Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Salome Nelson Mnyawi, amewataka wadau wa maendeleo na wakazi wa eneo hilo kwa ujumla kumtanguliza mbele na kujali maslahi ya Mirerani.
Salome ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya kata hiyo (WDC).
Ameeleza kwamba wakazi wa Mirerani na wadau wa maendeleo kwa ujumla wanapaswa kujitoa kwa moyo mmoja katika kuhakikisha Mirerani inapiga hatua katika maendeleo.
"Mirerani tunapaswa kuwa na dhamira ya dhati ya kuona Mirerani inapiga hatua za maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo, kwani hakuna mjomba wa kutusaidia," amesema Salome.
Amesema viongozi, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla wakishirikiana kwa umoja wataweza kuongeza tija katika kufanikisha maendeleo.
Hata hivyo, Diwani mstaafu na mdau wa maendeleo Justin Nyari ameunga mkono hoja hiyo kwa kusisitiza umuhimu wa wananchi na wadau wote kujali na kulinda maslahi ya Mirerani.
"Maendeleo ya Mirerani yanahitaji ushirikiano, uwajibikaji na uzalendo wa kila mmoja wetu, ni wakati sasa wananchi na wadau wote wa Mirerani kuweka mbele maslahi ya Mirerani kabla ya maslahi binafsi," amesema Nyari.
"Hoja ya Mhe Diwani ni ya msingi sana na inapaswa kuungwa mkono na kila mwenye nia njema na Mirerani," ameeleza Nyari.
Mdau mwingine wa maendeleo Lekaita Lekaita amepongeza Diwani Salome kwa uongozi wake thabiti, wa mfano na wenye maono makubwa unaogusa moja kwa moja maisha ya wananchi.
"Wewe ni kiongozi jasiri, mchapakazi na mwenye moyo wa kizalendo, anayejali kwa dhati maendeleo ya watu wake na maslahi ya Mirerani kwa ujumla," ameeleza Lekaita.
"Kwa kweli, wana Mirerani walipopata uongozi wako walipata zawadi ya kipekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wewe ni lulu adimu, kiongozi wa kipekee ambaye wananchi wa Mirerani wanapaswa kujivunia siku zote," amesema Lekaita.
"Uongozi wako umejengwa juu ya misingi ya uwajibikaji, uadilifu na maamuzi yenye maslahi mapana ya jamii, hali inayozidi kuimarisha imani ya wananchi kwako na kuleta matumaini mapya ya maendeleo endelevu ya Kata ya Mirerani," amesema.
Amesema kutokana na uongozi bora wa Salome na wa mfano, ni wazi kuwa viongozi wanawake kama Salome wanaendelea kumwakilisha vyema Rais Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
"Hongera sana Mhe Salome na kwa uhakika tutaendelea kukuunga mkono daima ili uweze kutimiza ndoto yako ya kuiona Mirerani ya maendeleo zaidi unayotamani iwe siku zote,tuko nyuma yako kukuombea na kukuunga mkono, Mirerani ya Salome Nelson Mnyawi , Mirerani ya Maendeleo kwa wote," amesema.


No comments:
Post a Comment