Na Avila Kakingo, Michuzi TV
HALI ya uwekezaji nchini imeendelea kuimarika kwa kasi, ambapo ndani ya kipindi cha miaka minne pekee, idadi ya miradi ya uwekezaji imeongezeka kwa zaidi ya mara tatu huku mitaji ikiongezeka kwa takribani mara nne, kwa mujibu wa takwimu rasmi za Serikali kwa mwaka 2025.
Akitoa taarifa ya hali ya uwekezaji kwa mwaka 2025, leo Desemba 30, 2025, Bagamoyo Mkoani Pwani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema kuwa kuanzia mwaka 2021 hadi kufikia Disemba 29, 2025, miradi iliyosajiliwa imeongezeka kutoka miradi 252 hadi miradi 915, sawa na ongezeko la zaidi ya asilimia 260.
Kwa upande wa mitaji, Prof. Mkumbo amesema uwekezaji umeongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 3.7 mwaka 2021 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 10.95 mwaka 2025, hali inayoifanya Tanzania kuendelea kuvunja rekodi ya usajili wa miradi na mitaji kila mwaka.
Ameeleza kuwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 29, 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) ilisajili jumla ya miradi 915 yenye thamani ya USD milioni 10,954.08, miradi ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 161,678 katika sekta za viwanda, ujenzi na usafirishaji.
Katika mgawanyo wa umiliki wa miradi hiyo, miradi 284 inamilikiwa na Watanzania, miradi 442 na wawekezaji wa kigeni, huku miradi 182 ikiwa ya ubia kati ya Watanzania na wageni, hali inayoonesha kuimarika kwa ushiriki wa wazawa katika shughuli za uwekezaji.
"Takwimu zinaonesha kuwa Tanzania kwa sasa ina jumla ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi na EPZ 34, yakiwemo yanayosimamiwa na TISEZA (16), Serikali za Mitaa (4), mashirika ya umma (2) na sekta binafsi (12)." Amesema
Kupitia programu ya EPZ na SEZ pekee kwa mwaka 2025, Serikali ilisajili miradi 20 yenye thamani ya USD milioni 243.17, inayotarajiwa kuzalisha ajira 4,822 na mauzo ya nje yanayokadiriwa kufikia USD milioni 227.43. Miradi hiyo imetekelezwa katika mikoa saba ikiwemo Pwani, Mtwara, Iringa, Ruvuma, Njombe, Kilimanjaro na Lindi, huku wawekezaji wakitoka katika nchi zaidi ya nane ikiwemo China, Uingereza, India, Marekani na Tanzania.
Katika kuimarisha mazingira ya uwekezaji, Prof. Mkumbo amesema Serikali imeanzisha Kituo cha Huduma za Mahala Pamoja chenye taasisi 14 ndani ya jengo moja, hatua iliyopunguza kwa kiasi kikubwa urasimu na muda wa kupata vibali, huku matumizi ya mifumo ya TEHAMA yakiwezesha cheti cha uwekezaji kutolewa ndani ya saa 24.
Ameongeza kuwa Serikali imezindua na kuendeleza SEZ tano za kimkakati zenye ukubwa unaozidi hekta 1,700, ikiwemo Buzwagi (1,333 ha) na Bagamoyo Eco Maritime City (151 ha). Kuanzia Agosti 2025, jumla ya wawekezaji 60 walionesha nia ya kuwekeza katika maeneo hayo, ambapo tayari wawekezaji watano wamekabidhiwa maeneo Bagamoyo, ikiwemo mradi wa kuunganisha magari wenye thamani ya USD milioni 50 unaotarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 1,000.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Benki ya Ardhi ya TISEZA kwa sasa inamiliki zaidi ya hekta 170,176 za ardhi isiyo na migogoro kwa ajili ya uwekezaji wa jumla na maeneo maalum ya kiuchumi, hatua inayochochea utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Akizungumzia mwelekeo wa mbele, Prof. Mkumbo amesema Serikali imelenga kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 15 na kusajili angalau miradi 1,500, hususan katika sekta za kilimo na uchakataji, nishati, madini, viwanda, TEHAMA, utalii, mafuta na gesi.
Amehitimisha kwa kuwataka Watanzania kuendelea kulinda amani na mazingira bora ya uwekezaji, akisisitiza kuwa takwimu hizo zinaonesha wazi kuwa uwekezaji ni nguzo muhimu ya ajira, mapato ya Serikali na ukuaji wa uchumi wa taifa.
Matukio mbalimbali wakati akitoa taarifa ya hali ya uwekezaji kwa mwaka 2025, leo Desemba 30, 2025, Bagamoyo Mkoani Pwani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.



.jpeg)


No comments:
Post a Comment