TAASISI ya Taifa ya Usafirishaji (NIT) imetakiwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu ya mafunzo maalumu ili kuzalisha rasilimali watu yenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya kisasa na changamano ya sekta ya usafirishaji.Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Superdoll, kampuni tanzu ya Super Group, Jamal Bayser, wakati Kongamano la wahitimu (Convocation) lililofanyika jijini Dar es Salaam leo Desemba 17, 2028 ambapo wanafunzi waliofanya vizuri walipewa zawadi mbalibali.
Akizungumza mbele ya wahitimu, wahadhiri na wadau wa sekta ya usafirishaji, Bayser alisema mabadiliko ya kasi katika sekta ya lojistiki yanahitaji mfumo wa elimu unaojumuisha nadharia na vitendo kwa kiwango cha juu zaidi.
Aidha ameipongeza NIT kwa “mchango mkubwa na wa kuigiwa mfano” katika maendeleo ya sekta ya usafirishaji na uchumi wa taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa mshikamano kati ya darasani na maeneo ya uzalishaji ni msingi muhimu wa maendeleo ya nchi.
“Kampuni yetu inaendeleza mawasiliano ya karibu na uongozi wa taasisi ili kuhakikisha mitaala inakwenda sambamba na mahitaji halisi ya viwanda,” alisema Bayser.
“Tumejizatiti kutoa fursa zaidi kwa wahitimu kupata uzoefu wa vitendo ambao mara nyingi hukosekana katika elimu ya nadharia pekee. Lengo ni kuhakikisha mhitimu anapomaliza masomo, siyo tu ana maarifa, bali yuko tayari kuajiriwa au kijiajiri na kufanya kazi.”
Akijibu wito huo wa sekta binafsi, Mkuu chuo cha NIT, Dkt. Prosper Mgaya, alieleza dira na mkakati wa ukuaji wa taasisi hiyo, akisisitiza kuwa NIT siyo tena kituo cha kujifunzia pekee, bali ni kitovu cha ubunifu na uendelezaji wa teknolojia.
Alibainisha kuwa miradi ya wanafunzi inayobuniwa wakati wa masomo sasa itapitia tathmini ya kina ili kuboreshwa na kutekelezwa kama suluhisho linaloweza kuleta tija kibiashara au kijamii.
Dkt. Mgaya pia alifafanua mgawanyo wa majukumu kati ya NIT na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) katika masuala ya usalama barabarani na uthibitishaji wa madereva.
“ Jukumu letu kubwa ni kuwafundisha madereva kwa kiwango cha juu cha umakini na taaluma, ili wahitimu wakiwa na uelewa kamili wa kazi yao,” alisema Dkt. Mgaya.
“ Wanapohamia LATRA, ndipo mamlaka hiyo hufanya tathmini za kiutendaji kama ufuatiliaji wa muda wa kuendesha ili kudhibiti uchovu. Sisi tunazalisha ubora; wao wanasimamia utekelezaji.”
Sehemu muhimu ya majukumu ya sasa ya NIT ni kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu ya serikali.
Dkt. Mgaya alieleza kuwa taasisi hiyo kwa sasa inaandaa idadi kubwa ya madereva kwa ajili ya mfumo wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
“ Serikali imetukabidhi jukumu nyeti la kuwaandaa madereva kwa ajili ya upanuzi wa mradi wa BRT. Kwa kutarajiwa kuingia mabasi mapya zaidi ya 500 barabarani, tunahakikisha idadi inayolingana ya madereva wenye ujuzi wa hali ya juu inakuwepo ili kuyaendesha kwa usalama na ufanisi,” aliongeza.
Kongmano hilo pi lilipambwa na ujumbe wa hamasa na ulezi wa kitaaluma kutoka kwa Edith Kisamo, mhandisi wa kwanza mwanamke wa ndege nchini Tanzania.
Baada ya kuanzia ngazi ya chini na kufanikiwa kupata leseni ya kimataifa, Kisamo aliwahimiza wahitimu kufikiria ushindani wa kimataifa.
“Ujuzi wa kitaaluma haukui wenyewe baada ya kuhitimu darasani,” alionya Kisamo.
“Tupo hapa kutoa malezi ya kitaaluma na ramani za mafanikio zitakazowawezesha wahitimu hawa kuwa na ushindani wa kimataifa. Dhamira yangu ni kuhakikisha wanafuata njia sahihi za kitaaluma ili wahandisi wa Kitanzania watambulike kama wataalamu wa kiwango cha dunia.”
Sherehe hizo zilihitimishwa kwa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali ili kuhakikisha NIT inaendelea kuwa kitovu kikuu cha ubora wa usafirishaji Afrika Mashariki.
.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)

.jpeg)



No comments:
Post a Comment