JIACHIE

Karibuni Jamvini Wanajamii

Tangaza Hapa

Post Top Ad


PWANI YAWEKA MKAKATI KUACHA TABASAMU KWA WANANCHI NDANI YA SIKU 100 ZA RAIS

Share This

Na Mwamvua Mwinyi, Pwani Disemba 19, 2025

Mkoa wa Pwani umejipanga kuhakikisha wananchi wa mkoa huo wananufaika moja kwa moja na utekelezaji wa ahadi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya siku 100, kwa lengo la kuacha tabasamu na kuboresha huduma muhimu za kijamii.

Akizungumza katika kikao cha tathmini kilichofanyika Disemba 18,2025 ukumbi wa Mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa mkoa huo Abubakar Kunenge, alisema wameshaanza kazi, wapo vizuri . 

Kunenge alisema yapo maeneo mengine ambayo wanahitaji kuongeza kasi na nguvu, ikiwemo eneo la Bima ya Afya kwa wote, ili kuhakikisha lengo linafikiwa kwa wakati na kuleta tija kwa wananchi.

Aliongeza kuwa mkoa umeamua kufanya uhakiki wa kina katika maeneo mbalimbali ili kubaini wananchi wenye uhitaji halisi wa bima ya afya, kwa lengo la kupata takwimu sahihi na kuhakikisha hakuna anayeachwa. 

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali, akieleza kuwa mifumo ya taarifa inapaswa kuoanisha ili kurahisisha utendaji badala ya kila taasisi kuwa na mfumo wake. 

Mratibu wa Bima ya Afya kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Silvery Maganza, akitoa wasilisho alieleza kuwa kaya zitakazonufaika na mpango huo ni zile zisizo na uwezo wa kiuchumi zipatazo 900,000, zikiwemo kaya zinazonufaika na mpango wa TASAF.

Alibainisha , utekelezaji wa siku 100 za ahadi za Rais ni wa majaribio, ukianza na makundi maalum yakiwemo watoto, wazee, watu wenye ulemavu na wasio na uwezo, kwa lengo la kutathmini changamoto na maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya utekelezaji wa kudumu.

Meya Manispaa ya Kibaha, Dkt. Mawazo Nicas alieleza, Manispaa hiyo imejipanga, imeshaanza kazi katika sekta ya afya na elimu ambapo milioni 900 zimetengwa kujenga madarasa elimu ya sekondari na milioni 400 ununuzi wa madawati. 

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, alipata fursa ya kusalimia kikao hicho na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kwa utendaji wenye kasi na mwelekeo mzuri wa kuwahudumia wananchi.

Aliwataka wataalamu kuwa wabunifu katika ukusanyaji wa takwimu sahihi za watu wenye mahitaji, akisisitiza kuwa elimu ya kweli ni uwezo wa kufikiri nje ya box ili kupata matokeo chanya.

“Tufungwe na matokeo ya huduma kwa wananchi, Tuwahudumie watu, Mheshimiwa Rais alisema anataka aache tabasamu kwa Watanzania, hivyo tumsaidie kulipeleka tabasamu hilo ndani ya siku 100 za ahadi zake,” alisisitiza Simbachawene.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani alimshukuru Waziri Simbachawene kwa ujio wake na kwa maelekezo na mwongozo alioutoa katika kuhakikisha ahadi za Rais zinatekelezwa kwa ufanisi.





No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad