ndaki hiyo, kilianzisha kituo cha ubunifu (UDICTI), ambacho lengo lake kubwa ikiwa ni kutoa mafunzo ya ubunifu kwa vitengo.

“Kituo kinatoa huduma ya eneo maalumu la kufanyia kazi, mafunzo maalumu kuhusu maarifa ya kutengeneza bidhaa za kiubunifu na kuunganishwa na wadau wa ubunifu watakaoweza kusaidia shughulia zao wanazozifanya.

“Ubunifu ni nyenzo muhimu sana katika maendeleo ya nchi na watu wake, kwani unasaidia kuongeza thamani ya bidhaa za ndani za kiubunifu, wengi tumekuwa watumiaji wakubwa wa bidhaa za nje, ndani tuna bidhaa mbalimbali za kiubunifu ambazo zinasaidia wanafunzi wetu kuwa sehemu ya wachangiaji wakubwa wa uzalishaji wa bidhaa hizi ambazo baadae zinakuwa makampuni na kusaidia kuongeza ajira hasa kipindi hiki ambacho tunataka vijana wetu wanaotoka vyuoni wawe nguzo muhimu katika utengezezaji ajira badala ya kuajiriwa”, alisema Dk. Ismail.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA), Bw. Godfrey Nyaisa akizungumza katika hafla hiyo aliwataka wabunifu hususani wenye biashara changa kujitokeza kusajili biashara zao Brela ili pamoja na mambo mengine waweze kupata miongozo mbalimbali itakayowawezesha kufanya shughuli zao za kiubunifu kwa ufanisi huku akitoa changamoto kwa Mtandao wa THN kuhusisha mamlaka za kiserikali katika utendaji wao wa kila siku.



Ukiwa na dira ya kuimarisha ushirikiano, kutoa rasilimali, na kuchochea ubadilishanaji wa maarifa miongoni mwa wanachama wake, THN pia inashirikiana na Tume ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICTC) kuimarisha mazingira ya ubunifu na kuhamasisha uanzishwaji wa vituo vya ubunifu katika mikoa mbalimbali.


Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN), Dk. Irene Shubi Isinika, akizungumza katika hafla ya kuwapongeza wadau waanzilishi wa ubunifu iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa THN, jijini Dar es Salaam jana. Tokea kuanzishwa kwake Mwaka 2020, THN imekuwa mstari wa mbele katika kujenga mfumo wa ubunifu katika kuviwezesha vituo vya ubunifu na kuwasaidia wabunifu pamoja na wajasiriamali kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN), Dk. Irene Shubi Isinika (kulia), akikabidhi tuzo ya heshima kwa Meneja wa Mradi wa Funguo unaoendeshwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Bw. Joseph Manirakiza, kwa kutambua mchango wake katika maendeleo ya nyanja ya ubunifu nchini. Ilikuwa ni katika hafla ya kuwapongeza wadau wa ubunifu iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa THN, jijini Dar es Salaam jana.

Mhadhiri Mwandamizi wa Ndaki ya Teknolojia za Habari na Mawasiliano ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mratibu wa Ubunifu kupitia Kituo cha Ubunifu cha chuo hicho (UDICTI), Dk. Moses Ismail (kushoto), akipokea tuzo iliyotolewa na Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN), kutoka kwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Westerwelle Tanzania, Isaack Shalo katika hafla iliyoandaliwa na THN jijini Dar es Salaam jana, ili kuwatambua wadau waanzilishi waliochangia maendeleo ya ubunifu nchini.

Meneja wa Uendelezaji wa Biashara Changa wa Benki ya CRDB, Bi. Sharon Nsule (kulia), akikabidhi tuzo iliyotolewa na Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN), kwa Bi. Esther Kimario kutoka Chanya Change ya mjini Arusha, aliyeipokea kwa niaba ya kituo cha Apps and Girls kwa kutambua mchango wao kama ‘kituo cha kwanza cha ubunifu cha wanawake’ katika hafla iliyoandaliwa na THN jijini Dar es Salaam jana, ili kuwatambua wadau waanzilishi waliochangia maendeleo ya ubunifu nchini.




Viongozi wa Mtandao wa Vituo vya Ubunifu Tanzania (THN), wabunifu, wawakilishi wa vituo vya ubunifu na wageni mashuhuri, wakionesha ubunifu wao wa kupozi mbele ya wapigapicha, mara baada ya hafla ya kuwapongeza wadau waanzilishi wa ubunifu nchini, iliyofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa Mwaka wa THN, jijini Dar es Salaam jana.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad