
Na Avila Kakingo, Michuzi Tv
SERIKALI ya Awamu ya Sita imeeleza kwa kina mwelekeo wake wa kuwawezesha vijana kiuchumi na kijamii, ikisisitiza kuwa vijana ni mhimili mkuu wa maendeleo ya Taifa na lazima wawe katikati ya ajenda ya ajira, uzalishaji, ujuzi na matumizi ya teknolojia.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, Mheshimiwa Joel Nanauka wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 23, 2025.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, viongozi wa Serikali na watendaji wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Waziri Nanauka amesema dhamira ya Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha vijana wanafikiwa walipo, wanasikilizwa kwa makini na wanashirikishwa kikamilifu katika kujenga mustakabali wa Taifa.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni takribani milioni 20.6, sawa na zaidi ya asilimia 55 ya nguvu kazi ya Taifa, hali inayolazimisha Serikali kuweka mikakati ya makusudi ya kuwawezesha ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Waziri alisema mwelekeo huo unaendana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa kufungua Bunge la 13 Novemba 14, 2025, akisisitiza kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya ajira, ujuzi, uzalishaji na matumizi ya teknolojia kwa vijana ili wanufaike na uchumi wa sasa na wa baadaye.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2025–2030, inayolenga kuzalisha ajira zenye tija zisizopungua milioni nane ndani ya miaka mitano kupitia uzalishaji, uwekezaji na kukuza sekta zenye fursa kubwa kwa vijana.
Katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana, Waziri Nanauka alibainisha kuwa Serikali inashughulikia masuala ya ukosefu wa ajira, ajira zisizo rasmi zisizo na tija, upungufu wa ujuzi unaohitajika sokoni, pamoja na changamoto ya mitaji kwa vijana wajasiriamali na kampuni changa zenye ubunifu (startups).
Amesema Serikali inaendelea kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 (Toleo la 2024), inayobainisha maeneo 13 ya kipaumbele ikiwemo elimu na ufundi stadi, ubunifu, uchumi wa kidijitali, ajira, afya na ustawi, malezi na makuzi, usawa wa kijinsia, mazingira na ujumuishwaji wa vijana wenye ulemavu.
Kwa upande wa ajira, Waziri amesema Serikali inaendelea kuimarisha mifumo ya ajira ndani na nje ya nchi, programu za mafunzo kazini (internship na attachment), pamoja na kuongeza ajira kupitia sekta za kilimo-biashara, madini, uvuvi na viwanda kwa lengo la kuongeza thamani na ajira katika mnyororo mzima wa uzalishaji.
Serikali pia inaweka msisitizo katika kuanzishwa kwa mifumo ya dhamana ya mikopo (credit guarantee schemes) ili kuwasaidia vijana wanaokosa dhamana kupata mitaji, sambamba na kusimamia utekelezaji wa kanuni za ununuzi wa umma zinazotenga asilimia 30 ya bajeti kwa makundi maalum yakiwemo makampuni ya vijana.
Aidha, Waziri Nanauka amesema Serikali inaandaa jukwaa la kidijitali la huduma jumuishi kwa vijana (Youth Digital One Stop Platform) litakalowaunganisha vijana na taarifa za ajira, mafunzo, masoko na fursa za kifedha kwa njia rahisi na ya haraka.
Alibainisha pia kuwa Serikali itaendelea kuvifufua vituo vya maendeleo ya vijana vya Sasanda (Songwe), Ilonga (Morogoro) na Marangu (Kilimanjaro) ili kutoa ujuzi wa vitendo, nidhamu, uzalendo na stadi za ujasiriamali, pamoja na kuanzisha programu maalumu ya Open Coding School kwa ajili ya kukuza ujuzi wa TEHAMA.
Akihitimisha, Waziri Nanauka ametoa wito kwa vijana wa Tanzania kuwa wazalendo, wachapakazi na wenye nidhamu, huku akizitaka vyombo vya habari kushirikiana na Serikali katika kuelimisha, kuhamasisha na kujenga ushiriki chanya wa vijana katika maendeleo ya Taifa.
“Kauli mbiu yetu ya Vijana Tuyajenge, Tanzania ni Yetu ni wito wa vitendo. Vijana ni suluhisho na nguzo ya maendeleo ya Taifa letu,” amesema.


No comments:
Post a Comment