JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


VIONGOZI WA DINI, WANASIASA NA VIONGOZI WA SERIKALI ACHENI KUTOA MATAMKO SUBIRINI MATOKEO YA TUME, MCHUNGAJI MASHIMO

Share This

WITO umetolewa kwa viongozi wa dini na serikali kuacha kutoa matamko kufuatia matukio yaliyotokea Oktoba 29, badala yake wasubiri matokeo ya tume iliyoundwa kuchunguza tukio hilo.

Wito huo umetolewa leo Disemba 23,2025 Jijini Dar es salaam na Mchungaji Daud Mashimo wakati akizungumza na waandishi wa habari.

"Ni muhimu kwa taifa kujipa muda wa kutafakari na kusubiri majibu ya mamlaka husika ili kuepusha kuchochea hisia na migawanyiko miongoni mwa wananchi, akisisitiza kuwa amani na utulivu ndio msingi wa mshikamano wa Taifa",Amesema.

Akizungumza kwa hisia, mchungaji huyo amewataka viongozi wa dini za madhehebu yote kusimama pamoja na kuwa sauti ya faraja kwa Watanzania, badala ya kuendelea kufufua maumivu ya matukio ya nyuma ambayo yanaweza kuzaa chuki na mpasuko wa kijamii.

Katika hotuba yake, Mashimo amempongeza Katibu wa Baraza la TEC, Padre Kitime, kwa mchango wake mkubwa katika kulijenga taifa kupitia maneno ya busara na faraja, akisema amekuwa sauti muhimu kwa Watanzania na kwa upande wa serikali katika nyakati ngumu.

“Mungu akubariki sana Padre Kitime kwa maneno yako ambayo yamekuwa faraja kwa wengi. Umekuwa mtumishi mwaminifu na sehemu ya baraka kwa taifa letu,” alisema Mashimo huku akisisitiza umuhimu wa viongozi kuzungumza kwa nia njema.

Aidha, alirejea kauli za baadhi ya wazee na viongozi waliowahi kuzungumzia kwa uchungu matukio ya chaguzi zilizopita, akisema ni vyema sasa taifa likaelekeza nguvu katika kuponya majeraha na kujenga upya matumaini ya wananchi.

Mashimo amebainisha kuwa serikali imeonyesha juhudi za kutafuta suluhisho kwa kuunda tume ya uchunguzi, hivyo akashauri jamii isubiri matokeo yake kabla ya kutoa hukumu, na endapo majibu hayatakuwa ya kuridhisha, ndipo wananchi watumie njia sahihi kutoa maoni yao.

"Taifa linaelekea kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, niwatake viongozi wa dini, wanasiasa na viongozi wa serikali kuhubiri amani, utulivu na upendo ili sikukuu hiyo iwe mwanzo wa kuzaliwa upya kwa mshikamano wa kitaifa",Amesema Mashimo.

Mchungaji Mashimo Amesisitiza kuwa hakuna serikali iliyo kamilifu, lakini kwa umoja na maombi, Watanzania wanaweza kulilinda taifa lao, akiwataka waandishi wa habari kufikisha ujumbe huo kwa wananchi ili kuendelea kuitunza amani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad